Wajumbe wa  Baraza  Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa, wakipiga kura kupitisha Azimio la  kuongeza muda wa vikwazo vya silaha na vikwazo vinginevyo  kwa makundi ya waasi yanayoendelea kuleta vurugu na machafuko katika  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mojawapo ya  kundi la waasi linalobanwa na Azimio hilo  ni lile la M23 ambalo hivi karibuni limetwaa  mji wa Goma. Muda huo wa vikwanzo umeongezwa hadi februari Mosi 2014. Baraza hilo pia limesisitiza kwamba,  mtu yoyote au taasisi  inayojihusisha na kulisaidia  kundi  hilo la M23 kuacha mara moja la sivyo nao watakabiliwa na vikwazo vikiwamo vya kutosafiri na kusitishwa kwa mali zao. 


 Na Mwandishi Maalum
Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa , limepitisha kwa kauli moja azimio linaloongeza muda   wa vikwazo vya silaha na vikwazo vingine dhidi ya vikundi vya waasi ambavyo  viko  katika  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo  (DRC)
Azimio hilo  nambari 2078 ( 2012) linaelezea pia haja ya  kuongeza vikwazo vya ziada kwa uongozi  na wapiganaji wa  kundi la waasi la M23, kundi ambalo hivi karibuni lilichukua  Jimbo la Goma.
Baraza Kuu  la Usalama  ambalo lilikutana siku ya Jumatano  limeongeza muda  huo wa vikwazo hadi  Februari Mosi mwaka 2014.
Vikwazo dhidi ya  silaha viliwekwa kwa mara ya kwanza mwaka  2003 mara baada ya kumalizika kwa vita vya mara kwa mara nchini DRC, vita ambavyo  vimedumu   kwa miaka mitano na kukadiriwa kuua zaidi ya watu  milioni tano.
Vikwazo vya silaha vimekwa dhidi ya makundi yenye silaha  na ambayo si sehemu ya  Jeshi la pamoja la Serikali au  Polisi na pia vinahusu vikwazo ya kusafiri na usitishwaji wa mali za   watu au taasisi ambazo zinakiuka vikwazo hivyo.
Azimio hilo pia linalaani vikali kundi la waasi la M23, kundi ambalo linahusisha  wanajeshi walioasi kutoka jeshi la kitaifa la DRC mwezi wa Aprili mwaka huu. Kundi   ambalo kwa sasa linashikilia Goma, ambao ni  Mji  Mkuu wa  Kivu ya Magharibi.
Baraza Kuu linalitaka kundi hilo la M23 na makundi mengine, kuacha  mara moja aina zote za mapigano au vitendo vinavyosababisha uvunjifu wa amani.
Aidha Baraza kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa limeagiza na kurudia tena  kusitishwa  mara moja kwa misaada ya aina yoyote kutoka nje inayoelekezwa kwa kundi la M23.
Kama hiyo haitoshi,  Baraza  Kuu la Usalama limeelezea nia yake ya  kupanua wigo wa vikwazo siyo tu kwa  viongozi wa M23 bali pia kwa yeyote yule ambayo kwa namna moja ama nyingine analisaidia kundi hilo la M23 au anakiuka vikwazo.
Wakati huo huo, Baraza Kuu la usalama pia limemwomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kuliongezea muda   Kikundi cha  Wataalamu  kuhusu DRC, hadi   February Mosi mwaka 2014 ili kiweze kufuatilia  utekelezaji wa  vikwazo hivyo.
Katika hatua nyingine,  Umoja  wa Mataifa, umemtuma Mshauri wake Mkuu kuhusu masuala ya Kijeshi,  Jeneral Babacar Gaye kwenda katika nchi za Maziwa Makuu ambako atakutana na kufanya majadiliano na wadau mbalimbali kuhusu masuala kadhaa yaliyojiri  hivi karibu wakati wa mkutano wa  Viongozi wa Nchi za Maziwa Makuu ( ICGLR).
Masuala  hayo ni pamoja na  utekelezaji wa kilomita 20 za  Ukanda Huru ( Neutral  Zone )eneo ambalo M23 litatakiwa kuondoka, na dhana ya  kuwa na Jeshi  la Kimataifa lisilofungamana na upande wowote. ( International Neutral Force).


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...