Salamaleko Ankal Michuzi na Timu nzima ya Globu ya Jamii.

Ama baada ya salamu,naomba unipandishie kwenye Globu ya Jamii hoja yangu hii kuhusiana na utaratibu wa ulipiaji wa maegesho ya magari katika Uwanja wa Ndege wa zamani (Terminal 1) jijini Dar es Salaam.

Maana hivi karibuni nilikuwa nimeenda uwanjani hapo kumsindikiza ndugu yangu,nilipofika getini nikamkuta jamaa kakaa kwenye kiti huku akiwa ameshika kamba iliyokuwa kwenye chuma lililokuwa limefunga njia na nilipokaribia kwenye chuma lile,jamaa huyo akanyanyuka kwenye kiti chake na akaja dirishani na kunipatia kikadi hicho pichani (si kama kule Terminal 2 ambako tunachukua kwenye mashine) kwa ajili ya kuonyesha muda wa kuegesha gari katika Maegesho ya uwanjani hapo,nikamuuliza kuwa na huku mnachukua ushuru wa Maegesho ya magari?akanijibu ndio na gharama zake ni kama zile za kule Terminal 2.

Sikuwa na maswali mengi zaidi,nikachukua kikadi hicho na kuendelea na safari yangu.

Nilifika sehemu nikaegesha gari na kwenda na yule ndugu yangu mpaka sehemu ya kukata tiketi na baada ya kupata,tukakaa kidogo kupiga stori mbili tatu wakati tukisubiri muda wa safari yake ukaribie ili tuweze kuagana na mie niondoke zangu.

Baadae muda wa safari ukawadia kwa ndugu yangu na mie ndio ukawa muda muafaka wa kuondoka uwanjani hapo,kabla sijaelekea kwenye gari nikakumbuka kuwa nilipewa kikadi cha Maegesho ya gari na hapo ndipo nilipo papasa macho kushoto na kulia ili nione sehemu ya kulipia na kwa bahati nzuri nilikiona kibanda kidogo cheupe (picha ya chini) chenye bango la njano linalotoa maelezo kuwa ni sehemu ya kulipia maegesho hayo.
Nikaenda mpaka pale na kumkuta mwanadada mrembo mwenye tabasamu la kumtoa nyoka pangoni,nikampatia kile kikadi nae akakiangalia na kuniambia natakiwa kulipia shilingi elfu tatu (3,000/=) kwa hesabu alizozipiga kupitia kalukuleta iliyokuwepo mezani pale.

Nikatoa noti ya Shilingi elfu tano nikampatia na yeye akanirudishia shilingi elfu mbili na hicho kikadi akiwa amekiandika tu na peni muda wa kuondoka.

Hapo ndipo nilipomuuliza yule dada kuwa Risiti iko wapi??akanijibu kuwa bado hawajaanza kutoa risiti katika maegesho ya uwanja huo.Nikamuuliza tena inamaana watu wote mnawafanyia hivi,akanijibu ndio wanafanya hivyo toka wameanza kutoza ushuru katika sehemu hiyo.

Sasa hapo ndipo nilipopatwa na Maswali mengi kichwani kuwa hela inayotozwa katika maegesho hayo inakwenda wapi??na inafayiwa kazi gani??na kwanini utaratibu wao ni mbovu namna hiyo?? na maswali mengine mengi bila ya majibu.

Nikaona isiwe shida nikaondoka zangu na leo ndio nimeona nikuletee wewe Ankal ili uiweke kwenye Libeneke letu la Globu ya Jamii ili wadau waweze kuchangia maoni yao na ikiwezekana swala hili lifanyiwe kazi na kuondoa kabisa mambo hayo yanayoendelea katika Maegesho hayo.

Ahsante.

-Mdau wa Globu ya Jamii
Jijini Dar.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 13 mpaka sasa

  1. Hiyo ndiyo bongo yetu watu wanajilia kilainilaini tu,sasa unamlipa mtu hakuna risiti na hiyo airport authority hovyo tu.Hizo pesa za parking zingefanya mambo mengi tu.Na kwanza wameanza sikunyingi kulipisha watu wangekuwa hawaweki hizo pesa mifukoni mwao,hiyo huduma ingekuwa iliboresha sikunyingi sana.

    ReplyDelete
  2. risiti lazima upewe, inakuwaje waanze service bila kuwa na risiti!!haikubaliki!!huo ni wizi wa mchanaaaaa kweupe!!wabongo jamani tutafika kweli!!!

    ReplyDelete
  3. WIZI MTUPU!

    Kwa taswira halisi ya hiyo Risiti huku tukizingatia Sheria ya Kodi kuanzia mwaka 2008 ni kuwa Malipo yeyote 'Halali' ni lazima yawe na FISCAL RECEIPT (Yaani Stakabadhi ya Malipo ya Digitali iliyochapwa kutoka kwenye Mashine iliyosajiliwa na Mamlaka ya Kodi-TRA).

    Ni jambo la kustaajabisha na aibu kubwa kabisa kwa Mamlaka kubwa kama Uwanja wa na Kutoa Risiti Holela (zisizo maalum) bila kutoa Stakabadhi zilizosajiliwa na Mamlaka ya Kodi !

    Moja kwa moja ni kuwa Fedha zinazokusanywa hapo zinaibika kirahisi kabisa!

    ReplyDelete
  4. Ahhh Bongo Tambarale!

    Hizo Risiti za Uwanja wa Ndege tena wa Kimataifa hazina Tofauti na zile za kwenye Vizuizi vya Vijijini ambako Halmasahauri za Wilaya zinakusanya ushuru kwa kutoza ada kwa kuhesabu magunia ya mikaa na kuhesabu idadi ya kuku majike na majogoo katika Matenga kutoka gari hadi gari!

    ReplyDelete
  5. Ohhh!

    Hiyo ni Saccos au nini?

    Hao wasimamizi wa Makusanyo ya hizo fedha usije shangaa ndio wanaojenga Mabaa na Maghorofa hapa Jijini!

    ReplyDelete
  6. Kuna watu wanachafua sana nchi yetu na kwa kweli wanaleta aibu kubwa sana.wahusika wameona na ninadhani watashughulika swala hili na mengineyo kama mtu kukulipisha parking kwa risiti ambazo haziaminiki maeneo ya kariakoo na posta na ninashangaa sijui TRA kazi yao nini hivi hadi zama hizi wanashindwa kuwabana hao wawe na machine maalum za TRA? Nchi yetu ni nzuri lakini wababaishaji ni wengi na hasa ukienda ubungo bus terminal ndio unaweza hata kutapika...!!mambo yanaenda tu kiholelaolela utadhani nchi wenyewe wamehama..na ukishangaa utakuta gari lako limetiwa pingu ukiuliza ooh hapo zinapaki taxi tu..!aah mi nishachoka jamani!!

    ReplyDelete
  7. SIO SALAMALEKO, NI

    ASALAAM ALEYKUM.

    Mpango wa kutoza magari ushuru wakati wa kuingia uwanjani Terminal ONE ulishawahi kusitishwa na Waziri husika nimemsahau yupi, baada ya kuonekana na kugundulika kuwa hayo mapato yalikuwa hayaonekani yanakokwenda, maana huduma muhimu na za msingi uwanjani zilikuwa zikizidi kuzorota.
    Kilichojitokeza ni hao wahudumu hususan wa kike kuanza kuvaa dhahabu kwa wingi.
    Kama kawaida yetu waTZ, huwa hatuna ngoma ya kukesha, yule waziri aliyesitisha utozwaji kiingilio bila shaka alishaondoka na ule mzuka akaondoka nao. Lakini kwa wakati ule wote tulishangilia na kumshukuru ndugu waziri maana aliyoyasema yaliingia akilini.

    ReplyDelete
  8. Ulaji huo.

    Wabongo basi tena kwa kufikira ulaji. Kama mpango wao ulikuwa haujakamilika kwa nini walianzisha kulipisha?

    Elfu tatu hiyo ina maana ulikaa kwa masaa mangapi?

    TRA mupooooooo? Fedha yetu ya kodi inakwenda mifukoni kwa watu hiyo.

    ReplyDelete
  9. Ni wizi tu!kwa kuwa hakuna risiti basi pesa zingine zinaingia mfukoni mwao!

    ReplyDelete
  10. Si kweli kama watu wanatozwa Maripo ya kuegesha magari pasipo kupewa risiti ! Jambo hili ni la uongo kwasababu terminal one kuna machine inayoitwa physical machine kutoka Tanzania revenue authority (T.R.A) nakama kunamtu anabisha aende akadhibitishe uwepo wa machine hizo za kutolea risiti !!!! Nawaomba wadau muwe makini sana katika kutoa hoja kama hizi katika jamii !

    ReplyDelete
  11. Mdau wa 10 hapo juu Anony Mon Jan 14, 11:28:00 pm 2013

    ....!!!!Nawaomba wadau muwe makini sana katika kutoa hoja kama hizi katika jamii!

    SASA WEWE KWA AKILI YAKO HIYO RISITI HAPO JUU NI NDIO HIYO YA TRA?

    UMEANDIKA KINYUME CHAKE AU MAHALA HAPO PENYE WIZI PANA MJOMBA WAKO UNAMFICHIA AENDELEE NA WIZI?

    KWA TAARIFA YAKO HAPO NDIO MSALA UMESHA CHANIKA MWAMBIE MJOMBA WAKO ATAFUTE GENGE LA BAMIA NA DAGAA PIA AKAE MKAO WA TAYARI KUFUKUZWA KAZI NA KUBURUZWA KATIKA SHERIA KWA WIZI WA UMMA!

    ReplyDelete
  12. Mdau wa 10 hapo juu Anony Mon Jan 14, 11:28:00 pm 2013

    ....!!!!Nawaomba wadau muwe makini sana katika kutoa hoja kama hizi katika jamii!

    Bora umejileta mwenyewe wakuone unavyotetea ujinga!hivi mtu na akili yako unakuja humu kutuambia hiyo risiti iliyoandikwa kwa mkono ni ya TRA au ya mjomba ako?hebu badilikeni jamani na muwe na aibu!

    ReplyDelete
  13. Inavyoonekana kuna baadhi ya wadau wanachangia maada pasipo kujua kipi wanakiongelea ! Iyo picha ya hapo juu Siyo risiti ya T.R.A. kama mnavyo dhani nyinyi ! Hiyo pichani ni card inayotolewa getini wakati wa kuingia na huwa inaandikwa time in namuda wakutoka cashier anakuandikia time out pamoja na kukugongea muhuli wa cashier ambapo utapewa card yako pamoja na risiti halali ya T.R.A. utaenda kumuachia mtu wa geti la kutokea ! Hiyo card kamailivyo hapo juu kwenye picha na mtu wagetini ataichukua card yako na kukufungulia ili utoke ! Huo ndio utaratibu uliopo terminal one nasikama mnavyofikiri wadau ! Naomba mlifanyie kazi kabla ya malalamiko .!! Ahsanteni..!!!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...