Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Khamis Suedi Kagasheki atakuwa
mgeni rasmi katika siku ya kilele cha maadhimisho ya Kumbukizi ya vita vya Maji
Maji na Utalii wa Utamaduni yatakayofanyika Songea mkoani Ruvuma Februari 27
mwaka huu.
Maadhimisho hayo
ya siku tatu ambayo kitaifa yameandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Mkoa wa Ruvuma yatafunguliwa
tarehe 25 Februari katika Makumbusho ya Vita vya Majimaji mjini Songea.
Madhumni ya
maadhimisho hayo ambayo hufanyika kila mwaka ni kuwakumbuka mashujaa 67 walionyongwa
tarehe 27 Februari 1906 walipokuwa katika harakati za kupinga ukoloni wa
Mjerumani. Baadhi ya mashujaa hao ambao wote
walizikwa katika kaburi moja ni Ndugu Mputa Gama, Songea Mbano, Mpambalyoto
Soko na MajiyaKuhanga Komba.
Katika siku tatu za maadhimisho wananchi na wadau mbalimbali wa utalii
watapata fursa ya kutembelea na kujionea utajiri wa vivutio vya utalii ulioko Kusini
mwa Tanzania hususan Mkoa wa Ruvuma ili waweze kuongeza uelewa na kushiriki
kuvitangaza vivutio hivyo.
Aidha, Wizara itaendesha mdahalo Februari 25 katika Club ya Songea ili
kutoa nafasi kwa wadau wa malikale na utalii kujadili namna bora ya kutumia
fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii Kusini mwa Tanzania.
Wananchi wote wa mkoa wa Ruvuma, na
nchini kote kwa ujumla, wanakaribishwa kuhudhuria maadhimisho hayo ya Kumbukizi ya vita vya Maji Maji na Utalii wa Utamaduni.
G. Matiko
MSEMAJI
WIZARA
YA MALIASILI NA UTALII
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...