Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mheshimiwa Peter Kallaghe mwishoni mwa wiki iliyopita (Jumamosi, 23 na Jumapili, 24 Machi 2013) alitembelea baadhi ya shughuli za miradi mbalimbali zinayofanywa na Watanzania waishio Leicester and Northampton kwa lengo la kufahamu mafanikio na changamoto zao.

Akisindikizwa na Afisa wa Ubalozi, Bw. Amos Msanjila, Balozi alipenda kufahamu nini mahitaji ya Watanzania hao ili kuweza kujenga mkakati muafaka wa kuwatia moyo na kuwashirikisha wananchi hao kujenga nchi.

Akiwa Leicester alipata fursa ya kutembelea kituo cha redio ya jamii ya mji huo na kufanyiwa mahojiano ya moja kwa moja kwa Kiswahili na Mtangazaji wa redio hiyo, Bw. Omar Hussein. Redio hiyo inasikika moja kwa moja katika maeneo yote ya Leicestershire na vitongoji vyake.

Aidha Balozi Kallaghe alitembelea kiwanda kidogo cha usindikaji wa vyakula na viungo kinachomilikiwa na mfanyabiashara mwenye asili ya Tanzania cha Jalpur Millers. Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho Bw. Deepen J. Pau alimwambia Balozi kwamba Kampuni yao ina mipango ya kuwekeza zaidi Tanzania.

Baadae Mheshimiwa alitembelea kituo cha kuratibu usafirishaji wa mizigo mbalimbali kwa makontena kwenda nchi za Afrika Mashariki na hasa Tanzania. Pamoja na kuonyeshwa shughuli mbalimbali zinazofanyika hapo, Balozi alipata pia fursa ya kuzungumza na wajasiliamali Bw. Abdul Nasser Hamed wa Zanzibar Driving School na Mussa Issa Mussa wa BMA Store and Shipping Agency.

Alipata pia fursa ya kutembelea mgahawa wa biriyani wa Maalim Hamis na kukutana na mpishi huyo maarufu kabla ya kukutana na Watanzania wachache, hasa viongozi wa Jumuiya ya Watanzania ya Leicester.

Siku ya Jumapili Balozi alitembelea Jambo Hair Salon na baadae kukutana na viongozi wa watanzania wachache kwenye Mgahawa wa Kass’s Grill unaomilikiwa na kijana wa kitanzania Kasongo Mohamed. Pamoja na kupata chakula cha mchana kwenye mgahawa huo, Mheshimiwa alifanya na mazungumzo na watanzania hao na kusisitiza umuhimu wa mshikamano na moyo wa kuunga mkono biashara za watanzania wenzao.

Mheshimiwa ataendelea kutembelea miji mbalimbali hapa Uingereza na kujionea shughuli zinazofanywa na Watanzania kila atakapopata fursa ya kufanya hivyo.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Balozi Kallaghe anaendelea kuonyesha uongozi ktk diaspora ya Watanzania, tafadhali tumuunge mkono na tumshirikishe ktk uwezo tulio nao ktk kufanya shughuli zetu.

    Tusimfiche pale tunapo kwama na tunadhani tunahitaji msaada ka manufaa ya Watanzania.

    MAINA A. OWINO

    ReplyDelete
  2. hiyo ni mifano kidogo tu ya project za watanzania hapa UK, wengi wako tayari kupeleka project na idea zao TZ lakini bado serikali yetu inakataa kuondosha kigugumizi cha urai wa nchi mbili. Majirani zetu wameshaanza kupeleka project zao nyumbani na mafanikio kwa pande zote mbili yashaanza kuonekana.

    ReplyDelete
  3. Hongera sana Mhe.Peter Kallaghe kwa kazi nzuri!

    ReplyDelete
  4. Balozi ameonyesha mfano mzuri sana kwa uamuzi wake wa kufanya ziara za mikoani hapa uingereza na kukutana na wafanyabiashara wa kitanzania hatuna budi kushirikiana naye kwa karibu ili kuweza kuwakirisha zile changamoto zinazotukabili ili tuweze kuvutiwa na uwekezaje wa hapa na kule nyumbani

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...