Na Profesa Mbele
Sisi tuliosoma sekondari miaka ya sitini na kitu tunaikumbuka picha ya Chinua Achebe inayoonekena hapa kulia. Ndio picha iliyokuwepo kwenye jalada, upande wa nyuma wa kitabu cha Things Fall Apart. Kwa bahati nzuri, ninayo nakala ya miaka ile ya Things Fall Apart. Niliipata miaka ya karibuni, nikaona niwe nayo, angalau kujikumbusha enzi za ujana wetu. Ninazo pia nakala za matoleo ya hivi karibuni, lakini ile ya zamani niliiona kama lulu.

Kuanzia mwaka 1966 hadi 1970 nilikuwa mwanafunzi wa sekondari, seminari ya Likonde. Wakati huo riwaya ya Things Fall Apart ilikuwa maarufu. Tulivijua pia vitabu vya watoto ambavyo Achebe alikuwa ameandika. Navikumbuka viwili: The Sacrificial Egg and Other Short Stories na Chike and the River. Shule yetu ilikuwa na maktaba kubwa na nzuri sana. Nidhamu ya kusoma ilikuwa kali, chini ya usimamizi wa mapadri waliokuwa waalimu wetu.

Miaka ile ile, Achebe alichapisha riwaya ya No Longer at Ease na Arrow of God na A Man of the People. Tulikuwa tunamsoma Achebe sambamba na Cyprian Ekwensi. Baadhi ya vitabu vya Ekwensi ambavyo tulivisoma ni Burning Grass, na People of the City na Jagua Nana. Hao wawili walikuwa kama mafahali wawili kutoka Nigeria katika uwanja wa uandishi.

Katika seminari ya Likonde, mwalimu wangu wa ki-Ingereza alikuwa Padri Lambert Doerr OSB, m-Jerumani, ambaye sasa ni askofu mstaafu pale Peramiho. Sidhani kama nimewahi kukutana na mtu anayesoma vitabu kama yeye. Alituwekea amri kwamba tusome angalau kitabu kimoja cha hadithi ya ki-Ingereza kwa wiki. Kitabu kimoja ilikuwa ni kiwango cha chini, lakini usikae wiki bila kumaliza angalau kitabu.

Padri Lambert alikuwa na mtindo wa kugawa daftari kwa kila mwanafunzi ambamo tulipaswa kuelezea kuhusu vitabu tulivyosoma, au ambavyo tulidai tumesoma. Wakati wowote alikuwa anaitisha daftari lako, ili akusikie ukimweleza habari ya kitabu chochote ulichokiorodhesha humo. Kumdanganya ilikuwa haiwezekani, wala huthubutu. Matokeo ya hayo ni kuwa kila mmoja wetu alisoma vitabu vingi sana, na ufahamu wetu wa ki-Ingereza ulikuwa mkubwa kabisa. Achebe, kwa uandishi wake wa kuvutia, alichangia kwa kiasi kikubwa kutufanya tupende kusoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Insipiring piece. Asante mzee wet.
    You can tell idea aliyokuwa anatumia mwl wenu ya kusoma, kurecord na kuadithia story baadae how helpful that was na actually ni staili wanayotumia walimu kunzia kindergarten level mfano hapa CANADA NA INAWASAIDIA KWELI WATOTO. I wish shule zetu TZ wangetumia pia style hiyo. Tatizo KUBWA hata maktaba mashuleni na vitabu ni sawa na hakuna.....

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...