Kuwepo ama kutokuwepo madarakani kwa Mwenyekiti wa klabu ya Simba Ismail Aden Rage kutaamuliwa na Kamati ya  Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji inayoongozwa na Wakili Alex Mgongolwa.
Afisa habari wa Shirikisho la soka Tanzania TFF Boniface Wambura amesema leo kuwa wamepokea barua kutoka uongozi wa Simba ikielezea kutotambua mkutano ulioandaliwa na wanaodaiwa kuwa wanachama wake uliofanyika jana kwenye  ukumbi wa Starlight, jijini Dar es salaam  huku wakimwondoa madarakani mwenyekiti wao.

Wambura alisema katika barua hiyo uongozi wa Simba umeahidi kuitisha mkutano wa wanachama wake na Mkutano huo utaitishwa na Mwenyekiti wa Simba kwa mujibu wa katiba ya klabu hiyo.

"Kutokana na hali hiyo, TFF imeitisha mara moja kikao cha Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji kinachoongozwa na Wakili Alex Mgongolwa kwa ajili ya kutoa mwongozo kwa matukio ya aina hiyo na ndio utatoa maamuzi yake kama chombo cha mwisho"alisema Wambura.

Hata hivyo Mwenyekiti wa muda wa mkutano uliomwondoa madarakani Rage Mohamed Wandi amesisitiza kuwa wameandaa muhtasari kwa ajili ya kuupeleka kwa msajili wa  vyama ili kuthibitisha uhalali wa katiba iliyotumika kumwengua Mwenyekiti huyo.

Jana wanachama wasiopungua700 kwa pamoja walifanya mkutano katika hotel ya Starlight na waliafiki kumwengua madarakani Mwenyekiti wao Rage kutokana na mwenendo mbaya wa timu.
Akizungumza jijini jana Wandi ambae aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa muda wa mkutano ulioitishwa na wanachama alisisistiza  pamoja na kauli ya Rage ya kugomea kujiondoa madarakani lakini msimamo wao upo pale pale wa kutomtambua kama Mwenyekiti na badala yake asiendeshe klabu kwa matakwa yake bali ni kwa maslahi ya Simba.

"Amesema tunajifurahisha lakini ukweli sisi tunafahamu  vyema Katiba ambayo inaruhusu wanachama wasipopungua 500  ibara ya 22( 2) wanauwezo wa kufanya mkutano ndani ya siku30 kama ambavyo tumefanya sisi,kwanza asiendeshe klabu kama sultani atambue sisi ni wanachama hai ambao tumekamilika na ndio maana kwa azimio moja tumeafikiana hivyo,"alisema Wandi.
Alisema wameandaa muhtasari ambao watauwasilisha kwa msajili wa vyama lengo ni kutaka kupata ukweli juu ya matumizi ya katiba iliyotumika katika mkutano huo na watauwasilisha wakati wowote kuanzia sasa.

Jana Rage alikaririwa akizungumza kwa njia ya simu akitokea India ambapo alipinga maamuzi yaliyofikiwa na wanachama hao huku akifananisha mkutano huo kama kikao cha harusi na kudai bado anajitambua kama Mwenyekiti na atakaporejea ndipo atatoa maamuzi yake mwenyewe kwa kuitisha mkutano mkuu wa wanachama wa klabu hiyo ya wekundu wa Msimbazi haujafanyika.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. wanachama hai 700 waliokutana na kupitisha maamuzi sio jambo la mzaha!mwelekeo wa simba sio mzuri na hauridhishi kwa ujumla!ifike mtu atambue kwamba Jua limezama,wanachama na wapenzi wa simba wanataka "delivery" ya uongozi bora na thabiti utakao toa mafanikio na ushindi,na sio blabla!soka sio siasa,hakuna ushindi na wewe huna chako,kaa pembeni ili wenye upeo nao waongoze!nao pia wakishindwa,watalazimika kukaa pembeni,hakuna kubebana hapa!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...