Daktari bingwa wa macho kutoka China akimfanyia uchunguzi mtoto Fatuma
juma Mzee wa kijiji cha Uzini walipofika kutoa tiba na uchunguzi kwa
wagonjwa mbalimbali,huko katika kituo cha Afya Uzini Wilaya ya
Kati Unguja.
Daktari bingwa kutoka China akimdadisi mgonjwa Madari Mgezu bada ya
kumueleza matatizo yake yanayo msumbua walipofika kutoa tiba na
uchunguzi kwa wagonjwa mbalimbali,huko katika kituo cha Afya Uzini
Wilaya ya Kati Unguja.
Badhi ya wagonjwa waliofika katika kituo cha Afya Uzini wakisubiri
kuonana na Madaktari bingwa wa China uliofika kutoa tiba na
uchunguzi,huko katika kituo cha Afya Uzini Wilaya ya Kati Unguja.
Timu ya Madaktari bingwa kutoka China wakiwa na wenzao wa Zanzibar
wakiwa katika picha ya pamoja,huko uzini Wilaya ya Kati Unguja.Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
========= ======= ======
Madaktari wa Kichina watoa huduma vijijini Zanzibar.Na Salum Vuai-Maelezo Zanzibar 16/03/2013..
WANANCHI
wa mbalimbali wa Wilaya ya Kati Unguja, wameelezea kuridhishwa kwao na
huduma za uchunguzi wa kiafya na tiba zinazotolewa na madaktari wa
kujitolea kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
Wakizungumza
na gazeti hili jana wakati wataalamu sita wa magonjwa mbalimbali kutoka
China wakitoa huduma hizo katika kituo cha afya Uzini, wananchi hao
walisema, mpango huo ni mzuri kwani unawapunguzia mzigo wa kufuata
huduma mjini na kuchukua muda mrefu wakiwa nje ya vijiji vyao.
Hamad
Juma, mkaazi wa Mgenihaji, alisifu ubora wa huduma zinazotolewa na
madaktari hao, na kusema tiba zao ni mjarabu kwnai zimemsaidia sana
kupata nafuu matatizo ya macho yanayomkabili.
“Kwa
muda sasa nimekuwa nikitibiwa na madaktari kutoka China katika
hospitali kuu ya Mnazimmoja badaa ya kuchomwa jichoni na kitu chenye
ncha kali, na leo wamekuja hapa nami nimefuata sawa zaidi”,
alifahamisha.
Naye
Mtumwa Jabu Khamis, aliyempeleka mtoto wake mwenye matatizo ya kifua,
alisema hatua hiyo ni muhimu na inafaa ifanyike kila kipindi kifupi ili
kuwafikia wananchi walio wengi na ambao hawana uwezo wa kufuata huduma
hizo mjini.
Akizungumzia
ujio wa madaktari hao, Sheha wa shehiya ya Uzini Vuai Mgeni Vuai,
alisema utaratibu unaofanywa na madaktari hao kupitia Wizara ya Afya,
unawapa faraja wananchi wa vijijini, kwa kuwaondoshea usumbufu wa
maradhi yaliyoficha na hatimaye kupatiwa tiba.
Alitoa
wito kwa wananchi wanapopata taarifa za kufikiwa na madaktari bingwa wa
maradhi mbalimbali, wasipuuze kwenda kufanyiwa uchunguzi, kwani huenda
wakawa wanaishi na maradhi ambayo hayajajitokeza.
“Siku
hizi kuna maradhi mengi, mengine hatuyajui mpaka tuchunguzwe, hivyo ni
vyema kunapokuwa na huduma kama hizi, wananchi wafike ili kuchunguzwa na
kuelezea matatizo ya kiafya waliyonayo ili yawahiwe mapema”,
alisisitiza Sheha huyo.
Mapema,
kiongozi wa timu ya madaktari hao Dk. Lu Jian Lin, alisema mpango huo
unaofadhiliwa na Serikali ya China, unalenga kuwasaidia wananchi wa
Zanzibar kuimarisha afya zao ili waweze kushiriki shughuli mbalimbali za
kiuchumi.
Alieleza
kuwa, serikali ya nchi yake inatambua uhaba wa madaktari unaozikabili
hospitali na vituo vya afya vilivyoko vijijini, hivyo imeamua kwa
makusudi kuandaa programu hiyo ya kupeleka huduma katika maeneo hayo
Unguja na Pemba.
Aliwashauri
wananchi kuchukua tahadhari ili kujiepusha na maradhi mbalimbali, kwa
kula chakula bora, kufanya mazoezi ya mwili na kujenga utamaduni wa
kuchunguza afya zao kila baada ya kipindi maalum.
Zaidi
ya wananchi 250 kutoka shehia mbalimbali za Wilaya ya Kati, walipatiwa
huduma hizo kwa kupimwa na kutibiwa maradhi ya macho, pua, kifua,
masikio magonjwa ya akinamama na ya mifupa.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...