*Azindua Tume ya watu 15, aipa wiki sita kukamilisha kazi
 WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amezindua Tume maalum aliyoiunda ili ifanye uchunguzi wa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyotangazwa Februari 18, mwaka huu na kuwataka wajumbe wa Tume hiyo watafute kiini cha mserereko wa kushuka kwa ufaulu kuanzia mwaka 2010 hadi 2012.
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Jumamosi, Machi 2, 2013) wakati akizungumza na wajumbe wa Tume hiyo kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni, jijini Dar es Salaam. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
“Nimetafuta takwimu za tangu mwaka 2005, Serikali ya Awamu ya Nne ilipoingia madarakani na kubaini kuwa tangu wakati huo hadi mwaka 2009 tulikuwa tukifanya vizuri, lakini kuanzia mwaka 2010 hadi 2012 matokeo yamekuwa yakishuka sana,” aliwaambia wajumbe wa Tume hiyo na waandishi wa habari waliohudhuria uzinduzi huo.
Alisema hali hiyo haikuwa kwenye shule za sekondari za umma (kata) peke yake bali hata kwa shule za Serikali, za watu binafsi na kwenye seminari ambazo kwa miaka mingi zimekuwa na sifa ya kufanya vizuri kuliko shule za kawaida.
Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema: “Mwaka 2005 kiwango cha ufaulu kilikuwa asilimia 89.3; mwaka 2006 asilimia 89.12; mwaka 2007 asilimia 90.6; mwaka 2008 asilimia 83.6 na mwaka 2009 asimilia 72.5, hapa napo tulikuwa bado tuko vizuri japo si sana ikilinganishwa na miaka mine iliyotangulia.”
“Lakini mwaka 2010, kiwango cha ufaulu kilishuka na kufikia asilimia 50.4, mwaka 2011 kilipanda kidogo na kufikia asilimia 53.6 na kilishuka zaidi mwaka jana ambapo kilifikia asilimia 34.5. Hapa ni lazima mtu utapata maswali ya msingi na kujiuliza nini kimetokea katika miaka ya hivi karibuni,” alisema.
Waziri Mkuu alibainisha kwamba idadi ya watahiniwa iliongezeka kutoka 85,292 mwaka 2005 na kufikia 248,336 katika mwaka 2009 wakati idadi ya walimu nayo pia iliongezeka kutoka 20,414 na kufikia 37,218 katika kipindi hichohicho.
Alisema anatambua changamoto nyingine zinazoikabili sekta ya elimu kama vile uhaba wa vitendea kazi, upungufu wa maabara na walimu wa sayansi, upungufu wa mabweni pamoja na nyumba za walimu.
Kinachoshangaza, Waziri Mkuu alisema, mbali na kuongezeka kwa walimu kutoka 44,053 mwaka 2010, walimu 55,982 (mwaka 2011) na kufikia walimu 68,784 mwaka 2012 bado kiwango cha ufaulu nacho kilikuwa kikishuka katika kipindi hichohicho.
Akitoa mfano, Waziri Mkuu alisema: “Kwenye shule za kata, mwaka 2010, walifaulu wanafunzi 114,883; mwaka 2011 wanafunzi 106,286 na mwaka 2012 wanafunzi 74,817 wakati kwenye shule za Serikali, katika kipindi hicho hicho ufaulu ulishuka kutoka wanafunzi 19,412, na kufikia wanafunzi 10,712.”
Waziri Mkuu alisema katika mchanganuo huo, jambo moja kuu lililo bayana ni kuwepo kwa mzao wa kwanza wa shule za kata katika mwaka 2010 lakini bado athari za kushuka kwa ufaulu zikasambaa kote hadi kwenye shule za serikali, za binafsi na seminari.
Akianisha kushuka kwa ufaulu wa daraja la kwanza katika makundi hayo, Waziri Mkuu alisema: “Mwaka 2010, kwenye shule za kata, walifaulu wanafunzi 1,225 wakati mwaka 2011 walikuwa wanafunzi 564 na mwaka 2012 walikuwa wanafunzi 162”.
“Kwenye shule za Serikali, mwaka 2010, walifaulu wanafunzi 952, mwaka 2011 wanafunzi 771 na mwaka 2012 wanafunzi 253. Kwenye shule za binafsi, mwaka 2010, walifaulu wanafunzi 2,476 mwaka 2011 wanafunzi 1,614 na mwaka 2012 wanafunzi 1,032. Kwenye seminari, mwaka 2010, walifaulu wanafunzi 695, mwaka 2011 wanafunzi 428 na mwaka 2012 wanafunzi 197.”
Akianisha matokeo ya waliofeli kwa kupata daraja ‘0’, Waziri Mkuu alisema: “Mwaka 2010, kwenye shule za kata, walifeli wanafunzi 151,848 wakati mwaka 2011 walifeli wanafunzi 143,552 na mwaka 2012 walifeli wanafunzi 223,774”.
“Kwenye shule za Serikali, mwaka 2010, walifeli wanafunzi 7,926, mwaka 2011 wanafunzi 9,790 na mwaka 2012 wanafunzi 16,176. Kwenye shule za binafsi, mwaka 2010, walifeli wanafunzi 13,346 mwaka 2011 wanafunzi 16,620 na mwaka 2012 wanafunzi 25,055. Kwenye seminari, mwaka 2010, walifeli wanafunzi 638, mwaka 2011 wanafunzi 972 na mwaka 2012 wanafunzi 1,329.”
Alisema kwa  mujibu wa hadidu za rejea, wajumbe wa tume hiyo watatakiwa kuangalia ni sababu zipi zimechangia kuwepo kwa matokeo hayo mabaya, mserereko wa kushuka umekuwa ukiongezeka kwa sababu gani, usimamizi katika Halmashauri ukoje, ukaguzi wa elimu na uhamishiwaji wa sekta ya elimu kwenye Wizara ya TAMISEMi umechangiaje kushuka kwa kiwango cha ufaulu.
Vilevile, watatakiwa kuangalia mitaala na mihutasari ikoje, kuangalia uwiano uliopo kwenye mitihani inayotungwa ikiwa ni pamoja na uhakiki wa mitihani hiyo; kuangalia mazingira ya kufundishia, mfumo wa upimaji, usimamizi na uendeshaji, na kutokuwepo kwa chakula shuleni kunachangiaje kushuka kwa utendaji mbaya wa wanafunzi katika masomo yao.
Tume hiyo yenye wajumbe 15, imepewa muda wa wiki sita kuanzia Machi mosi iwe imekamilisha kazi hiyo na kuwasilisha taarifa yao kwa Waziri Mkuu. Itaongozwa na Prof. Sifuni Mchome wa Tume ya Vyuo Vikuu, na Makamu wake atakuwa Bi. Bernadetha Mushashu (Mbunge wa Viti Maalum – Kagera).
Wajumbe wengine ni Bw. James Mbatia (mbunge wa Kuteuliwa), Bw. Abdul J. Marombwa (Mbunge wa Kibiti), Prof. Mwajabu Possi (Chuo Kikuu - UDSM), Bibi Honoratha Chitanda (CWT) na Bibi Daina Matemu (TAHOSSA) na Bw. Mahmoud Mringo (TAMONGSCO).
Wengine ni Bw. Rakhesh Rajani (TWAWEZA), Bw. Peter Maduki (CSSC), Mwl. Nurdin Mohamed (BAKWATA), Bw. Suleiman Hemed Khamis (Baraza la Wawakilishi), Bw. Abdalla Hemed Mohamed (Chuo Kikuu – SUZA), Bw. Mabrouk Jabu Makame (Baraza la Elimu Z’bar na Bw. Kizito Lawa (Taasisi ya Kukuza Mitaala)
    
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P 3021,
DAR ES SALAAM.
JUMAMOSI, MACHI 2, 2013.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 20 mpaka sasa

  1. Michuzi leo urushe...usinibanie maoni yangu:

    Kiini kinaanzia kwa mawaziri wenyewe. Kama naibu waziri hajui Tanzania ni muungano wa nchi gani (Mulugo=Tanganyika na Zimbabwe), je mwanafunzi atatoa wapi jibu!

    Kama waziri hajui kutamka mwaka 1964 kwa Kiingereza (anasema "One Nineteen Sixty Four'), je mwanafunzi atajuaje!?

    ReplyDelete
  2. Kiini cha kuanguka kwa elimu ni mfumo wenu wa kusomesha na wakutoa mtihani. Hebu tokeni nje na waanagalieni wenzenu wanvyosomesha.
    1) Watu wanahifadhi tu huku. Hakuna anaelewa. Sababu? Walimu waliyochoka mbaya. Yaani hawajui lolote.

    2) KUsoma ili kufaulu "syndrome". Maradhi haya yanamsababisha mwanafunzi kuanza kuhifadhi vitu bila ya kuelewa.

    3) Ondoeni upumbavu wa NECTA. Mnakaa huko mnatunga masuala magumu ambayo mwanafunzi hata hajawahi kuona hiyo topic. Halafu manakaa mkisema, loh! mibunju imefeli. Kumbe nyie ndo majumbu.

    Now, after giving my opinion, I know for sure that this government will not do anything about it. Because that's how we are. We just don't care.

    ReplyDelete
  3. Facebook, ughaibuni, siasa nyingi, na wizi wa mali ya umma.

    ReplyDelete
  4. KIINI NI KILE KILE KILICHOUA MASHIRIKA YA UMMA.. KWA MALENGO YAJE KUMILIKIWA NA VIGOGO.

    ..Sasa hii pia ni dili nyingine ya Vigogo kufungua shule binafsi za Kuwauzia Elimu kwa walala hoi

    ReplyDelete
  5. Maswali unayouliza Mheshimiwa Waziri Mkuu ni Mazuri sana na ya Msingi,mtu mwenye majibu yote haya ni Mh.Waziri wa Elimu.

    Mh.Mbatia(MB) amesema hatuna Mitahala,kidogo atolewe Macho Bungeni na wewe ukiwemo humo bungeni.Tumepoteza mwelekeo.Kila shule inafundisha 'kivyake vyake'.Ondoeni siasa kwenye Elimu.Hawa wanaofeli wanaelekea wapi huko mtaani?Ajira zipo?.We wait and see.

    David V

    ReplyDelete
  6. Simple, upendeleo ambao umekuwa unafungiwa macho kwa generations sasa haya ndio matatizo yake. Itakuaje mtoto awe anaishi tegeta au mwenge anachaguliwa kwenda kusoma sekondari JKT mgulani halafu yule anaeishi kurasini anapelekwa kwenda kusoma makongo hii inatokana na serikali kuweka incompetent people katika position muhimu halafu wanapo under perform na wananchi wanakasema serikali inadharau vilio vya wananchi sasa madawa hayachanganyiki jipu limekuwa donda ndugu mnataka kusaidiwa, anzeni na kufukuza na kwambwa na yule mama wa baraza la mitihani halafu kaeni mjiulize inaitwa accountability au uwajibikaji.

    ReplyDelete
  7. Kuna mabadiliko mengi yametokea inavyoonyesha ambayo yalianza 2009 na kwamba matokeo mabaya ya kidato cha nne 2012 huenda ikawa ni ni carry-over effect ya mabadiliko yaliyoanzia mwaka 2009. Kama idadi ya wanafunzi ili-triple 2009 wakati walimu waliongezeka then only by 1.8 times, more likely ni kuwa wanafunzi hao hawakupata msingi mzuri then wa kuweza kuwavusha vizuri miaka iliyofuatia 2009, na kwa vile kuna large number of students ambao hawakuwa na good foundation ya masomo katika kundi hili la shule za kata hii yaweza kuwa imechangia kuongeza drastically proportion ya failures 2012. Tuna data nyingi kama zinavyojionesha kwenye hili tangazo, lakini majibu ya ukweli yatapatikana kiutaalamu kama hizi data zitakuwa analysed scientifically. Wajumbe wa hii kamati itabidi waendeshe surveys kwenye mashule target ikiwa ni wanafunzi (hata hao waliomaliza), walimu wao na wadau wengine kwenye suala la elimu ili kupata undani nini kime-itervene hapa kati kati kilichosababisha matokeo mabaya. Hii ni pamoja na ku-collect data kuhusu what happened during past 10 years at least (history) ili kuweza kujua kwa undani intervening factors during this time. Indepth interviews za hao wahusika pia zitasaidia kuconfirm na kupata more information kuhusu the real problem. Kuna haja pia ya kuchanganua data hizo kwa aina ya shule private, govt, na seminari kujua kama failure ilikuwa accross the board, je shule hizi zilianguka kwa kiwango kile kile ama zilitofautiana kiwango cha kufeli. Japo haina maana kuwa hakuna other factors, hata tu kwa upande wa utungaji mitihani, usahihisaji, kuzuia leaking ya exams pamoja na mambo mengine yaliyochangia hii poor performance, from the surface, shule za kata zinaweza kuwa one of the important underlying factors, kwa vile zilianzishwa bila kuangalia kama uwezo wa ku-run hizo shule kwa maana ya idadi walimu inayotakiwa, vitabu, maabara na vinginevyo viko available. Kwa kweli inasikitisha kwani nchi nyingi za wenzetu zina-invest kwenye elimu (as a package, na sio tu madarasa), sasa watanzania tunaenda wapi? Tusipokuwa waangalifu miaka kadhaa ijayo nchi yetu itaendeshwa na wataalamu wa nje ya nchi kwa vile sisi wenyewe tumeshindwa kutoa wataalamu wenye sifa. Something needs to be done soon..

    ReplyDelete
  8. Hivi hiyo kamati inayo wajumbe ambao ni walimu wa sekondari pamoja na wazazi? Ungeweka hata mwanafunzi! Hawa labda hata wasingeomba hata posho. Kitu kingine, kamati ya kuangalia maendeleo na matokeo ya mtihani iundwe na kuwa ya kudumu.

    ReplyDelete
  9. Kuna kipengele hapo nimesoma kinasema idadi ya walimu imeongezeka lakini wanafunzi wanazidi kufeli, hao walimu walioongezeka ni walimu bora ama bora walimu, hayo ma vyuo vikuu mliyoyaruhusu yafunguliwe jama uyoga na count off point mmezishusha hata mtu mwenye E S anaenda kusomea ualimu mlitegemea nini?
    Na je hao walimu tele mnawalipaje, mnawalipa bora au bora kuwalipa? Yale marupurupu mnayowapa walioko maofisi ya elimu wamekalia vitu tu wanazunguka na mkamnyima mwalimu hata posho ya ufundishaji mnaona ni sawa?
    Kila jambo hufanywa kwa malengo, malengo yenu ya elimu ya sekondari ni yapi? Mngekuwa nayo hayo malengo tungewasaifia jinsi ya kuyatimiza lakini hamna malengo zaidi ya kumtaka mwanafunzi afaulu mtihani wa mwisho...ndio maana wanafunzi wanafanya juu chini wapate myihani kabla, kwani mwisho wa siku lazima afaulu huo myihani alopewa na sio kile alichofundishwa darasani kwani mara kibao maswali ya mtihani hayaoani kabisa na walichokisoma darasani kwasababu moja au nyingine.
    Kila elimu huwa na filosofia yake. Je, elimu yetu hii mheshimiwa imejikita katika filosofia gani ya elimu? Bado tuko kwenye ESR? Au?
    Kwenye mtaala, hata kama upo ingawaje nina uhakika haupo kilichopo ni mihutasari tu ya kila somo nayo ni mmoja kwa shule nzima mnanyang'anyana kama dhahabu, ni mibovu isiyoendana na ihalisia na inataka kumjenga mwanafunzi katika kukariri na kujibu mitihani, ndo mitaala tunayotaka?!
    Waziri wa elimu na naibu wake, wako kwenye hiyo nafasi kisiasa kwanini jamani? Kwanini msiweke professionals? Balalusesa mnaye hapo wizarani muulizeni/mtumieni

    ReplyDelete
  10. HALI HII INATOKANA NA KUTOKUWA NA MAZOEA YA KUFUATILIA KILA MWAKA KUPANDA AMA KUSHUKA HATA KAMA IMESHU-
    KA KWA 0.5%. NDG WASOMAJI WA BLOG ZOT E ZA JAMII WALIOPO TZ NA NJE. TUNAZO IDARA ZA UKAGUZI KILA KANDA, HUKAGUA NINI? MAONI YANGU NI MH. PM VUNJA NA KUONDOSHA UCHAFU HUO KWANZA NDIPOSA
    TUANZE KAZI UPYAAAAAAA!

    ReplyDelete
  11. HIVI KUNA AANAYEONA KUWA UANGALIAJI WA TV, FACEBOOK, TWITTER NA VINGINEVYO VINA MCHANGO MKUBWA WA KUDISTRACT WANAFUNZI, WAALIMU NA WAZAZI?

    PILI,

    KUFANIKIWA KIELIMU KUNATEGEMEA SANA MCHANGO WA WAZAZI.

    ReplyDelete
  12. Muda mwingi walimu na wanafunzi wanaupoteza kujadili ligi ya Uingereza na Champions League!!

    ReplyDelete
  13. mnawalaumu wasiohusika. Ni jukumu la mwanafunzi kujibu mtihani mgumu hata kama hakufundishawa alitakiwa ajuwe ajiandae.

    kurekebisha ugumu wa mtihani ndo kutashusha elimu. matakuwa na watu wenye div I 90% lakini hawajui kitu kama nchi kadhaa za asia.

    ReplyDelete
  14. Kamati ya matokeo ya mtihani, walalamikaji ndo wanakamati unategemea nini? Bias!

    Kisingizio: eti kushirikisha wadau woote. Hapa hatupigi kura tunatafuta suluhu ya kitaalamu. SIASA YA UJAMAA INATUPELEKA PABI.

    ReplyDelete
  15. SHULE NYINGI PASIPO WALIMU WA MAANA NDIO KIINI CHA KUSHUKA ELIMU TANZANIA.

    ReplyDelete
  16. Hii kamati, haina hata mwalimu wa hizo sekondari, kuna examination setter au moderator kutoka necta? Je watunga hiyo mitaala wamo? Wazazi kidogo? Wanafunzi kidogo especially walofanya mtihani huo au walioko shule sasa! Tume sijui kamati kwali ( excuse my makonde) imepwaya!

    ReplyDelete
  17. mwacheni kikwete aendelee kujenga nchi kwa kujenga barabara na madaraja na kutoa sapoti kubwa kwenye michezo hali ya kuwa elimu ya taifa la kesho ni zero 0,

    ipo haja ya kujihusisha zaidi katika mambo ya elimu na kujitahidi kulipa mishahara mizuri kwa walimu kuliko wabunge

    kumbuka bila walimu pasingepatikana wabunge na mawaziri

    mheshimiwa tunakuomba uanzishe usemi wa ELIMU KWANZA.

    ReplyDelete
  18. kufaulu kutaongezeka pale tu tutakapotofautisha siasa na mambo ya maendeleo

    ReplyDelete
  19. heheheeee mie yangu macho ila naona ile sera ya chadema ya majimbo iwe applied sasa ili kila jimbo liwe na ministry of education yake ya education kama nigeria na canada labla itasaidia,,,,

    kweli yangu macho wala siwalaumu serikali hata sisi wanafunzi tunamakosa kabisaa

    ReplyDelete
  20. Sababu kwa uhakika zajulikana ila iliyobakia ni serikali kukubali hali halisi ilivyo.
    Miaka ya nyuma serikali ilijenga shule nyingi za kata ili kuwawezesha wanafunzi wengi kusoma sekondari.
    Bila kupimia; shule hizi zilijengwa katika mazingira kwamba mradi kuonekana kuna shule na yenye jina la sekondari. ukiingia kwenye shule hizi; hakuna madawati; viti kwa wanafunzi wala waalimu wao; walimuwachache na kinacokatisha tamaa ni kwamba hakuna vitabu; ubao, mahabara na vifaa vya sayansi; na hata usipojiadhari; hakuna chaki kwa mwalimu.
    Zaidi ya ya vifaa; lugha ya kigeni ndiyo inayowaumiza wanafunzi wengi pamoja na walimu wao.
    Mimi siwaelewi kabisa mafikira ya watanzania wenzangu. kila nchi duniani; wanatumia lugha yao ya taifa lao kufundishia kwenye ngazi zote za elimu nchini; sasa swali ni kwa nini kusifanyika mabadiliko Tz. hata ingalawa kuwepo na shule za sekondari na vyuo vinavyotumia lugha yetu ya "KISWAHILI" kwa masomo yote? Tukizingatia kwamba wanafunzi watakapomaliza mafunzo yao; wanawahudumia watanzania wenye kuongea lugha ya kiswahili na sio kiingereza.
    Hebu; bila kujali taifa lifanye majaribio kwa shule chache nchini ili kuona kama kuna matunda mema kuliko kuwasukumia watoto wetu lugha ambayo hawatakaa waote ndoto kwa lugha hiyo (kiingereza).
    Lugha mama itawaangazia zaidi upevuko wa kufikiri na pia kuweza kujieleza kinaganaga zaidi na kuweka kumbukumbu ya kudumu vichwani mwao.
    Shule zetu zapaswa kuwa na vitabu vya kutosha kwa kila somo,madawati na viti kwa wanafunzi, na mahabara kwa ajili ya masomo ya sayansi na kazi za mikono na mwishowe walimu wa kutosha kwa kila somo.
    Ngerapapa (Ottawa/Canada).

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...