Na Frank John-Maelezo.
Jumla ya shilingi
bilioni 18 zitatumika kwa ajili ya uchimbaji wa visima 20 vya maji vitakavyokuwa na uwezo wa kuzalisha zaidi ya lita milioni 266 kwa
siku katika maeneo ya Kimbiji wilaya ya Temeke na Mpera wilayani Mkuranga kuanza
mwezi wa sita mwaka huu na kukamilika mwezi wa sita mwaka 2014.
Hayo yamesemwa leo na afisa
mtendaji mkuu wa mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam
(DAWASA) Archard Mutalemwa wakati akiwasilisha
ripoti ya utendaji kwa kamati ya Bunge ya
Kilimo, Mifugo na Maji ilipotembelea maeneo ya miradi ya visima hivyo.
Mutalemwa alisema kwamba utafiti
uliofanywa umeonesha kuwa maji hayo ni
safi na salama kwa matumizi ya binadamu na tayari mkandarasi kwa ajili ya
kutekeleza wa mradi huo ameshapatikana . Pia mpango huo utahusisha maeneo
kadhaa ikiwemo upanuzi wa kituo cha Ruvu juu ambao utaanza Julai mwaka huu na kukamilika Machi mwaka 2015.
“Tumeandaa mpango maalum wa
kuhakikisha tunatatua tatizo la maji
safi linalowakabili wakazi wa jiji la Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na kujenga bwawa la Kidunda kuanzia Septemba mwaka huu na upanuzi wa mtandao wa mabomba
utakaoanza mwakani na miradi yote hii itakamilika mwaka 2015”, alisema Mutalemwa.
Aliitaja miradi mingine
katika mpango huo kuwa ni upanuzi wa mfumo wa majitaka unaotarajiwa kuanza
mwakani na kukamilika mwaka 2016 na upanuzi
wa mtambo wa Ruvu Chini.
Kwa upande wa mradi wa
upanuzi wa Ruvu Chini ambao unagharamiwa na Serikali ya Marekani kwa gharama ya
zaidi ya shilingi Bilioni 57, Mutalewa alisema kuwa utaongeza uwezo wa
upatikanaji wa maji lita milioni 270 kwa siku.
Naye Naibu Waziri wa Maji
Mhandisi Dk. Binilith Mahenge alisema kuwa shilingi bilioni 27 zimetengwa kwa
ajili ya kulipa fidia kwa wananchi watakaotakiwa kupisha mradi huo na aliwataka wananachi wa jiji la Dar es Salaam
kuipa Serikali muda wa kufanya kazi hasa za kutatua tatizo la maji.
Tatizo la upatikanaji wa maji
safi kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam limekuwa ni changamoto kubwa ambapo
hadi sasa DAWASA ina uwezo wa kuzalisha lita milioni 300 kwa siku huku mahitaji
yakiwa ni lita milioni 450.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...