Mhe. Jaji Engera Mmari Kileo, akizungumzia uzoefu wa Majaji Wanawake wa Tanzania katika kukabiliana na tatizo la matumizi mabaya ya mamlaka kudhalilisha kijinsia na kushawishi rushwa ya mapenzi ( sextortion) wakati Chama cha Majaji Wanawake- Tawi la Tanzania kilipoanda mkutano wa pembezoni ( side-event) sambamba na mkutano unaoendelea wa 57 wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu Hadhi ya Wanawake ( CSW). aliyekaa kati kati ya Jaji Kileo, na Naibu Mwakilishi wa Kudumu Balozi Ramadhan Mwinyi ni, Bw. John Hendra aliyewahi kuwa Mratibu wa UNDP nchini Tanzania, Bw. Hendra ndiye aliyekuwa mwendashaji wa mkutano huo, bado anakumbuka vizuri kiswahili, kwa sasa ni Katibu Mkuu Msaidizi na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Sera na Mipango katika Taasisi ya UN- Women
Bi. Anne T. Goldstein, Esg; Kutoka Chama cha Kimataifa cha Majaji Wanawake akizungumza wakati wa mkutano huo, Chama cha Kimataifa cha Majaji wanawake, kinafanya kazi kwa karibu na Chama cha Majaji Wanawake- Tawi la Tanzania, na ndiyo chimbuko la neno Sextortion. katika mchango wake licha ya kueleza kwa mapana udhalilishaji wa kijinsia na rushwa ya mapenzi, alihimiza sana umuhimu wa wazazi kuzungumza na watoto wao wote wa kike na wakiume kuhusu madhara ya ukatili huo na namna ya kukabiliana nao.
wajumbe wanaoshiriki mkutano wa 57 wa CSW wakijumuika na washiriki wengine kujifunza nini Chama cha Majaji kinafanya katika ajenda zima ya kupiga vita udhalilishaji wa wanawake na watoto wa kike
Mshiriki ambaye alijitambulisha kwamba ni askari Polisi kutoka nchini Zambia akiuliza swali
wajumbe kutoka Tanzania wanaoshiriki mkutano wa 57 wa CSW wakijumuika na washiriki wengine kujifunza nini Chama cha Majaji kinafanya katika ajenda zima ya kupiga vita udhalilishaji wa wanawake na watoto wa kike.
Na Mwandishi
Maalum
Mwenyekiti
wa Chama cha Majaji Wanawake Tawi la Tanzania, Mhe. Jaji Engera Mmari Kileo ameeleza
kwamba jamii ikishirikiana inaweza kwa kauli moja kupiga vita udhalilishaji wa kijinsia na rushwa ya mapenzi.
Jaji Kileo
ametoa kauli hiyo siku ya jumanne,
wakati chama hicho cha majaji kilipoanda
mkutano wa pembezoni ( Side event) sambamba na Mkutano wa 57
wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu
hadhi ya mwanamke ( CSW) unaoendelea
hapa Makao Makuu ya Umoja wa
Mataifa,
Chama hicho cha
Majaji, kiliandaa mkutano huo ikiwa ni
mara ya kwanza kuendesha mkutano wa aina
hiyo ndani ya viunga vya Umoja wa
Mataifa, kwa lengo la kuelimisha, kufahamishana, kupashana na kubadilishana
mawazo na wajumbe wengine, kuhusu matumizi mabaya ya mamlaka kwa lengo la
kudhalilisha kijinsia na kushawishi rushwa ya mapenzi ( Sextortion).
Bw.
John Hendra ambaye aliwahi
kufanya kazi nchini Tanzania kama Mratibu wa UNDP ndiye aliyekuwa mwendeshaji
wa mkutano huo uliovutia wajumbe wengi
waliokuwa na hamu ya kujielimisha kuhusu
sextortion. Hendra kwa sasa ni Katibu
Mkuu Msaidizi na Naibu Mkurugenzi Mtendaji
wa Será na Mipango katika Taasisi ya UN-WOMEN
“ Unyanyasaji wa kijinsia na rushwa ya mapenzi ni mambo yanayotokea katika jamii yetu, yanatokea
vyuoni, mashuleni, majumbani,
maofisini na hata mitaani. vitendo hivi siyo tu kwamba ni kosa la jinai , bali pia ni ukiukwaji wa haki za binadamu”
akasema Mhe. Jaji Engera Kileo ambaye
alikuwa mmoja wa wasemaji wakuu katika mkutano huo.
Na kwa sababu hiyo na kwa
kulitambua tatizo hilo, akasema,Tanzania
kupitia Chama cha Majaji Wanawake, imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ikiwamo ya kuwaelimisha wanawake na watoto wa kike
katika taasisi za elimu ya juu,
mashuleni na katika maeneo mengine
kuutambua na kutoufumbia macho ukatili huo.
Aidha amefafanua
kwamba, udhalilishaji wa kijinsia na rushwa ya ngono, si tatizo linalowakumba
wanawake na watoto wakike pekee , bali
hata watoto wa kiume wamekuwa wahanga wa janga hilo.
Mhe. Jaji Kileo
amesema hivi sasa kumekuwa na mwamko
mkubwa wa kulitambua tatizo hilo, ingawa amekiri kwamba bado safari ni ndefu na changamoto nyingi.
Akazitaja baadhi changamoto hizo ni ufinyu wa raslimali ili kuwafikia walengwa
wengi zaidi, kutokuwapo kwa utashi wa wahanga kujitokeza na kutafuta haki
yao, uwezeshaji wa wakufunzi pamoja na uwezeshaji wa kiuchumi
kwa wanawake na watoto wa kike.
Katika utoaji
elimu hiyo wa suala zima la sextortion,
Mzungumzaji mwingine alikuwa ni
Bi. Anne Goldstein, Esq ambaye ni
Mkurugenzi wa Elimu ya Haki za Binadamu, katika Chama cha Kimataifa cha Majaji
wanawake.
Akitoa ufafanuzi kuhusu udhalilishaji wa kijinsia na rushwa ya
mapenzi, Anne,alisema tatizo hilo haliko
katika nchi zinazoendelea peke yake bali lipo duniani kote.
Akasema ni
tatizo kubwa, sugu na lenye sura nyingi
na kwamba kulikabili kunataka nguvu za
pamoja na ushiriki wa wadau wengi.
Lakini akasema
ni tatizo linaloweza kutafutiwa ufumbuzi ikiwa tu wadau wote wataonyesha utashi
wa kufanya hivyo.
Akahimiza sana
suala la wazazi kukaa na watoto wao wa
kike na kiume na kuelezana kinabaubaga kuhusu madhara
ya udhalilishaji wa kijinsia na rushwa ya ngono ikiwa ni pamoja na kuwajengea mazingira ya kuwa
huru kueleza pale wanapohisi kutaka
kufanyiwa ukatili huo.
Akasema chama
cha Kimataifa cha Majaji Wanawake,
kimekuwa kikifanya kazi kwa karibu sana na Chama cha Majaji Wanawake – Tawi
la Tanzania, na kwamba wanajivunia uhusiano na ushirikiano huo na kitaendelea kufanya kazi kwa karibu na
Majaji watanzania.
Naye Katibu Mkuu
Msaidizi, Bw. John Hendra, yeyé
pamoja na kuwapongeza Chama cha Majaji
Wanawake kwa kazi nzuri, kwa
ujumla aliipongeza Serikali na watanzania wote, kwa kukubali na kutambua kwamba
kuna tatizo hilo la udhalilishaji wa
kijinsia na rushwa ya ngono na hivyo
kuamua kulikabili.
Akasema UN- Women itaendelea kufanya kazi kwa karibu
na Tanzania katika maeneo mbalimbali.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...