Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia na. Watoto Mhe Sophia Simba ( Mb) akiongoza ujumbe wa Tanzania wakati wa ufunguzi wa  Mkutano wa 57 wa Kamisheni kuhusu Hali ya  Wanawake ( CSW) mkutano huo wa wiki mbili umeanza siku ya jumatatu hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa, wengine katika picha ni Balozi  Tuvako  Manongi, Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Mhe.  Engera Kileo Mmari Jaji wa Mahakama ya Rufa, Naibu Mwakilishi wa Kudumu, Balozi Ramadhan Mwinyi, wengine ambao wapo katika meza  hiyo ya Tanzania, ni  Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bi. Kijakazi Mtengwa  na Mhe. Imani Aboud Jaji wa Mahakama ya Rufaa


Na Mwandishi Maalum
Mkutano  wa  57 wa  Kamisheni ya Umoja wa Mataifa Kuhusu Hali ya Wanawake (CSW),  umeanza siku ya jumatatu hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa.
Mkutano huo  wa wiki mbili  na ambao hufanyika kila mwaka unawakutanisha Mawaziri  wanaohusika na masuala ya wanawake na maendeleo ya jamii kwa ujumla,  wataalamu mbalimbali vikiwamo vyama visivyo vya kiserikali kutoka  duniani kote.
Ujumbe wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  katika  mkutano huu unaowajumuisha washiriki kutoka Serikali  ya Mapinduzi Zanzibar  unaongozwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Mhe. Sophia Simba ( MB).
Miongoni mwa wajumbe wa Tanzania  ni  Bi Kijakazi Mtengwa, Katibu Mkuu Wizara ya  Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Bi. Fatma Gharib Bilal, Katibu  Mkuu, Wizara ya  Ustawi na  Maendeleo ya Jamii,     Vijana,Wanawake, na  Watoto,  Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Majaji wa  Mahakama ya Rufaa, Mhe. Engera Kileo Mmari na Mhe. Iman Daud Aboud.
Akifungua mkutano huu, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Jan  Eliasson amesisitiza kwa kusema, vita  vya kuutokomeza   ukatili dhidi ya wanaweke lazima iwe ya kufa na kupona.
Akaeleza kwamba  ukatili dhidi ya wanawake ni jambo  linalotokea kila mahali hata katika nchi  zilizoendelea.
Akabainisha kwamba ili kukakibiliana na ukatili dhidi ya wanawake, panahitajika  mbinu mchanganyiko   kuanzia serikalini kwa kutekeleza sera za kuwawezesha waathirika wa vitendo hivyo , kuwaadhibu wahalifu
Akaeleza pia kwamba,  wanaume na watoto wa kiume wanatakiwa kuhamasishwa kushiriki katika kupiga vita ukatili dhidi ya wanawake ikiwa ni pamoja na kuwajengea utamaduni wa kuwajibika katika shughuli mbalimbali za kifamilia.
Akaeleza  zaidi kwamba,  vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto  wakike vinafanyika katika  maeneo yenye vita na migogoro lakini pia vinafanyika katika nchi zenye amani na utulivu. Na kama hiyo haitoshi vinatendeka pia kwenye miji mikuu   na halikadhalika vijijini.
“Ni vitendo” anasema Naibu Katibu Mkuu. “Vinavyotokea katika maeneo ya wazi na yaliyojificha pia. Na kwa kuwa ni jambo lisilokubalika katika maisha yetu ya kila siku, tunawajibika kulishughulikia kwa nguvu zote kila mahali na katika ngazi zote”.
Kwa mujibu wa  Taasisi ya  UN-WOMEN zaidi ya asilimia 70 ya wanawake katika baadhi ya nchi ni wahanga wa  ukatili au ukatili wa ngono katika maisha yao. Na katika nchi kama vile Australia, Canada, Israel, Afrika ya Kusini na Marekani asilimia kati ya 40 na 70 vifo vya wanawake vinasababishwa na  masuala  ya mapenzi.
Naye  Mkurugenzi Mtendaji wa  UN-WOMEN Bi. Michelle Bachelet amewaeleza wajumbe wa  Kamisheni hiyo kwamba, dunia haiwezi tena kuendelea  kuhimili gharama za vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Akaongeza kwamba ni wakati muafaka  na wa haraka kwa serikali kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivi ambayo anasema vinaendelea kulalamikiwa katika jamii
 Mwenyekiti wa CSW  Balozi Marjon Kamara ambaye ni Balozi  wa Liberia  yeyé amesema katika wiki mbili za mkutano huo wajumbe watajadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu mbinu mbadala na zinazotekelezeka za kuzuia ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa  wakike,  mbinu ambazo kweli zitaweza kuleta matokeo.
Pamoja na Ujumbe wa Tanzania  kushiriki  kikamilifu katika  mikutano na mijadala mbalimbali ambayo imo ndani ya  ratiba kuu ya    CSW.  Tanzania  nayo itakuwa na  mijadala yake miwili ( side Events), kwa lengo la kuonyesha uzoefu wa Tanzania katika kukabiliana na  ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike
Mjadala wa kwanza  umeandaliwa na washiriki kutoka Tanzania Visiwani,    mada yake itahusu: Vunja ukimya, unga mkono juhudi za sekta mtambuka katika  kuzuia na kukabiliana na unyanyasaji dhidi ya wanawake;  uzoefu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; mfano wa Zanzibar.
 Na  mjadala wa pili   umeandaliwa na Chama cha Majaji Tanzania, utajadili kuhusu: Ukomeshaji wa matumizi mabaya  ya mamlaka kwa madhumuni ya kudhalilisha  kingono ( sextortion); Uzoefu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...