Kocha wa Azam FC, Stewart Hall akizungumza na Florian Kaijage Mratibu wa klabu katika mashindano ya Afrika, baada ya kuwasili Cassablanca leo


Na Mahmoud Zubeiry, Rabat
AZAM FC imewasili salama nchinio Morocco tayari kwa mchezo wa marudiano dhidi ya wenyeji, FAR Rabat, Raundi ya Tatu ya Kombe la Shirikisho Afrika Jumamosi wiki hii.  
Azam, imewasili Cassablanca, majira ya saa 9:15 za huku Alasiri, sawa na saa 10:15 za Afrika Mashariki na kusafiri kwa basi kwa saa mbili kwenda Rabat, mji ambao mechi itachezwa.
Azam imetua Morocco ikitokea Dubai, UAE ambako ilifika usiku jana saa 6:00 kwa saa za huko sawa na saa 5:00 kwa saa za Afrika Mashariki, ikitokea Dar es Salaam.
Msafara huo unaouhusisha wachezaji na benchi la Ufundi, baada ya awali viongozi na wapenzi kadhaa kutangulia nchini humo, ili kuweka mazingira sawa, uliondoka Dar es Salaam kwa ndege ya shirika la Emirates, wadhamini wa Arsenal ya England saa 11:00 jioni kwa saa za Tanzania.
Ni safari ndefu iliyohusisha mabara mawili, kutoka Afrika, Tanzania kupitia Asia Dubai na kurudi Afrika nchini Morocco.
Azam walilala katika hoteli ya nyota tano ya Copthorne Dubai kabla ya kuunganisha ndege saa 7:35 asubuhi ya leo kuja Morocco kesho.
Wachezaji wanawasili Morocco

Azam imefikia katika hoteli ya Golden Tulip, maeneo ya Rabat, kaskazini mwa Cassablanca,  kilomita 120 kutoka Uwanja wa Ndege wa Cassablanca, umbali wa takriban saaa mbili.
Azam itaanza rasmi mazoezi kesho kujiandaa na mchezo huo, ambao wanatakiwa kutoa sare ya mabao au kushinda ili kusonga mbele, baada ya awali katika mchezo wa kwanza kulazimishwa sare ya bila kufungana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki iliyopita.
Japokuwa hilo linachukuliwa kama jambo gumu mbele ya wengi, lakini rekodi ya timu hiyo, mali ya bilionea Alhaj Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake inaonyesha linawezekana.
Wachezaji wanatua Morocco

Azam imekuwa ikicheza vizuri na kupata matokeo mazuri katika mechi za ugenini kwenye michuano hii, kuliko nyumbani na hata kufuzu kwake hadi hatua hii zaidi kulitokana na matokeo ya mechi za ugenini.
Raundi ya kwanza, Azam ilianza kwa kushinda kwa taabu 3-1 Dar es Salaam dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini, sehemu kubwa ya mchezo huo matokeo yakiwa 1-1 kabla ya mabao ya dakika za jioni ya Kipre Tchetche kutengeneza ushindi huo.
Mchezo wa marudiano, Azam ilishinda 5-0 ugenini na kufanya ushindi wa jumla wa 8-1, ikisonga mbele kibabe.
Raundi ya Pili, ilianza kwa ushindi wa 2-1 ugenini, Liberia dhidi ya wenyeji, Barack Young Controllers II, lakini katika mchezo wa marudiano ilibanwa kwa sare ya 0-0.
Kocha Muingereza Stewart Hall hakuipa umuhimu mechi ya Ligi Kuu Ijumaa dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga iliyoisha kwa sare ya 1-1 akiwapumzisha wachezaji wake kadhaa wa kikosi cha kwanza kwa ajili ya mechi na FAR Rabat.
Wakati mabeki Waziri Salum, Joackins Atudo, viungo Khamis Mcha ‘Vialli’, Kipre Balou na mshambuliaji Kipre Tchetche hawakukanyaga kabisa nyasi za Uwanja wa Mkwakwani Ijumaa, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ alicheza kwa dakika 15 tu za mwisho- ili kuhakikisha wanakuwa vizuri Jumapili mjini Rabat.
Kutoka kikosi cha kwanza cha sasa cha Azam waliocheza dakika zote juzi ni kipa Mwadini Ally, kiungo aliyehamishiwa beki ya kulia, Himid Mao, beki David Mwantika, kiungo Humphrey Mieno na washambuliaji Brian Umony na John Bocco ‘Adebayor’.
Azam, itakuwa Rabat kwa wiki nzima hadi Jumamosi itakapocheza mechi na imejipanga vema kuhakikisha inavuka hatua hii.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. yaani hakuna kabisa usafiri wa kwenda morocco kutoka Tanzania bila ya kutoka nje ya africa?

    mfano egypt air si inatua dar? pia inafanya safari za morocco kwa nini hawakutumia route hii?

    ReplyDelete
  2. Hata mie nashangaa, ila lakini yawezekana walitaka kubana matumizi, ndio maana wakaamua wazunguke.
    Jamani vichwa vya habari wakati mwengine viwe vyenye kutia moyo na si kukatishana tamaa mapema au ndio mnatanguliza ujumbe???

    ReplyDelete
  3. Wewe hilo linakuhusu nini si ungewakatia hiyo Egypt air wafanye route unayotaka ww? Wenzio wamejipanga toa comment zenye akili sio mradi tu unaandika utumbo wako.

    ReplyDelete
  4. wewe anony wa tatu ndio umeandika utumbo na pumba! soma kichwa cha habari "wamechoka ile mbaya kwa urefu wa safari" mwenzako ana suggest shortest route wewe unakurupuka kwa comment za pumba humu!

    ReplyDelete
  5. Kila la Kheri AZAM.Mechi ya kwanza mlifanya makosa makubwa ya kutoielewa vizuri hii timu.Ina wachezaji wanne walioko timu ya Taifa ya Morocco na walikuwa wametoka kucheza uwanja wa Taifa(Stars vs Morocco),kwa hiyo walikuwa kama wako nyumbani;naongelea Younnes Hammal,Youness Belakhdar,Abderrahim Achchakir na Salahedinne Said.Chezeni mpira wenu,mnawatoa hao

    David V

    ReplyDelete
  6. wewe mdau wa tatu ndio unaeleta comments za utumbo. mwandishi ameeleza fika kuwa timu imefika morocco ikiwa wamechoka kwa sababu ya mzunguko wa usafiri, sasa kuna kosa gani kwa mtu kuuliza ni kwa nini wakachukua route hiyo ilhali zipo route nyengine ambazo zingeliwafikisha mapema na bila ya kuwa na uchofu mkubwa?
    Tumia kichwa utasemaje wamejipanga ikiwa wamefika wakiwa hoi na huku wanakabiliwa na mechi ngumu? walihitaji kufika mapema, wapumzike vizuri ili waweze kuhimili vyema pambano lao, mtu yeyote yule atakwambia hivyo ndivyo kujipanga kunavyotakiwa.

    ReplyDelete
  7. kwi kwi kwi mdau pumba

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...