Na Profesa Mbele

Nimerejea jioni kutoka Montana, ambako nilikwenda jana, kuonana na Mzee Patrick Hemingway (akiwa nami pichani), mtu maarufu sana. Ni yeye pekee ndiye bado hai kati ya watoto wa mwandishi maarufu Ernest Hemingway (BOFYA HAPA).

Mwandishi Hemingway, ambaye alizaliwa mwaka 1899 jirani na Chicago na kufariki 1962, ni maarufu duniani kote. Kwa miaka yapata kumi, nimevutiwa na jinsi alivyoandika kuhusu Afrika, kutokana na kutembelea na kuishi Afrika Mashariki, mwaka 1933-34, na mwaka 1953-54. Ninasoma na kufundisha maandishi ya Hemingway, kama nilivyoandika hapa, na hapa.

Kwa muda mrefu nilitaka niwasiliane na Mzee Patrick Hemingway, ambaye ni mtoto pekee wa Hemingway aliyebaki. Nilifahamu kuwa aliishi Tanzania miaka yapata 25. Moja ya shughuli alizofanya ni kufundisha katika chuo cha Mweka. Nilisoma sana maandishi yake na kusikiliza mazungumzo yake ambayo yako mtandaoni.

Nilijua kuwa huyu ni hazina kubwa kwa yeyote anayefuatilia maandishi na maisha ya Ernest Hemingway. Siku moja, miaka yapata miwili iliyopita, nilijipa moyo nikampigia simu. Nilifurahi jinsi alivyonifanyia ukarimu, tukaongea sana. Kuanzia hapo, nimeongea naye mara kwa mara.

Hatimaye, jana nilisafiri hadi Montana, ambako tumepata fursa ya kuongea kwa masaa mengi, jana na leo. Nimefurahi kwa namna ambayo siwezi hata kuelezea. Nategemea kuandika taarifa mbali mbali za ziara hii siku zijazo.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Professor Mbele hata na wewe ni mwamdishi mzuri sana. Mimi nipo Hapa Saskatchewan- Canada na kuna wakati nilikuja kutembea Minneapolis ningejua upo karibu hapo ningekutafuta. Naona kuna siku tutarudi kutembea tena.Basi nasubiri makala yako kuhusu mzee Patric.

    ReplyDelete
  2. Ankal, shukrani kwa uamuzi wako wa kuiweka taarifa yangu hapa kwenye blogu ya jamii. Kwa namna hii inawafikia watu wengi sana.

    Kuna anonymous ameandika kwenye blogu yangu kuhusu hii taarifa yangu, nami nikamjibu. Soma hapa.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...