Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia
salamu za rambirambi Rais wa Kenya, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta kuomboleza kifo
cha Mjumbe wa Baraza la Seneti na Waziri muhimu wa zamani wa nchi hiyo,
Mheshimiwa Mutula Kilonzo (pichani), aliyefariki dunia juzi, Ijumaa, mjini Nairobi.
Katika
salamu zake za rambirambi, Rais Kikwete amemwambia Rais Kenyatta kuwa amepokea
habari za kifo cha ghafla cha mwanasiasa huyo kwa mshtuko na huzuni na kuwa
kifo chake kimeipokonya nchi hiyo mmoja wa viongozi waliokuwa wanajali na
kutanguliza maslahi ya Kenya na wananchi wake.
“Kwa
hakika, kifo cha Mheshimiwa Mutula Kilonzo kimeipokonya Kenya kiongozi muhimu.
Mchango mkubwa aliuotoa katika kipindi cha kuivusha Kenya kutoka kwenye
changamoto za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2007 hadi sasa ambako nchi imetulia na
inasonga mbele, kamwe hautasahaulika,” amesema Rais
Kikwete na kuongeza:
“Katika
nafasi zote za Uwaziri alizozishikilia katika kipindi hicho, kwanza kama Waziri
wa Sheria na Masuala ya Katiba na baadaye kama Waziri wa Elimu, alijithibitisha
na kujipambanua kama Mzalendo wa kweli kweli wa Kenya na mpenzi halisi wa nchi
yake.”
Ameongeza
Rais: “Nakutumia Mheshimiwa Rais salamu zangu za rambirambi na zile za
Serikali yangu kufuatia msiba huu. Aidha, kupitia kwako naomba unifikishie
salamu zangu kwa familia ya Mheshimiwa Kilonzo. Nataka wajue kuwa niko nao
katika kipindi hiki kigumu cha majonzi na naungana nao kuomboleza na kumwomba
Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya Marehemu Mutula Kilonzo.Amin.”
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
IKULU,
DAR ES SALAAM
28 Aprili, 2013
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...