Na Ripota wetu, Dodoma

KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ameibuka na kupinga vikali tuhuma zilizotolewa dhidi yake na kambi ya upinzani bungeni kuhusu shehena ya pembe za ndovu iliyokamatwa Vietnam mwaka 2009 kuwa ni za kupika na za uongo.

Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma. "Tuhuma hizo hazina ukweli wowote, zina nia mbaya dhidi yangu na zemelenga kuniharibia taswira yangu na ya chama changu," alisema Kinana. Aliongeza kuwa tuhuma hizo hazina msingi wowote na kuwa hata kambi hiyo ya upinzani bungeni inatambua kuwa mamlaka zote za ulinzi na usalama za ndani na kimataifa zilimsafisha kuhusiana na sakata hilo.

Kinana alisema baada ya shehena hiyo kukamatwa, Mamlaka ya Kimataifa ya Kudhibiti Wanyama Walio Hatarini Kutoweka (CITES) na Polisi wa Kimataifa (INTERPOL) walifuatilia na wakabaini kuwa hakuhusika kwa namana yoyote na shehena hiyo. Kwa mujibu wa nyaraka za uchunguzi kuhusiana na shehena hiyo, watuhumiwa walikamatwa na kufikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Kisutu ambao ni Eladius Colonerio (Mkurugenzi wa Team Freight (T) Ltd) Gabriel Balua (Meneja wa TEA Freight (T) Ltd) na Shaban Yabula (Mkurugenzi Mtendaji wa Kigoma M.N Enterprises (T) Ltd).

Wengine waliofikishwa mahakamani ni Erick Morand (Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania katika Bandari ya Dar es Salaam) Issa Lweno, Norbert Kiwale na Abubakari Omar Hassan. Nyaraka hizo ambazo gazeti hili lina nakala zake, zinaonyesha kuwa maofisa wa forodha huko Haiport and Hanoi, Vietnam waliokamata pembe za ndovu kilo 6,200 zilizosafirishwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam. Pia, kati ya Machi na Juni, 2009, maofisa wa forodha wa bandari ya  South harbor mjini Manila, Philippines walikamata shehena nyingine ya kilo 4,861 zilizosafirishwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam.

Kutokana na taarifa za kukamatwa kwa shehena hiyo ya pembe za ndovu kutoka Vietnam, Jeshi la Polisi lilianza uchunguzi kwa kushirikiana na Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), INTERPOL na Taasisi ya Kupambana na Ujangili Kusini na Mashariki mwa Afrika (LAFT).Uchunguzi huo uliongozwa na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Angelist Bonga ambaye kwa sasa ni marehemu. "Timu hiyo ya wachunguzi ilifanya kazi yake kwa umakini na kufanikiwa kuwanasa watuhumiwa watano ambao baadaye walifunguliwa mashitaka mahakamani," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Wakati kesi hiyo ikiendelea, serikali iliamua kupeleka timu ya wachunguzi nchini Vietnam, lakini nchi hiyo ilikataa kuwaruhusu kufanya uchunguzi nchini humo kutokana na Tanzania kutokuwa na makubaliano ya kubadilishana taarifa za masuala ya uhalifu. Hadi sasa mafaili ya kesi hiyo yapo Mahakama ya Kisutu.

"Tuhuma dhidi yangu hazina msingina ukweli wowote, hivyo hazina uzito wowote. Najua  hii ni sehemu ya siasa chafu na nilitarajia mambo kama haya baada ya kuhutubia nikiwa Morogoro wiki mbili zilizopita kuwa Watanzania wajiepushe na siasa zenye lengo la kuleta vurugu kwa taifa....Msigwa (Peter) na CHADEMA wanapaswa kutoa hoja," alisema Kinana.

Akiwasilisha hoja wakati wa kuchangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Waziri Kivuli wa wizara hiyo Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini - CHADEMA) aliilaumu serikali kwa kushindwa kuchukua hatua kwa baadhi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya ujangili na kumtaja Kinana kuwa mmoja wa wanaomiliki meli iliyosafirisha pembe za ndovu.

Hata hivyo, Kinana hamiliki meli yoyote na hajawahi kujihusisha na usafirishaji wa nyara hizo za serikali, suala ambalo kwa sasa bado lipo mahakamani. Katika mkutano wake na waandishi wa habari, alimtuhumu Msigwa kuwa ana agenda ya siri na kuwa ameamua kumtuhumu huku akijilinda kwa kinga za bunge na kuwa kufanya hivyo ni kutumia vibaya kinga hizo.

Alisema ahusiki na hana uhusiano wa aina yoyote na tuhuma hizo na kwamba hata kipofu anaweza kuona kuwa hausiani nazo na alituhumu kambi ya upinzani bungeni kwa kushindwa kujadili hoja za maana za maendeleo na badala yake kujihusisha na siasa za kuchafua heshima za watu wengine.

"Bado nina nguvu na sijayumba kwa namna yoyote. Nina jukumu la kuilinda CCM na kutekeleza ahadi tulizozitoa kwa wananchi kupitia ilani ya uchaguzi," alisisitiza na kuhoji kuwa suala la shehena hizo ni la tangu mwaka 2009, kwa nini lijitokeze sasa? "Jibu lake ni jepesi, lengo lao ni kumvunja moyo Katibu Mkuu wa CCM ambaye CHADEMA wanamuona kuwa ni tishio kwao," alisema Kinana.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...