Tarehe kama hii, miaka mitano uliyopita,mama mpendwa Adelina Mapango, uliagana nasi. Nikisema 'uliagana nasi' inaweza kutafsiriwa kana kwamba ulipata nafasi ya kutuaga.Nilikuja huko nyumbani kukuuguza Februari 2008, lakini tangu nilipokuona pale Muhimbili hadi tarehe 29 Mei 2008 hukuwahi japo kuniambia neno moja la mwisho.Nakumbuka ulivyokuwa ukiniangalia kwa upendo wako mkubwa,nakumbuka pia tabasamu lako licha ya maumivu makubwa uliyokuwa nayo.Lakini kila nilipojaribu angalau kusikia neno lako moja tu,haikuwezekana hadi siku unafariki.

Mama mpendwa, kabla ya kifo chako sikuwahi kuelewa maana ya kufiwa na mzazi au mtu wa karibu.Sasa sio tu naelewa bali kila siku ya Mungu tangu siku ulipotutoka imekuwa kama ndoto mbaya ambayo natamani iishe ili hali irejee kuwa kama zamani.Kwa bahati mbaya, ndoto hiyo mbaya ni ukweli (hali halisi), na hadi sasa matarajio kuwa kuna siku nitaamka na kukuona au kukusikia ukiwa hai yanazidi kufifia.Kwa kifupi,mama mpendwa,hadi leo bado napata shida kuamini na kukubali kuwa haupo nasi.

Nyakati mbili ngumu zaidi kwangu ni wakati ninapofanya sala kabla ya kulala ambapo wakati wa uhai wako nilikuwa nikisali "Ee Bwana uijalie familia yangu yani Baba na Mama..." lakini sasa inabidi nimtaje Baba pekee.Pia wakati wa uhai wako,nilijenga utaratibu kwamba nikipiga simu naanza kuongea na Baba kisha anapitisha simu kwako tunaanza kutia stori mbalimbali.Sasa,mama,nikimaliza kuongea na Baba huwa najikuta nasahau kuwa haupo hapo nyumbani,na kumwambia Baba akupe simu...then nakumbuka haupo.Naishia kutoa machozi.

Nikiwa mbinafsi,nitaangalia tu jinsi ninavyopata shida kukabiliana na ukweli kuwa hauko nasi.Lakini kuna rafiki yako kipenzi Baba Mzee Chahali ambaye yeye amekuwa mtu tofauti kabisa tangu ulipoondoka.Kama unavyokumbuka,baba ni mtu mkimya,mwenye marafiki wachache, na rafiki yake mkuu ulikuwa wewe.Sasa tangu uondoke,baba amekuwa mnyonge kupita kiasi.Kibaya zaid, ameendelea kudai labda yeye ndio angestahili kutangulia mbele ya haki kwa vile alikuwa amekuzidi kiumri.Kwa hakika, baba ameendelea kuwa katika wakati mgumu sana licha ya sapoti kubwa tunayompatia.

Lakini pia kuna rafiki zako wapenda Kulwa na Doto (Peter na Paul). Pengine kwa vile wao ni last borns, walikuwa wakikuchukulia zaidi ya mzazi, ulikuwa kama bibi yao, shangazi yao, na kikubwa zaidi, rafiki yao.Kila ninapoongea na wadogo zangu hawa najiskia kutokwa na machozi.Kimsingi, sidhani kama waliwahi kuwaza kuwa na maisha bila ya uwepo wako mama.

Familia yote kwa ujumla inakukumbuka sana mama.Nina mkanda wa video niliowarekodi wewe na baba mlipokuwa mnaadhimisha miaka 50 ya ndoa yenu mwaka 2005,lakini kila nikijaribu kuuangalia najikuta nabubujikwa na machozi.Katika mkanda huo uliongea mambo mengi ya msingi kuhusu maisha.Kuna nyakati nataka kuuangalia ili nirejee wosia wako lakini nashindwa kwa sababu ya uchungu.

Mama nilikupenda sana,ninakupenda sana,na nitaendelea kukupenda milele.Kwangu, japo hupo nasi kimwili,lakini unaendelea kuishi nasi kiroho.Nitazidi kukukumbuka kwa sala kila siku,na ninaamini huko uliko unapata faraja kila ninapotenda mambo kwa kuzingatia mafundisho yako.

WE MISS YOU SO MUCH MAMA MPENDWA
PUMZIKO LA MILELE AKUPE EE BWANA NA MWANGA WA MILELE AKUANGAZIE UPUMZIKE KWA AMANI AMINA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. AnonymousMay 29, 2013

    Hakuna msiba usiokuwa mchungu maishani kama wa mama. Mwenyezi mungu akutie nguvu zaidi. Nimesoma article yako ingawa siwafahamu familia yako lakini maneno yanachoma moyo

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 29, 2013

    Pole sana, mwombe sana Mwenyezi Mungu aendelee kukutia nguvu, kweli maneno yako yanachoma sana na kuliza. Sasa mshike sana Baba Mungu kwani yeye ni baba wa yatima na Wajane.Anapotoa kitu huwa analeta kitu kingine kama ukimwamini.Pole sana.

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 29, 2013

    Pole sana mpendwa. Lakini amini kuwa mama yenu yuko "pazuri" na yuko nanyi bado (spiritually)........ Wanasema kuwa marehemu wetu huwa "wapo" nasi ingawa siyo rahisi kuamini. Angalia ujumbe wako ulivyouandika, ni ushahidi tosha kuwa "unaongea" naye. Muhimu ni kukubali hiyo hali ili na yeye huko alipo aweze "kupumzika". Kama wewe ni muumini mzuri wa dini yako, please kila umkumbukapo mama yako, sali ili Mwenyezi Mungu akupe wepesi na kukuwezesha ku-move on. Sisi tuliondokewa na mama yetu miaka tisa iliyopita, lakini tulibahatika kuwa "aliaga" kwa muda wa karibu miezi mitatu kabla ya kifo chake. Alimtayarisha kila mpendwa wake na hasa baba yetu, ambaye twamshukuru mungu kuwa bado yuko hai and very strong (at 85). Kinachotusaidia sana ni sala na pia hali nzuri ya baba inatupa moyo sana. Kwa hiyo, pamoja na ukweli kuwa mama hayupo "physically" tumeshazoea kila tunapopata jambo jema katika famili, tunasema "ni mambo ya mama hayo", tukiamini kuwa huko aliko, naye anatuombea kheri kila siku. Pole sana dear, lakini usisahau kuwa kifo NI SEHEMU YA MAISHA.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...