MKE WA WAZIRI MKUU Mama Tunu Pinda amewaasa Makatibu
Muhtasi na kuwataka wazingatie maadili ya taaluma yao ya uhazili ili kuongeza
ufanisi wa majukumu ya kazi zao.
Ametoa wito huo leo mchana (Alhamisi, Mei 16, 2013) wakati
akifungua Kongamano la Tatu la Makatibu Muhtasi (Tanzania Personal
Secretaries Association - TAPSEA) kwenye ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha
(AICC), Jijini Arusha.
Kongamano hilo la siku mbili, limehudhuriwa na Makatibu
Muhtasi zaidi ya 1,500 kutoka mikoa yote nchini, na baadhi ya wawezeshaji
kutoka Kenya, Uganda na Rwanda.
“Umuhimu wa taaluma ya uhazili katika taasisi tunazofanyia
kazi unatokana na nafasi kubwa ya makatibu
muhtasi kama wasimamizi wa ofisi na wasaidizi wa watendaji wakuu. Nafasi yenu inawapa
fursa ya kuandaa na kutunza nyaraka mbalimbali za kiofisi zinazohusu menejimenti
ya taasisi hizo. Niwaombe makatibu muhtasi wote mzingatie maadili ya kazi ya uhazili
katika kutekeleza majukumu yenu,” alisisitiza.
Aliwataka waongeze
jitihada za kukimarisha Chama cheo ili hatimaye TAPSEA iweze kuenea Mikoa yote
na kuwa Chombo kitakachosimamia miiko na maadili ya fani ya Uhazili.
Alisema majukumu
ya makatibu muhtasi siyo kupiga chapa pekee na kuongeza kwamba, kama chama cha kitaaluma,
TAPSEA lazima iendeleze jitihada za kubadili mtazamo huo ili jamii iweze
kutambua umuhimu wa nafasi ya makatibu muhtasi katika taasisi mbalimbali za
umma na za sekta binafsi.
“Hata hivyo, napenda ieleweke kwamba kazi ya kuleta
mabadiliko ya kimtazamo inaanzia kwa katibu muhtasi mwenyewe. Nawashauri wanachama
wote wa TAPSEA wawe mstari wa mbele katika kubadilika kifikra na kujiendeleza
kila wakati ili kujijengea uwezo wa kuzikabili ipasavyo changamoto za taaluma
ya uhazili katika mazingira ya sasa,” alisema.
Mama Tunu Pinda
alisema kuwekeza katika teknolojia ni jambo muhimu lakini teknolojia pekee
haiwezi kuleta mabadiliko chanya katika kuboresha huduma na kuongeza tija. “Jambo
hili ni lazima liende sambamba na uwekezaji katika rasilimali watu kwa
watumishi kusoma zaidi na kupatiwa fursa za mafunzo zaidi ndani na nje ya nchi,”
alisisitiza.
Mama Tunu Pinda
pia alizindua TAPSEA SACCOS na kuwataka makatibu muhtasi hao wajiunge kwa wingi
ili kutunisha mfuko wa chama chao.
Mapema, akimkaribisha kuzungumza na washiriki wa mkutano, Mlezi
wa TAPSEA Dk. Mary Nagu ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Uwekezaji na Uwezeshaji aliwataka wawe waaminifu katika
kuijenga TAPSEA SACCOS ili hatimaye ifikie hatua ya kuwa benki yao maalum kama ilivyo
kwa Chama cha Walimu nchini.
Naye Naibu Waziri
wa Katiba na Sheria, Bi. Angela Kairuki ambaye pia mshauri wa Kisheria wa
TAPSEA aliwataka washiriki wa kongamano hilo kuzingatia maadili kwa kutunza
siri za ofisi wanazozitumikia.
“Inasikitisha
kuona kila mara kunakuwa na taarifa ambazo zinavuja lakini ukifuatilia wapi
taarifa hizo zimetokea utabaini kuwa chanzo ni makatibu muhtasi... ninawaomba
sana mjitahidi kutunza siri za taasisi zenu,” alisisitiza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,
ALHAMISI, MEI 16,
2013.
very insipirational state lady...she knows where the country is stuck at......customer service and best practice..
ReplyDeleteMaina A. Owno