Na. Eliphace Marwa - MAELEZO
Serikali
imesema kuwa itaendelea kutumia njia mbalimbali kuwahamasisha
wananchi kuzingatia matumizi ya lishe bora kwa kuweka msisitizo katika
kilimo cha matunda, mbogamboga, ufugaji wa samaki na matumizi ya vyakula
vilivyowekewa virutubisho muhimu .
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri mkuu Peniel Lyimo akiongea na
waandishi wa habari kwa niaba ya Katibu mkuu Kiongozi ,leo jijini Dar es salaam amesema kuwa hali ya lishe nchini hairidhishi na tatizo la utapiamlo limeeendelea kuiathiri jamii ya watanzania.
Amesema takwimu
za mwaka 2010 zinaonesha kuwa asilimia 42 ya watoto walio na umri chini
ya miaka mitano wamedumaa, asilimia 16 wana uzito pungufu na asilimia tano wamekonda.
Aidha amesema asilimia 59
ya watoto wenye umri kati ya miezi sita hadi 59 wana upungufu wa damu,
asilimia 33 ya watoto chini ya miaka sita wana upungufu wa vitamin A”,
alisema Lyimo.
Pia
ameongeza kuwa asilimia ya wanawake walio katika umri wa kuzaa yaani
miaka 15 hadi 49 wanapata changamoto mbalimbali za
kiafya zinazosababishwa na lishe duni za upungufu wa damu,
matatizo ya ukosefu wa madini joto mwilini, upungufu wa uzito na baadhi
ya mama wajawazito kuwa na tatizo la ukosefu wa vitamini A.
Pia ameeleza kuwa tatizo la utapiamlo unaotokana na
ulaji unaozidi mahitaji kilishe linaendelea kuongezeka na unaathiri
zaidi kwa wakazi wa mijini na tatizo hili hupelekea magonjwa yasiyo ya
kuambukiza kama moyo, kisukari na kansa.
Kwa
upande wake Msaidizi wa Rais masuala ya lishe Dkt Wilbald Lorri amesema
kuwa ufumbuzi wa tatizo la lishe bora kwa jamii liko mikononi kwa
wanajamii wenyewe kujenga tabia ya kula matunda na mbogamboga vitu ambavyo hupatikana kwa wingi na urahisi katika maeneo yao.
Amefafanua
kuwa serikali imeweka msukumo katika kukamilisha mkakati wa taifa wa
lishe pamoja na mpango wake wa utekelezaji, kuanzisha kamati ya kitaifa
ya ushauri wa lishe nchini, kuanzisha dawati la lishe katika halmashauri
zote nchini pamoja na kuanzisha kasma ya lishe katika bajeti ya
halmashauri,kuingiza na kuimarisha masuala ya lishe katika kilimo na
uongezaji wa virutubisho katika mafuta ya kula, unga wa ngano na unga wa mahindi.
Aidha
wananchi wameombwa kujitokeza kwa wingi katika maonesho hayo
yatayofanyika kuanzia mei 15 na kufikia kilele chake mei 16 katika
viwanja vya Mnazi mmoja yakiongozwa na kauli mbiu isemayo " Lishe bora ni Msingi wa Maendeleo , Timiza Wajibu wako"
ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya atazindua kampeni ya uhamasishaji wa matumizi ya Lishe bora.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...