Ndugu zangu waTanzania wenzangu,

Sisi watanzania wapigania maendeleo - CHADEMA UK tumelazimika kuwasilisha majonzi yetu kwenu kwa njia hii, ikiwa ni katika kuonyesha mshikamano wa kitaifa kwa kujifariji na pia kuwafariji ninyi waTanzania wenzetu kutokana na tukio kubwa la kuhuzunisha sana ambalo limetokea hivi majuzi nchini mwetu huko mkoani Arusha.

Pamoja na kwamba pamekuwa na matukio kadhaa yaliyoikabili nchi yetu hili la Arusha tumeonelea tulisemee kwa njia ya kipekee,kwa sababu licha ya kwamba ni tukio la kigaidi, lisilokuwa na mantiki yeyote ile zaidi ya umwagaji damu wa raia wasio kuwa na hatia,bali pia utekelezwaji wake unaweza kutuachia athari kubwa sana kisaikolojia na kimahusiano kama tusipojaribu kulitathmini na kulitafakari kwa upekee wake.

Wakati ambapo sala na maombi yetu kwa sasa yawaeendee wafiwa na wale ambao wamedhurika moja kwa moja kimwili ama kisaikolojia kutokana na tukio hili, tunapenda pia kupongeza juhudi zilizofanywa na kila mmoja wetu aliyeweza kuwafikia na kutoa msaada wa aina moja ama nyingine kwa wahanga wa janga hili bila kujali tofauti ya vyama, itikadi, kabila, dini ama falsafa. Hiyo ndiyo Tanzania tunayoijua sisi. Pamoja na tofauti zetu nyingi ki hali,afya ama kipato, lakini kamwe hatubaguani katika misingi ya rangi, kabila ama dini. Na hili ndio haswa linalotusukuma sisi kuwasilisha huu waraka wa rambirambi kwenu ninyi wenzetu leo hii.

Tuna imani kwamba vyombo vyetu vya usalama vitafanya utafiti wa kina kuchimbua na kutujuza chanzo cha ufedhuli huu, ni lazima sisi wenyewe pia tufarijiane kwa maombi, michango na tafakuri mbalimbali zenye kutiana moyo katika kipindi hiki kigumu kwetu sote. Tuna imani kwamba yeyote aliyehusika katika mkakati huu atapatikana na kupewa adhabu inayostahili.

Kwetu sote watanzania, huu ni wakati muafaka kuonyesha mshikamano wetu kuwatumia ujumbe hao wachache wenye nia mbaya kwamba waTanzania tumeundwa kutoka jumuiya ya makabila zaidi ya mia moja, wenye asili, rangi, dini na madhehebu mbalimbali na wasioamini. Na kati yetu wote sisi ni marafiki na ndugu, wengine ni ndugu wa damu kabisa, kupitia ndoa, wazazi n.k. Hivyo sisi hatuwezi kubaguana wala kuwa na chuki miongoni mwetu kwani hiyo si asili yetu. Na yeyote yule atakayejaribu kupandikiza mbegu hii chafu miongoni mwetu tumkatae na kumchukilia hatua stahiki kumtokomeza yeye na kundi lake.

Ujumbe wetu kwa watanzania ni huu:

HII NI VITA DHIDI YA UMOJA WETU WA KITAIFA NA SIYO KUNDI AU IMANI FULANI.

Asanteni sana, 
Mungu awabariki nyote. 
Mungu alibariki taifa letu Tanzania.

Kwa niaba ya CHADEMA UK        
G Mboya
Secretary

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 7 mpaka sasa

  1. Hiiimetulia wakubwa! nawakubali!

    ReplyDelete
  2. AnonymousMay 08, 2013

    Kwa hakika ni ujumbe murua ulio na sura ya kitaifa.Huo ndio utanzania,na kwa hakika ndivyo hasa tunavyopaswa kuishi.MUNGU ibariki nchi yetu.

    ReplyDelete
  3. AnonymousMay 08, 2013

    Mpaka sasa hakuna ukakika kamili kama ni vipi:

    1.Pana mivutano ya Waumini wa Dini ndani kwa ndani Makanisani Arusha,

    -Pana Mogogoro wa muda mrefu wa KKKT tulishuhudia silaha za moto zikitumiwa ktk mgogoro miaka ya 1997-1999,

    -Pana Kibwetere mmoja wa Kanisa la Kilokole Arusha alichangisha waumini Mil. 500 halafu akafanyia mipango isiyoeleweka, wauimini wakaja juu.

    2.Siasa za Jazba zimetawala sana ktk Arusha ya sasa.

    Arusha sasa ni mji wa maandamano kila kukicha, biashara hazifanyiki ipasavyo tofauti na ilivyokuwa zamani Arusha ilikuwa ni mji wa fedha na sasa ni mji wa Siasa za chuki na visasi.

    Hivyo kwa msingi huo hatuwezi kujua kwa haraka inawesekana ni ktk hili.

    3.Waarabu wageni Raia wa Saudi Arabia waliokamatwa na kushikiliwa ni kuwa sio watuhumiwa isipokuwa wanafanyiwa uangalizi kwa kile walicho onekana wakisafiri kuelekea Nairobi siku moja baada ya tukio...tusije tukajenga mtazamo wa moja kwa moja dhidi ya Misimamo ya Kigaidi kutoka kwa Waarabu kwa kuwa ''wavumao ni wachache, lakini na wengine wengi wamo pia''

    ReplyDelete
  4. AnonymousMay 08, 2013

    Nia waTZ tunayo ya kulindaa umoja wetu. Lakini wachache wenye nguvu zao wanatuharibia.Kuna mdau mmoja kwenye blog hii aliandika" ukiona kero imeshindikana kutanzuliwa ujue kuna kigogo nyuma."

    Aliendelea kutoa mfano wa ajali za barabarani. Haziishi kila kukicha. Madereva hawako tayari kufuata sheria za barabarab. Kumbe wenye magari ni maafande, mawaziri , wabunge n.k

    Na huu ugaidi hauko mbali kukamata. Itategemea atakayekubali kumfunga paka kengele.

    ReplyDelete
  5. Hakika huu ujumbe umeandikwa na Mtanzania wa kweli. Naomba wachangiaji tuache kupotisha maana ya ujumbe huu. Tuwaze Kama Watanzania natuache kuweka maslahi binafsi mbele. Mungu atusaidie Uzalendo wa enzi za Mwalimu urudi tena!

    ReplyDelete
  6. AnonymousMay 08, 2013

    Ninyi mnaotoa MAKALA hii mrudi TZ na siyo mbakie huko Uingereza wakati chama chenu kinafanya vibaya nchini na hasa hukohuko Arusha ambako kumekuwa ZAIDI YA DODOMA KWENYE MAKAO MAKUU YA SERIKALI NA BUNGE ni kuwa ARUSHA YA SASA IMEGUBIKWA NA SIASA KAMA MDAU WA 4 ANAVYOSEMA.!!!

    Mlitakiwa Makada wa Chama mshuke kutoka huko UK mtinge Arusha ili kukinusuru chama chenu kinacho boronga kila kukicha na sio kutoa makala pekee!

    ReplyDelete
  7. AnonymousMay 09, 2013

    HAPO NDIPO TUTAMKUMBUKA MWALIMU, NA TUSIMUONE. UONGOZI SIO MCHEZO.MWL ALISIMAMA KWA WAKOLONI NA KWA MAKABURU NA TUKASHINDA. JE, VIONGOZI HAWA WA SASA WANASHINDWA VIPI KUTHIBITI HALI YA USALAMA NDANI YA NCHI? KAMA MDAU ALIVYOSEMA HAPO JUU, JUU YA AJALI BARABARANI! NA SASA WATU KUUWAWA OVYOOVYO TU! JE,KAMA WATU WANAUWAWA MUTAONGOZA NANI KESHO?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...