Profesa Said A Mohammed 
SEHEMU YA KWANZA

Profesa Said A Mohammed umeandika vitabu vingi. Ama kweli wewe ni hazina ya fasihi ya Kiswahili ambaye hujapata heshima inayokustahili. Najua hupendi kusifiwa – lakini lazima tukuthamini ungali hai maana wewe fahari yetu Waswahili. Hata ukiweka neno “Tanzanian Novelists”, “Zanzibar Writers”, au “Tanzanian Writers” katika Wikipedia hutajwi. Unadhani kwanini wengi  hasa Tanzania bara na visiwani hawakufahamu ipasavyo?

Mwandishi : Said A Mohammed
 Kama nilivyokueleza katika mkumbo wa masuali uliyoniuliza mwanzo hapo kitambo, Watanzania na zaidi Wazanzibari hawana utamaduni wa kusoma vitabu vya fasihi. Kwa hivyo hawajapata ari wala mwamko wa kujali na kuthamini fasihi yenyewe na waandishi wake. Kweli kuna wachache ambao wanatangazwa katika vyombo vya mawasiliano, lakini mimi simo katika orodha ya waandishi hao. Hili ni suala la vyombo vya habari ambavyo mara nyingi huwatukuza wale ambao wanataka wao watukuzwe. 
Vilevile kuna wasanii wanaopenda kujipeleka mbele ili wasikike na hata kuwa na fikra kwamba waandishi wengine wadidimie. Kwa bahati mbaya au labda kwa bahati nzuri, mimi si mtu wa kimbele mbele. Naamini sana maneno ya wahenga kwamba Kizuri chajiuza na kibaya chajitembeza.

Katika dunia ya sasa kujipeleka mbele ili usikike bila umakinifu, ndilo jambo linaloharibu mambo mengi ikiwemo sanaa ya lugha. 
Vipawa vinadharauliwa na sanaa tunazokutana nazo ni sanaa zinazokuzwa tu bila ya kupitiwa kwa kina na kujadiliwa. Chambilecho, gwiji wetu wa fasihi, Profesa Ebrahim Hussein, hakuna fasihi tena kwa maana ya fasihi. Hakuna wasomaji wazingatifu. Hakuna uhakiki kwa maana ya uhakiki. Kuna fikra ya kwamba chochote kile ni sawa. Shairi, riwaya, hadithi fupi au tamthilia ikiwa ina sura ya tanzu inayohusika, basi ni fasihi tu kwa maoni ya wengi.  
Fasihi haipo. Wasomaji hawapo. Umakinifu wa fasihi haupo. Uhakiki umepotea. Hata wale ambao tunawatarajia kufanya hivyo hawashughuliki na kusoma, kuandika, kuhakiki na kuzitangaza kazi za fasihi ya Kiswahili. Sisi waandishi hatuwezi kujitetea. Wanaojitetea na kuwaponda wenzao ndio katika hao wanaowekwa mstari wa mbele na wanaojitapa kuwa wanajua hata kuandika kazi za waandishi wenzi wao.    BOFYA HAPA KUSOMA MAHOJIANO YOTE

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...