Wawakilishi wa Benki ya Dunia na Timu ya Mradi wa
Kuendeleza Miji Tanzania (TSCP) ulio chini ya OWM-TAMISEMI, wakikagua ujenzi wa
Mifereji jijini Mwanza wakati walipokuwa na ziara ya kutembelea miradi hio na
kuona maendeleo yake.
Stnedi mpya
ya Mabasi ya Dala dala iliyopo katikati ya mji wa Kigoma, Ni moja kati ya
matunda ya Mradi wa Kuendeleza Miji hapa nchini
(TSCP) chini ya OWM-TAMISEMI.
Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda (wa pili kulia), Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI,
Hawa Ghasia (wa pili kushoto), Mkurugenzi wa Benki ya Dunia – Tanzania, Philippe Dongier (kulia), pamoja na Mkurugenzi wa
Uendelezaji wa Miji (OWM-TAMISEMI), Anna Mtani (kushoto) katika tukio la
Uzinduzi wa mradi wa kuboresha Miji wa ULGSP, mradi uliozaliwa na mradi Mkakati
wa Undelezaji Miji (TSCP) chini ya OWM-TAMISEMI kwa mkopo wa Banki ya Dunia.
Ujenzi wa Dampo Jijini Arusha, wa TSCP, mradi chini ya
OWM-TAMISEMI, ukikaguliwa na wawakilishi wa Banki ya Dunia na timu ya TSCP.
Takwimu zinaonyesha mabadiliko ya idadi ya wakazi
vijijini kwenda mijini ni kubwa. Katika nchi ya Tanzania idadi ya watu waishio
mjini wataipiku idadi ya watu waishio vijijini ifikapo mwaka 2030. Tanzania pia
upatikanaji wa miundombinu ni hafifu kwa sekta zote, na hivyo ni vigumu kwenda
sambamba na ongezeko la idadi ya watu.
Tanzania
kama zilivyo nchi nyingi zinazoendelea, imekuwa ikikabiliwa na changamoto
mbalimbali za maendeleo ya miji zikiwemo; ongezeko la watu kwa kasi mijini;
miundombinu isiyokidhi mahitaji ya uendeshaji wa miji; uwezo mdogo wa
rasilimali kwa ajili ya kutoa huduma toshelevu za jamii na kupanuka kwa kasi
kwa maeneo ya miji bila kuzingatia taratibu za Mipango miji na Usimamizi
usiokidhi kasi ya maendeleo ya miji katika Halmashauri zetu.
Hata hivyo jitihada zinazoendelea kufanyika nchini
Tanzania katika miradi mbalimbali zitaleta ahueni ya tatizo linalofikiriwa
kutokea, ikiwa ni pamoja na miradi ya TSCP, Mpango wa Kuimarisha
Serikali za Mitaa Mijini (ULGSP) na hata mradi unaofanana na TSCP na ULGSP,
mahususi kwa Jiji la Dar es Salaam, (Dar es Salaam Metropolitan Development Project
- DMDP), ulio katika
mchakato wa kujiandaa kwa utekelezaji
wake.
Mradi wa uendelezaji Miji (TSCP) unaoendelea kutekelezwa katika Miji 7
nchini (Arusha, Dodoma,Tanga, Mbeya, Mwanza, Mtwara na Kigoma), umezaa matunda
kwa mradi mwingine wa ULGSP. Hali hii ilielezwa rasmi na Waziri Mkuu, Mizengo
K. Pinda (Mb.) wakati akizindua mradi huo wa ULGSP – 18 juni, Kuringe Hall –
Moshi.
Akitoa pongezi zake kwa timu ya TSCP, alisema kuwa mafanikio
yaliyoonekana katika mradi wa TSCP yamerahisisha kupatikana kwa mkopo mwingine
kutoka Banki ya Dunia kwa ajili ya kuendeleza azma hiyo hiyo, mradi huo umejikita
katika kuimarisha Halmashauri za Miji 18, ambazo ni Miji yote iliyobaki ya
Tanzania Bara, na mradi utagharimu kiasi cha Dola milioni 255 kwa kipindi cha
miaka mitano.
Aidha Mhe. Pinda alieleza kuwa jambo muhimu sana la kuzingatiwa na
kuhakikisha kuwa mradi huu unatekelezwa kwa kiasi cha watu kujidhihirishia
wenyewe kwa kuona kwa vitendo mafanikio, alieleza kuwa Serikali haitafumbia
macho uzembe au ubadhirifu wa fedha au vifaa utakaosababisha kazi hii kukwama
au kutekelezwa chini ya kiwango.
Pia Mhe.Pinda alisisitizia Wananchi kushirikishwa kikamilifu, alisema;
“Nasisitiza wadau wote washirikishwe katika ngazi zote na taarifa za
utekelezaji wa mradi ziwekwe wazi ili wadau wote wajue, watoe maon ya kukosoa
au kuboresha”. Aliendelea kusema; “Kwa wale wanasiasa wenzangu, ni fursa ya
kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha mradi unafanikiwa kama tunavyotarajia”.
Aidha Mkurugenzi wa Benki ya Dunia – Tanzania, Bw. Philippe Dongier
alieleza furaha yake ya kuona maendeleo mazuri ya utekelezaji wa TSCP, na
kueleza kuwa ana matarajio makubwa zaidi na ULGSP. Alisema; “Lengo kuu
la Mpango ni kujenga na kuimarisha uwezo wa Halmashauri kutoa huduma na
usimamizi wa Miji. Kupitia mpango huu,
mabadiliko ya ufanisi ya muda mrefu yanatarajiwa katika maeneo ya Mipango Miji,
mfumo wa kudhibiti fedha, uwajibikaji, uendeshaji na matengenezo na ukusanyaji
wa mapato”.
Miji husika (18), imeshaandaa Mipango Mikakati tayari kwa kuanza
utekelezaji ifikapo mwezi Julai 2013.Mradi umelenga kuendelea
kuziimarisha Halmashauri za Miji katika maeneo makuu matano ili ziweze kutoa
huduma bora zaidi kwa kuzingatia sera ya Ugatuaji Madaraka (D by D). Maeneo yaliyolengwa ni pamoja na; Uboreshaji wa mfumo wa
Mipango miji, ukusanyaji wa mapato ya ndani hususan mapato yatokanayo na kodi ya
majengo, uboreshaji wa mifumo ya udhibiti wa fedha, manunuzi na masuala ya
mazingira na kijamii, uboreshaji wa mifumo ya utekelezaji, uendeshaji na
utunzaji wa miundombinu kwa ajili ya huduma za jamii, na kuboresha uwajibikaji
na uwazi. Na baadhi ya shughuli husika zitahusisha; ujenzi wa barabara, masoko,
maeneo ya kupumzika na kudhibiti taka ngumu.
ULGSP ni mradi wa kwanza katika
Bara la Afrika chini ya “Mpango kwa Matokeo” (Program for Results – P for R).
“Mpango kwa Matokeo” ni mbinu ya utoaji fedha kulingana na matokeo ya
utekelezaji malengo mliyojipangia. Chini
ya Mpango huu, Halmashauri husika zitafanyiwa tathmini ya utekelezaji wa vigezo
vilivyopangwa kila mwaka na fedha zitatolewa baada ya matokeo kuhakikiwa.
Mbali na mradi wa TSCP na ULGSP, Serikali
ya Tanzania ikishirikiana na Benki ya Dunia na Wadau wengine kuanzia
miaka ya 1990 imetekeleza Miradi ya Ukarabati wa Miundombinu Mijini [Urban Sector Rehabilitation Project (USRP)] kuanzia 1997 hadi
2004 kwa gharama ya dola za Kimarekani
million 104.9. Mradi huu ulitekelezwa katika miji 9 ya Tanga, Moshi,
Arusha, Mwanza, Tabora, Morogoro, Mbeya, Iringa na Dar es Salaam na Mradi wa
kuzisaidia Serikali za Mitaa zote (Local
Government Support Project - LGSP)
kuanzia 2004 hadi 2012 nao ulikuwa ni mkopo wa Benki ya Dunia kwa gharama ya dola za Kimarekani million 52.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...