TAASISI ya Aisha Sururu, imetoa msaada wa baiskeli maalum kwa mtoto
mlemavu, Saada Hamis Hamad (14), ambaye ni mshindi wa kwanza, kundi
maalum, katika mashindano ya kuhifadhi Quran Tukufu, kitaifa.
Saada ambaye mikono na miguu yake imelemaa, alikabidhiwa baiskeli hiyo
juzi jioni, na mwenyekiti wa taasisi hiyo, Aisha Sururu, ambapo
alisema ina mahitaji muhimu kwa mtu mwenye ulemavu, ikiwemo sehemu ya
kujisaidia.
Akizungumza mara baada ya kupokea baiskeli hiyo, aliishukuru taasisi
kwa kumsaidia kwa mambo mengi, ikiwemo kuibua kipaji chake cha
kuhifadhi Quran na kumsafirisha kwa mara ya kwanza.
Alisema tangu apate akili, amekuwa akijisaidia kwa tabu bila staha na
kwamba kupitia baiskeli hiyo, itamsaidia mambo mengi ikiwemo kuzunguka
maeneo mbalimbali, ambapo hapo awali alishindwa kwani ili kutoka
sehemu moja kwenda nyingine ilikuwa lazima abebwe.
"Kabla ya hapo nilikuwa nipo tu nyumbani, sikuwahi kupelekwa shule
wala kutoka nje ya mji wangu, lakini nashukuru nimejifunza mengi na
nimepata msaada huu,"aliongeza Saada.
Mtoto huyo, ambaye ni mkazi wa Mamoja, Pemba, alisema kuwa, ana ndugu
zake wanne, ambao wawili kati yao ni walemavu kama yeye isipokuwa kaka
yake wa kwanza ambaye alizaliwa akiwa mzima wa viungo.
Aisha, ambaye pia ni diwani wa viti maalum Ilala, aliwataka wahisani
wengine kujitokeza na kununua baiskeli mbili kwa ajili ya ndugu zake
Saada hasa mdogo wake ambaye anasoma chekechekea.
"Mdogo wake amekuwa akibebwa kwa ajili ya kupelekwa shule na
kuridishwa nyumbani, hivyo baiskeli hiyo itapunguza adha na kumsaidia
kuhudhuria masomo bila wasiwasi,"aliongeza.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...