Baraza la Katiba la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa lilikutana tarehe 26 Agosti, 2013 kujadili Rasimu ya Katiba mpya. Mkutano huo ulifanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.

Mkutano ulifanyika chini ya Uenyekiti wa Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kufunguliwa na mgeni rasmi, Waziri Mkuu Mstaafu, Dkt. Salim Ahmed Salim ambaye pia ni Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Balozi wa Tanzania nchini Misri na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa. Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Mabalozi Wastaafu, Wafanyakazi wa Wizara na Taasisi zilizo chini yake.

Wizara iliamua kuunda Baraza la Katiba kwa kuzingatia kuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ni Wizara ya Muungano; Rasimu ya Katiba imependekeza masuala ya Sera ya Nje kuendelea kuwa miongoni mwa masuala ya Muungano; na kuwa yako masuala yaliyopendekezwa kwenye rasimu ya Katiba ikiwemo mipaka, uraia na muundo wa muungano ambayo yanagusa majukumu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Baraza la Katiba la Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, liliazimia mapendekezo yafuatayo katika maeneo ya Mipaka, Muundo wa Jamhuri, Uraia wa Jamhuri na Sera ya Mambo ya Nje:-

1) Mipaka ya nchi iwekwe wazi mwishoni mwa Ibara ya 2 ili isomeke kama ifuatavyo: “Eneo la Jamhuri ya Muungano ni eneo lote la Tanzania Bara na Zanzibar ikijumuisha ardhi, maziwa na sehemu yake ya bahari (Territorial Waters) pamoja na anga kwa mujibu wa sheria za kimataifa;

2) Baraza pia lilipendekeza mabadiliko katika Muundo wa Jamhuri ya Muungano kwamba Muundo wa Serikali Mbili uliopo, uendelee na kuboreshwa kwa kuwekewa mifumo imara ya kisheria itakayoakisi maslahi ya pande zote mbili za Muungano ili kupunguza changamoto na manung’uniko kutoka kwa wadau wa Muungano.

3) Kuhusu suala la uraia katika Jamhuri ya Muungano; Baraza lilipendekeza kuwa suala la uraia wa nchi mbili kwa Mtanzania wa kuzaliwa litamkwe Kikatiba na Raia huyo asipoteze uraia wake wa kuzaliwa kwa sababu ya kupata uraia wa nchi nyingine. Uraia wa nchi mbili utatoa fursa kwa Taifa letu kufaidika kimaendeleo kutokana na kutumia rasilimali za Watanzania walioko nje ya nchi;

4) Kuhusu Uraia, Ibara ya 55(4) inayozungumzia kumpa uraia wa kuzaliwa mtoto atakayekutwa ndani ya mipaka ya nchi yetu, ambaye wazazi wake hawajulikani ni raia wa nchi gani, Baraza linapendekeza “….Uraia huo utasitishwa endapo uraia wa asili (wa nchi nyingine) wa mtoto huyo utagundulika na kuthibitishwa pasipo na shaka au kama itagundulika kuwa ulifanyika udanganyifu wa kumtupa kwa makusudi mtoto huyo kwa nia ya kupata uraia wa Jamhuri ya Muungano.”

5) Kuhusu Uraia wa kuandikishwa, Ibara ya 56(2), mtu aliyefunga ndoa na raia wa Jamhuri ya Muungano anaweza kutuma maombi ya kuandikishwa kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano baada ya kuomba uraia wa Muda wa kuishi nchini kama mwanafamilia wa ndoa (dependant) mpaka ndoa iwe imedumu kwa miaka kadhaa (miaka itamkwe na sheria)”.

6) Kuhusu Sera ya Mambo ya Nje; Baraza linapendekeza mabadiliko katika Ibara ya 12 ya rasimu kwamba Misingi (Principles) ya Sera ya Mambo ya Nje ijumuishwe badala ya majukumu ya Wizara kwa kuwa majukumu hubadilika na nyakati. Aidha, Katiba ilielekeze Bunge litunge Sheria itakayosimamia utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania.

7) Kuhusu Ibara ya 39 (3) inayohusu raia wa Tanzania kutokupelekwa nje ya nchi kujibu mashtaka au kufanyiwa mahojiano ya aina yoyote bila ya ridhaa yake, Baraza linapendekeza Kifungu hicho kifutwe, kwa sababu kuna ugumu wa haki inayotajwa kwenye Kipengele hiki kutekelezeka bila kuathiri wajibu ya kimataifa wa nchi (international obligations) katika makosa ya jinai, kwa kuwa ni vigumu sana kupata ridhaa ya mtuhumiwa kuhojiwa kwa makosa aliyoyatenda au anayotuhumiwa kuyatenda.

WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 4 mpaka sasa

  1. Mm naona hapa kwenye uraia wa mtu kuowa au kuolewa patazamwe kwa upana wa hali ya juu sn coz hii midada yetu inayotujazia mijambazi ya nchi jirani na mitapeli toka west africa kama naigeria na migana kwahiyo iwekwe sheria kali ikigundulika jitu limeowa dada zetu kwa kuutaka tu uraia watz nakupata passipot yetu kisha akaichafue kwa kubebea madawa ya kulevya basi uraia wake utenguliwe na kuludishwa kwao au afungwe maisha jela,na huo mdada upewe azabu kali ili iwe fundisho kwa wengine wenyekupapatikia mijambazi na mitapeli,na wadosi pia wamulikwe wana tabia ya kuletana kama kuku toka kwao iwe mwisho wao,ni hayo tu kwaleo ndugu zangu au nyie wenzangu mnaonaje kwa hayo?,,naitwa mdudu KAKAKUONA mwenye macho ma3

    ReplyDelete
  2. Uzuri wa nchi yetu ni kuwa serikali ikitamka, imetamka. Nani bungeni atakayekataa maazimio hayo. Uraia wa nchi mbili utapita bila wasiwasi. Poleni sana wale mnaopinga.

    ReplyDelete
  3. Mambo ya Nje mmejipanga vilivyo. Hongereni sana kwa maazimio haya yenye tija kwa nchi.

    ReplyDelete
  4. Mbona katika hayo maazimio hawajatamka bayana kuhusu uraia wa watoto waliozaliwa nje ya nchi to Tanzanian parent(s)? Je hawa watoto wenye uraia wa nje simply because wamezaliwa ughaibuni watapata uraia wa Kitanzania as well by default kwa sababu wazazi wao ni Watanzania? Mwenye kujua kuhusu hili naomba ajibu. Asante.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...