Kijana Jimmy Changchuu alieachana na matumizi ya dawa za kulevya akimkabidhi Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete picha aliyochora yeye na kijana mwenzake wakati vijana hao walimpomtembelea Rais Ikulu jijini Dar es Salaam leo.Vijana hao wanalelewa katika kituo cha Pilli Missanah Foundation kilichopo Kigamboni Jijini Dar es Salaam.
Vijana walioachana na Matumizi ya dawa za kulevya kutoka katika kituo cha Pilli Missanah Foundation kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam wakiwa katika picha ya pamoja na Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete ikulu jijini Dar es Salaam leo.Kulia pembeni ya Rais ni Mwanzilish Kituo hicho Bi.Pilli Missanah na watatu kushoto ni mfadhili mkuu wa kituo hicho Bwana Zacharia Hans Poppe(picha na Freddy Maro).

Rais Jakaya Mrisho Kikwete ameiagiza Wizara  ya Afya kupitia kitengo cha magonjwa ya akili  pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya nchini kushirikiana na Kituo cha Ushauri Nasaha cha Pili Misana Foundation, ambacho kinawasaidia  waathirika wa  madawa ya kulevya ili kiweze kuwahudumia watu wengi zaidi hapa nchini.

Rais Kikwete amesema hayo leo Ikulu alipokutana na  vijana walioachana na matumizi ya dawa za kulevya ambao wamepata ushauri nasaha na usaidizi kutoka katika kituo cha Pili Misana kilichopo  Kigamboni jijini Dar es Salaam.“Jamii lazima ishiriki katika utatuzi wa jambo hili, ni tatizo kubwa na linamgusa kila mtu na inabidi wote tushiriki katika kulipiga vita” Mhe. Rais amesema na kumpongeza Bi. Pili Misana na 

Zacharia Hans Pope ambaye ndiye mfadhili wa kituo hicho ambacho  tayari vijana wapatao 203 wamepatiwa huduma ya ushauri nasaha na kuweza kuachana na madawa ya kulevya na kurudia katika shughuli zao za kimaendeleo.

Rais Kikwete amesema tatizo la madawa ya kulevya ni la muda mrefu lakini hapo awali lilikuwa halisikiki sana kwa sababu jitihada za kuzuia madawa hayo zilikua hazitangazwi wala kufuatiliwa sana.

“Sasa hivi juhudi mbalimbali za kupambana na madawa ya kulevya zinatangazwa na hivyo kusikika sana na pia taarifa nyingi zinazohusiana na madawa ya kulevya zinawekwa wazi kwa jamii” Mhe. Rais amesema, na kueleza kuwa taarifa nyingi zinawekwa wazi na kutangazwa ili kushirikisha jamii katika kupambana na tatizo hili.

Kiasi cha vijana 35 leo wamefika Ikulu ambapo wametoka katika nyanja mbalimbali za kitaaluma, elimu na kijamii na pia umri tofauti kutoka miaka 14 hadi miaka 53. Kituo hicho kinahudumia watu wenye jinsia tofauti wake kwa waume kutoka sehemu mbalimbali nchini.

Rais Kikwete amesema Serikali inafanya jitihada kubwa sana za kuwasaidia vijana mbalimbali na bado itaendelea kutoa msaada huo, huku juhudi mbalimbali za kupambana na madawa hayo zikiendelea.

Naye mfadhili wa kituo hicho Bw. Zacharia Hans Pope ameitaka jamii kushiriki na kuwa karibu zaidi na vijana ili kuweza kusaidia katika mapambano ya madawa ya kulevya na athari zake nchini.

Imetolewa na;

Premi Kibanga,
Mwadishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu Dar-es-Salaam, Tanzania. 
13 August, 2013


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. kama haya mheshimiwa Rais anayafanya kutoka moyoni mwake ni jambo jema,mungu anaweza kumsamehe makosa yake,mwisho ajitahidi kuhusu wahamiaji haramu wasije hapo baaadae wakaharibu nchi yetu kama ilivyowahi kutokea huko kwao.

    s.makoye

    ReplyDelete
  2. Cha msingi ni kiasi gani anapambana na madawa ya kulevya?orodha aliyosema anayo mbona ana kigugumizi kuitoa mpaka leo,hapo tafsiri yake ni nini?kwamba anaogopa kukata tawi alilokalia?

    ReplyDelete
  3. Kwa kweli inaurahisha kwa hatua hii kuona wenyewe Waathirika wa Madawa wakiyakataa.

    Hadi Mhe. Raisi JK anacheka ktk Picha ya juu ?

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...