Mkurugenzi Mtendaji wa Taassisi ya Sekta Binafsi Nchini (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye (kushoto) akizungumza na wajumbe wa kamati maalumu ya taasisi hiyo inayoshughulikia uharakishwaji wa upatikanaji wa hati ya umiliki rasilimali ardhi na majengo (Land Title Deeds) jijini Dar es Salaam. Kulia ni afisa wa TPSF Bw. Adam Gahhu
------------------------------------------
TAASISI ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), imesema kukosekana kwa umiliki wa raslimali ardhi na majengo (Land Title Deeds) miongoni mwa watanzania wengi kutarudisha nyuma uharakishwaji wa kujipatia maendeleo hapa nchini.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Bw. Godfrey Simbeye alisema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa kikao cha kamati cha taasisi hiyo kilichokuwa kikijadili umuhimu wa kuwa na hati ya umiliki wa raslimali hiyo kuwa ni asilimia tatu tu ya watanzania mpaka sasa ndiyo wenye hati za umiliki huo.
“Tunashindwa kupata maendeleo kutokana na kwamba hatuna hati hizi ambazo zinatumika kuombea mikopo katika taasisi za fedha,” alisema Bw.Simbeye na kuongeza kuwa raslimali isiyohamishika  ndiyo inayokubarika zaidi katika kupata mikopo.
Alisema kikao walichofanya kilikuwa ni mwendelezo wa vikao vinavyoendelea kufanyika kwa ajili ya  kuungana  na vile vinavyofanywa na sekta ya umma katika mbinu za kutaka kurahisisha upatakanaji na kutaka kuboresha mazingira ya biashara.
Alisema pia viwango vya Benki ya dunia vinaonyesha Tanzania ipo nyuma sana, hivyo kuna kila sababu ya kuhakikisha maboresho yanafanyika haraka ili kila mtu aweze kuwa na hati ya umiliki wa ardhi na majengo bila usumbufu.
Alisem mchakato wa raslimali hizo kutakiwa kuwa na hati za umiliki ulianzishwa mwaka 2009 na ilipofika mwaka 2010 serikali ilikubali lakini utekelezaji wake umekuwa wa kiwango cha chini sana.
“ Kwa sasa kamati yetu inajadili viwango vilivyowekwa na Benki ya Dunia na taarifa ya serikali ya utekelezaji wa mpango kazi wa maboresho ya mazingira ya biashara na uwekezaji (ROADMAP) katika kipindi cha robo mwaka ya tatu na nne ya mwaka wa fedha 2012/13,” alisema.
Alisema pia kamati hiyo imejichimbia kujadili kwa kina vikwazo mbalimbali vilivyopo katika kutekelezaji wa makubaliano hayo ili kuja na mapendekezo ya kuisukuma serikali kuharakisha swala hilo kwa maslahi ya taifa na watu wake.
Alifafanua kwamba sekta binafsi inahitaji kuona mtu anayetaka kuanzisha kiwanda hapa nchini anaanzisha bila ya kuchukua muda mrefu kupata umiliki wa ardhi.
Alisisitiza kwamba serikali inahitajika kuiwezesha Wizara ya Ardhi ili iweze kuwa na uwezo mkubwa wa upimaji ardhi na utoaji vibari vya umiliki ardhi na pia kuwa na mipango ya matumizi ya ardhi endelevu.
Alisema Millenium Challenge Corporation kutoka Marekani imetenga dola milioni 800 za kimarekani ambapo sehemu ya fedha hizo zitatumika katika maswala ya ardhi ikiwemo kupima na kutoa hati za umiliki.
Mshauri wa, maswala ya wajasirimali TPSF, Dkt. Donath Olomi alisema mrorongo wa kuandikisha usajiri wa majengo na ardhi ni mgumu na mazingira hayo ndiyo yanarudisha nyuma maendeleo ya nchi.
“Pia  mfumo mzima wa utoaji wa vibari kwa mtu anayetaka kufanya tathimini ya ardhi au jengo, survey ya ardhi, kubadilisha hati ya umiliki ardhi au jengo na usanifu wa majengo bado unaukiritimba mkubwa,” ambao kikosi kazi chao kitakuja na mapendekezo ya kuitaka serikali kuondoa hali hiyo.
Alisema nchi ikifikia viwango vya kimataifa vya utoaji wa hati za umiliki ardhi na majengo na vibari mbalimbali umasikini utapungua kwa asilimia kikubwa. 


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...