Na Dixon Busagaga wa Globu ya Jamii, Moshi.
MAMLAKA ya maji safi na maji taka mjini Moshi(MUWSA) imefanikiwa kunasa moja ya nyumba ya kisasa iliyopo eneo la Chekereni Weruweru ambayo mmiliki wake anadaiwa kujiunganishia maji kinyume cha sheria.
Mbali na wizi huo pia Kigogo huyo amejenga tanki la maji la chini linalokadiriwa kuwa na ujazo wa lita 10000 za maji lingine dogo lenye ujazo wa lita 2000 ambalo pembeni yake imejengewa mashine maalumu ambayo imekuwa ikitumika kupandisha maji.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka mamlaka ya maji safi na maji taka mjini Moshi,MUWSA na kuthibitidhwa na ofisa habari wake Dorah Killo zilionesha mmiliki huyo hakuwahi kuunganishiwa maji katika nyumba yake hiyo ambayo pia imetia shaka katika ujengwaji wake hadi kukamilika. “Kwa sasa tunashindwa kutoa taarifa za huyu mmiliki wa nyumba hii kwa sababu hatuna taarifa zake ofisini ingawaje zipo taarifa zisizo rasmi kuwa ni mkaguzi wa mahesabu na kama ulivyoona amejiunganishia maji pasipo kufuata utaratibu, hiii ni hujuma kwa mamlaka lakini pia ni hujuma kwa serikali…tutamchukulia hatua mtu huyu zinazomstahili”alisema Killo.
"Kumekuwepo na upotevu mkubwa wa maji katika kijiji hiki, kwani kwa siku tumekuwa tukizalisha maji mita za ujazo 1,200, lakini asilimia 80 ya maji hayo hupotea, na upotevu huu husababishwa na watu kujiunganishia maji kinyume cha sheria," aliongeza Killo.
Alifafanua kuwa Mamlaka hiyo kwa sasa hupoteza asilimia 28 ya maji yanayozalishwa ambapo asilimia 80 ya upotevu wa maji kati ya hizo inatoka katika kijiji cha Chekereni Weruweru.
Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Katanini katika kijiji cha Chekereni Weruweru, Yahaya Salum,alikiri kufuatwa na maofisa wa Muwsa na kuonyeshwa namna mkazi wa kitongoji hicho alivyojiunganishia maji kinyume cha sheria na kuwaomba wananchi kuacha mara moja wizi huo.
Maofisa wa mamlaka ya maji safi na maji taka mjini Moshi(MUWSA)wakifukua sehemu inayodaiwa kuunganishwa maji kinyemela kwenda katika moja ya nyumba ambayo haikuwahi kuunganishiwa maji na mamlaka hiyo.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...