JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

Awamu ya Pili ya Operesheni Kimbunga imeweza kukamata majambazi ya kutumia silaha 67 na wahamiaji haramu 134  katika kipindi cha wiki moja tangu  kuanza kwake Septemba 21hadi Septemba 27 mwaka huu katika mikoa ya Kagera, Kigoma na Geita.
Silaha zilizokamatwa ni pamoja na bunduki aina ya SMG Moja, Pistol Moja na Magobole 17 pamoja na risasi 115 zikiwemo za bunduki aina ya SMG 102 na Risasi za Pistol 13. Aidha, Magazine mbili zilikamatwa pamoja na Sare za Jeshi la Burundi.
Wahamiaji haramu waliokamatwa wengi wao ni kutoka nchi za Burundi ambapo raia wake 114 walikamatwa wakiishi nchini kinyume na sheria wakati raia wa Rwanda 20 walikamatwa katika kipindi hicho.
Aidha, watu Watatu walikamatwa kwa tuhuma za kuhifadhi wahamiaji haramu nchini huku Lita 271 za gongo , ngozi ya Mbwea, Bangi kilo Tatu na Makokoro 12 vilikamatwa wakati wa operesheni Kimbunga awamu ya Pili ikiwa katika wiki yake ya kwanza.  
Wakati huo huo, Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera imejipanga kukabiliana na tatizo la wahamiaji haramu ili kuhakikisha kuwa tatizo hilo linafikia mwisho wake na kuwapa nafasi wananchi kufanya shughuli zao za kijamii na kimaendeleo bila ya hofu ya kufanyiwa uhalifu na wahamiaji haramu.
Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Bi Dari Rwegasira amewaambia          Maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata aliokutana nao katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, mwishoni mwa wiki iiliyopita kuwa kuanzia sasa kila kiongozi, kuanzia ngazi ya Kiijiji/Mtaa, Kata, Tarafa na Wilaya, atawajibika kwa jinsi anavyoshughulikia kumaliza tatizo la wahamiaji haramu katika eneo lake.
Wilaya ya Karagwe ni moja ya wilaya zenye tatizo sugu la wahamiaji haramu ambao wanatuhumiwa kuwanyanyasa wananchi katika baadhi ya maeneo ya Wilaya hiyo, kwa kuendesha vitendo vya wizi wa mifugo, kuvamia maeneo ya kilimo, na pia kuchochea uhalifu wa unyang’anyi wa kutumia silaha na kusababisha mauaji.
Wahamiaji hao haramu wanashutumiwa kufanya baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Karagwe yasipitike kwa urahisi, mojawapo ikiwa ni eneo la msitu wa Kimisi, ambapo eneo hili limekuwa na matukio mengi ya ujambazi wa kutumia silaha na wananchi kuvamiwa na kuibiwa mali zao na hata wengine wakipoteza maisha katika matukio hayo.
Maazimio kadhaa yalitolewa katika kikao hicho kati ya Mkuu wa Wilaya ya Karagwe na Watendaji Wakuu wa Wilaya hiyo, ikiwa ni pamoja na kuwa:
·         Viongozi kuanzia ngazi ya Kijiji/Kitongoji, Kata hadi Tarafa kutia saini mkataba wa kushughulikia wahamiaji haramu, majambazi wa kutumia silaha na wafadhili wao, mifugo haramu inayoingia nchini kutoka nchi jirani pamoja na vitendo vyote vya uhalifu katika maeneo wanayoyaongoza.
·         Kiongozi yoyote wa Kijiji, Kata au Tarafa atakayeshindwa kushughulikia wahamiaji haramu walioko katika eneo lake atawajibishwa.
·         Wahamiaji wote haramu ambao bado wapo katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo wasakwe na kurejeshwa kwao mara moja.
·         Msako uanzishwe mara moja kuwasaka wahamiaji haramu wote ambao wamejificha katika maeneo ya misitu na ranchi za mifugo zilizoko katika wilaya hiyo kwa kuvishirikisha vyombo vyote vya Utawala na vya Ulinzi na Usalama vilivyoko katika Wilaya hiyo.
·         Kila kijiji kiwe na takwimu sahihi za wageni waliopo katika maeneo yao.
·         Wahamiaji haramu wote wanaorejeshwa kwao wasipewe nafasi ya kurudi tena nchini na mwananchi yoyote atakayebainika kuwapokea au kuwasaidia kurejea  atolewe taarifa haraka ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.
·         Vibali vyote vya Ukazi vilivyotolewa kwa wageni mbalimbali sasa vitakaguliwa upya ili kuhakiki uhalali wake.

Imeandaliwa na: 
Timu ya Habari ya Operesheni Kimbunga

Septemba30,2013

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 6 mpaka sasa

  1. huko ambako hata raia huwa na wasiwasi wa uraia wao.

    huko ambako hawatoki wakuu.

    ukisikika unaongea kiha dar basi we mrundi au mkongo. kubaguliwa nchini mwako.

    ReplyDelete
  2. hamna operesheni za hivi moshi, arusha, mara, mtwara, wala rukwa. viongozi wa nchi wametokea huko. wengine ndo hunyanyaswa.

    ReplyDelete
  3. Bigup Kimbunga, ila kwa nini vyombo vya ulinzi na usalama visubiri operation maalum ndo vionyeshe kama vinaweza kufanya kazi? siku zote mnatakiwa kutenda kazi kwa namna hiyo ili nchi iwe salama.Mpaka JWTZ waingilie kati jamani ndo kazi ifanyike?Polisi na uhamiaji mnaonyesha udhaifu mkubwa hasa jinsi mnavyopenda rushwa.

    ReplyDelete
  4. safi sana serikali najivunia utanzania for real.big up sana MHE rais

    ReplyDelete
  5. Ninafikiri hili zoezi la Operesheni Kimbunga litekelezwe kwa kushitukiza na si kwa kutangaza Ratiba za sehemu linako endelea!

    Kwa mtaji huo, Wahamiaji Haramu ni kama Magaidi wa Al-Shabab au Al-Qaida ni wazi waakuwa wanaepuka Mikoa na Wilaya hizo wasikamatwe.

    ReplyDelete
  6. naipongeza sana serikali kwa hatua hii nzuri. Lakini serikali isifanye jambo hili ki-operation bali liwe endelevu. Wekezeni kwa wananchi ili mpate taarifa kuhusu wageni wasiofuata sheria za nchi. Pia nashauri operation hii isambae na maeneo mengine ya nchi kwani hao jamaa wanaweza kuhamia mikoa ambayo zoezi hilo halifanyiki na wakaendeleza uharamia wao.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...