Katibu Mkuu wa SHIMIWI Bw.Ramadhani Sululu akiongea mapema leo ofisini kwake kuhusu ufunguzi wa mashindano ya michezo ya SHIMIWI itakayofanyika mjini Dodoma Septemba 21 mwaka huu.
Timu za mpira wa miguu za Hazina na Ofisi ya Mkoa Dodoma zinatarajiwa kucheza mechi ya ufunguzi wa mashindano ya michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayohusisha watumishi wa umma katika viwanja vya Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) .
Katibu Mkuu wa SHIMIWI Bw. Ramadhani Sululu alisema hayo mapema leo alipokuwa akiongea kuhusu ufunguzi wa mashindano hayo ambayo yanayotarajiwa kuanza Septemba 21 mkoani Dodoma.
Alisema timu zote zinatakiwa kukamilisha usajili haraka iwezekanavyo na kuwahi kufika mjini Dodoma kabla ya tarehe 20 Septemba mwaka huu.
“Timu zote zitakazoshiriki katika mashindano zinatakiwa kufika katika kituo cha mashindano siku moja kabla ya kuanza mashindano na timu itakayochelewa kufika katika kituo na kukuta michezo yake imepita itahesabika kuwa imepoteza michezo hiyo”alifafanua Bw.Sululu.
Aidha,alizitaja timu nyingine zitakazofungua pazia la michuano hiyo kuwa ni Bunge na TAMISEMI kwa upande wa mpira wa pete, Wizara ya Kilimo na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa upande wa timu za kamba wanawake na wanaume.
Sambamba na ufunguzi huo Bw. Sululu alisisitiza juu ya wachezaji kupima afya zao kabla ya kuanza kwa mashindano ili waweze kushiriki kikamilifu na kujua kama wako fiti kwa michezo hiyo yenye ushindani mkubwa miongoni mwa watumishi.
“Kila mchezaji anawajibika kupimwa afya yake na daktari wa michezo kabla ya kuanza michezo”alitahadharisha Bw. Sululu.
Michezo ya Watumishi wa Serikali (SHIMIWI) imekuwa ikijizolea umaarufu siku hadi siku kutokana na ushindani wake na nidhamu inayoonyeshwa na washirikihivyo kutoa picha tofauti na mashindano mengine yanayoendeshwa hapa nchini.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...