Balozi wa Japan hapa nchini Mheshimiwa Masaki Okada (kushoto) amemthibitishia Waziri wa Ujenzi kuwa upanuzi wa barabara inayoanzia eneo la Bendera Tatu hadi KAMATA jijini Dar es Salaam, utaanza mapema mwakani. Balozi huyo alikutana na Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa John Pombe Magufuli (kulia) mwishoni mwa wiki alipomtembelea ofisi kwake kuzungumzia utekelezaji wa miradi mbali mbali inayofadhiliwa na nchi ya Japan hapa Tanzania.
Ilielezwa kuwa, kwa hivi sasa mchakato wa kumpata mkandarasi umeanza nchini Japan na imepangwa kuwa hadi ifikapo Januari 2014 mkandara awe amepatikana.
Mchakato huu utahusisha pia zabuni ya ujenzi wa barabara ya juu katika eneo la TAZARA kwenye makutano ya barabara za Nelson Mandela na Nyerere pia hapa jijini Dar es Salaam.
“Taratibu zote zimekamilika na kwa hivi sasa tuko katika hatua ya kupata makandarasi wawili wa kujenga miradi hiyo miwili na mchakato huu utakamilika mwezi Januari 2014” Balozi Okada alisisistza.
Mheshimiwa Magufuli kwa upande wake alimhakikishia Balozi huyo wa Japan kuwa taratibu za kusafisha eneo hilo la mradi zimekwishafanyika na barabara hiyo iko tayari kwa kuanza ujenzi.
Sehemu ya barabara kuanzia Bendera Tatu hadi KAMATA eneo la Gerezani imekuwa ikisababisha msongamano mkubwa kwa watumiaji wa barabara ya Kilwa kutokana na barabara hiyo kuwa nyembamba.
Hivyo kukamilika kwake kutakuwa ni faraja kubwa kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na watumiaji wengine kuelekea mikoa ya kusini mwa nchi yetu.
Katika kikao hicho ulizungumziwa pia mradi wa Mwenge – Tegeta ambao ujenzi wake uko katika hatua za mwisho.
Ilielezwa kuwa Mkandarasi kwa sasa anaendelea kukamilisha ujenzi wa madaraja mawili makubwa pamoja na marekebisho ya maeneo yaliyobainika kuwa na dosari.
Tanroads kwa upande mwingine wanafanyia tathmini ombi la mkandarasi Konoike anayeijenga barabara hiyo akiomba nyongeza ya muda wa kumamilisha mradi huo kutokana na ongezeko la kazi lililojitokeza wakati akiitekeleza kazi hiyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...