Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa ufafanuzi kuhusu kauli mbalimbali zilizotolewa na baadhi ya wanasiasa kuwa imekuwa ikiingilia uhuru wa wananchi wa kutoa maoni kuhusu Katiba Mpya katika mikutano ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya iliyomalizika hivi karibuni.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo (Alhamisi, Oktoba 3, 2013), Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Joseph Warioba amesema siku zote Tume yake imekuwa ikitekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na kuwataka wanasiasa hao kujadili rasimu iliyotolewa badala ya Tume au Wajumbe wake.

“Moja ya kazi za kisheria za Tume ni kutoa elimu kwa umma, na ni kazi ya wakati wote,” alisema Jaji Warioba wakati akijibu swali la waandishi waliofika ofisini kwake jijini Dar es Salaam kutaka ufafanuzi wa kauli ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Bw. Abdallah Bulembo.

Bw. Bulembo amenukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari leo na jana (Alhamisi, Oktoba 3 na 4, 2013) akiwa mkoani Tanga akisema kuwa Tume ya Warioba imeacha kutekeleza majukumu yake na kuingilia uhuru wa wananchi wa kutoa maoni.

Kwa mujibu wa Tume, katika mikutano ya Mabaraza ya Katiba ya Wilaya, wananchi ambao walikuwa ni wajumbe wa Mabaraza hayo walikuwa na fursa ya kuuliza maswali na Wajumbe wa Tume walitoa elimu kuhusu hoja na maswali yaliyoulizwa kwa mujibu wa sheria.

“Sasa anaona (Bw. Bulembo) kuwa kutoa elimu ni dhambi,” alisema Mwenyekiti huyo ambaye amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Waziri Mkuu.

Katika ufafanuzi wake leo, Jaji Warioba pia alikumbusha kuwa Tume yake imekuwa ikifanya kazi katika mazingira magumu kutokana na kauli za wanasiasa mbalimbali na kuongeza kuwa, pamoja na kauli hizo, Tume yake inafarijika na kauli za kutia moyo wanazozipata kutoka kwa wananchi wa kawaida.

“Nilisema mwishoni mwa mwezi uliopita, wanasiasa wamekuwa wakitoa matamshi yaliyoifanya kazi ya Tume kuwa ngumu katika mikutano ya Mabaraza ya Katiba,” alisema na kuongeza:

“Matamshi mengine yalilenga Tume na wakati mwingine yalinilenga mimi binafsi au wajumbe wa Tume badala ya kuzungumzia rasimu,” alisema Mwenyekiti huyo anayeongoza Tume ya Mabadiliko ya Katiba yenye Wajumbe 32.

Jaji Warioba alisema Tume yake siku zote imekubali kukosolewa kwa kuamini kuwa kukosolewa ni jambo la kawaida lakini akaongeza kuwa ni vema wananchi na wanasiasa wakajadili rasimu ya katiba iliyotolewa badala ya watu au Tume.

“Nadhani wangezungumzia rasimu wangetusaidia sana, badala ya kuzungumzia Tume na watu,” amesema Jaji Warioba na kuongeza kuwa haamini kuwa kauli za viongozi hao wa kisiasa ndiyo misimamo ya vyama vyao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 2 mpaka sasa

  1. Jaji Warioba wewe usingekabidhiwa jukumu hilo kama ungekuwa si mweledi wa mambo hayo.

    Mbona hakukabidhiwa huyo Bulembo?

    Endelea na kazi yako kwani mwiba umekuwa mchungu kwa baadhi wa wanasiasa ndiyo maana wanapayuka tu.

    Sisi wananchi tunakuaminia endelea na msimamo wako pamoja na Tume yako na Mungu atawalinda nyote.

    ReplyDelete
  2. Hon J. S Warioba, ni wa pili kwa uadilifu, wa kwanza Nyerere. Hii ni vita na wewe ndiye Kamanda wa sisi wananchi tusiyo na msemaji Bungeni wala katika vyombo vingine vya maamuzi. Shikilia usukani na Mungu atakutuza.
    Wameingia uongozi kwa upanga wa pesa, hawawezi kuiva uadilifu.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...