Wizara ya Ujenzi kuanzia tarehe 01 Oktoba 2013 imefuta msamaha uliokuwa umetolewa awali kwa magari yaliyokuwa yanapimwa na kukutwa na ongezeko lisilozidi asilimia 5 juu ya viwango vilivyoweka kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani Na. 30 ya mwaka 1973 na maboresho yake.
Hatua hiyo ya Wizara ya Ujenzi imechukuliwa kutokana na baadhi ya wasafirishaji kuutumia vibaya mwanya huo kwa kuhakikisha kuwa, mbali na kuweka mzigo kwa mujibu wa sheria ambayo inaruhusu uzito usiozidi tani 56, wasafirishaji hao wamekuwa wakiongeza mzigo mwingine unaolingana na asilimia hiyo tano iliyokuwa imepewa msamaha wa tozo.
Hapo awali jumuia ya wasafirishaji iliwasilisha kwa iliyokuwa Wizara ya Miundombinu malalamiko kuhusu vipimo vilivyokuwa vikitolewa katika vituo vya mizani ya barabarani kwa wakati huo kwamba vilikuwa na dosari. Hivyo wakati tathmini ilipokuwa ikiendelea kuangalia usahihi wa vipimo hivyo kwa wakati huo, ndipo kibali kikatolewa cha kutotoza mzigo wowote uliozidi ndani ya asilimia 5 juu ya viwango vilivyowekwa kisheria.
Sehemu kubwa ya mizani inayotumika kwa sasa imethibitika kufanyakazi vizuri na baadhi yake ni mipya kabisa. Hata hivyo baada ya kufanyika tathmini zaidi ndipo ikabainika kuwepo kwa ujanja huo wa makusudi kwa baadhi ya wasafirishaji kuongeza kwa hiyo asilimia tano juu ya viwango rasmi. Mtindo huo umesababisha uharibifuu mkubwa katika baadhi ya barabara hapa nchini ambazo zimejengwa kwa fedha nyingi za walipakodi.
Kutokana na kuondolewa kwa msamaha huo wa tozo kwa uzito uliozidi ndani ya 5% ya viwango vilivyowekwa kisheria, msafirishaji atakayebainika kwenda kinyume na mwongozo uliotolewa na wizara, atatakiwa kupunguza mzigo huo au kupanga kulingana na maelekezo ya sheria na ikishindikana basi nyongeza hiyo italazimika kulipiwa mara nne ya tozo ya kawaida kulingana na matakwa ya Sheria ya Usalama Barabarani.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...