*Asikitishwa na idadi kubwa ya wasafirishaji wa dawa za kulevya 

 WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amewasili Beijing, China saa 10 leo jioni (Jumatano, Oktoba 16, 2013) na kuanza vikao ikiwa ni sehemu ya ziara ya kikazi yake ya siku tisa kwa mwaliko wa Serikali ya nchi hiyo. 
 Mara baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa Beijing, Waziri Mkuu alielekea kwenye nyumba ya wageni ya Serikali ya Diaoyatui ambako alipokea taarifa fupi kuhusu hali ya kisiasa na kiuchumi nchini China. 
 Akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Balozi wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali (Mst.), Abdulrahman Shimbo alisema sehemu kubwa ya utekelezaji wa miradi kati ya Tanzania na China iko chini ya mwamvuli wa FOCAC (Forum on Africa China Cooperation) ambayo inagawanyika katika maeneo sita. 
 Aliyataja maeneo hayo kuwa ni misaada (grants), mikopo ya masharti nafuu (preferential loans), mikopo ya kibiashara (preferential buyers credit), uwekezaji, ushirikiano maalum na ushirkianao wa kihistoria. 
 “Miradi mahsusi inayogharimiwa kwa pamoja baina ya Serikali ya Tanzania na China imeongezeka sana na inatarajiwa kufikia Dola za Marekani milioni 800 ifikapo mwaka 2014/2015,” alisema Balozi Shimbo. 
 Kuhusu elimu na mafunzo, Balozi Shimbo alisema programu hiyo ambayo imeanza muda mrefu, hadi kufikia Desemba 2011, ilikuwa imekwishawanufaisha wanafunzi wa Kitanzania 110 na wataalamu 1,020 ambao walipatiwa mafunzo chini ya udhamini wa Serikali ya China. 
 Kwa mwaka huu 2013, Balozi Shimbo alisema kuna wanafunzi zaidi ya 300 ambao wanasoma nchini humo. 
“Hivi sasa kuna wanafunzi 31 wanaodhamimiwa na serikali ya Tanzania, wanafunzi 249 wanaofadhiliwa na serikali ya China na wengine zaidi ya 100 wanaojidhamini wenyewe katika shahada za Uzamili na Uzamivu,” alisema. 
 Pia alisema Tanzania kwa kushirikiana na Dalian University of China, itanufaika na mradi wa kupandisha hadhi Chuo cha Usafiri wa Baharini (Dar es Salaam Maritime Institute) hadi kufikia ngazi ya Chuo Kikuu cha Kanda ya Afrika Mashariki. 
 Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekabidhi kwa kampuni ya Kichina ya China Rail Engineering Group ambayo inakifufua kiwanda cha viatu na ngozi cha Zanzibar na kukifanya kiwe kiwanda cha samani. Kiwanda hicho kilijengwa kwa msaada wa Serikali ya China katika miaka ya 70. 
 Hata hivyo, Balozi Shimbo alisema Tanzania inakabiliwa na changamoto kubwa ya kimahusiano na China ambapo vijana wa Kitanzania 175 wapo katika magereza ya nchini China kutokana na makosa ya uhalifu yakiwemo ya kusafirisha madawa ya kulevya. 
 “Kati ya hao, watatu uraia wao ni wa kutiliwa mashaka. Kati yao 48 wako China Bara, Hong Kong wapo 117 na Macau wapo 10. Kati ya hao 175, wanawake ni 34, ambapo 28 wako Hong Kong na sita wako China bara,” alisema. 
 Akizungumza na maafisa ubalozi pamoja na wajumbe wa msafara wake, Waziri Mkuu alisema tatizo la madawa ya kulevya linaharibu sifa ya Tanzania pamoja na mahusiano baina yake na nchi marafiki.
 “Tunahitaji kufanya kazi ya ziada ili kupambana na wasafirishaji wa dawa za kulevya. Watu 175 ni wengi kwa nchi moja lakini cha kusikitisha zaidi ni idadi kubwa ya wanawake waliokamatwa... wizara zinazohusika inabidi tukae na kuweka mkakati wa pamoja,” alisema. 
 Kuhusu misaada ya China kwa Tanzania, Waziri Mkuu alisema, kuna miradi ya kufa na kupona ambayo itabidi iwekewe uzito katika ziara yake hii na kuiainisha kuwa ni ujenzi wa reli ya kati, usambazaji wa umeme na ukuzaji wa utalii baina ya Tanzania na China hasa fursa ya kuanzisha usafiri wa ndege wa moja kwa moja baina ya Chiona na Tanzania. 
 Kesho (Alhamisi, Oktoba 17, 2013) Waziri Mkuu atakuwa na mazungumzo na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Mhe. Li Keqiang, Rais wa Benki ya Exim ya China, Rais wa Benki ya Maendeleo ya China na uongozi wa China Railway Jianchang Engineering. Pia atahudhuria dhifa ya Taifa itakayoandaliwa kwa heshima yake kesho jioni. 
 IMETOLEWA NA: OFISI YA WAZIRI MKUU, 
JUMATANO, OKTOBA 16, 2013
   Waziri Mkuu, Mizengo  Pinda na Mkewe Tunu wakimsikiliza Balozi wa Tanzania nchini China Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo  (kushoto) wakati aliposoma taarifa kwa Waziri Mkuu  ambaye leo Oktoba 16, 2013 aliwasili mjini Beijing kwa   ziara ya kikazi nchini China.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda  akiagana na Makamu wa Rais wa Kampuni ya China  National Machinery Industry Federation na Mwenyekiti wa Bod ya Kampuni ya TBEA, Bw, Zhang Xin  baada a mazungumzo yao mjini Beijing Oktoba 16, 2013. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 3 mpaka sasa

  1. kwani hiyo taarifa anayoisoma huyo muheshiwa balozi wetu haiwezi kutolewa kwa mh waziri mkuu pekee yake bila mkewe kuwa pembeni..hii ni shughuli za serekali sasa kwani huyu mke wa waziri mkuu naye ni mtumishi wa serekali jamani...tuache kushirikisha wake zetu kwenye shughuli za kiserekali..siri za serekali zinahitaji usiri mkubwa ndugu waTanzania wenzangu..kama umeenda na mkewe kwenye ziara hii basi muache mama sehemu mliyofikia, kafanye shughuli zilizokuleta hapa na halafu kama unataka kutalii na mkewe basi fanya hivyo nje ya mda na shughuli za seerekali..I am just saying..wadau wenzangu mnalionaje hili....tuweke mdahalo basi kwa hili...

    ReplyDelete
  2. Majina hayo wa ndugu zetu waliopo jela na rumande yanaweza kuchapishwa kama taarifa kwa umma?

    Nadhani njia ya kuyaweka majina hayo hadharani ktk vyombo vyote vya habari ni muhimu na kusaidia vijana kufanya maamuzi sahihi maana tarakimu za wafungwa na mahabusu 175 si kamilifu.

    ReplyDelete
  3. ndugu yangu naona hujui usemalo, fuatilia Mama Pinda ni Mtumishi wa ofisi gani tena kwa miaka Mingi na ndo maana walikutana wakaoana! Huyo mama ni mtu smart kuliko unavyidhani! Fanya utafiti kabla ya kuongea!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...