Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji RUBADA Bw. Aloyce Masanja, (kulia) akiteta
na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro,
Bi. Azimina Mbilinyi wakati wa semina ya kuwajengea uwezo watendaji wa ngazi
mbalimbali wa Halmashauri hiyo juu ya mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN) pamoja
na mpango wa uendelezaji wa kilimo katika ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA), Bw. Aloyce Masanja, (kushoto)
akizungumza na Meneja wa shamba la kampuni ya Kilombero Plantation Ltd (KPL), Bw.
Mare Dempsey (katikati) alipofanya ziara ya kuangalia maendeleo ya shamba hilo. Kulia ni Meneja
rasililimali watu wa kampuni hiyo, Bw. David Lukindo.
--------------------------------------------------------------
Zaidi ya wakazi wapatao 1000 wamefaidika
na ajira za kudumu na za muda kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na kampuni
ya kilimo ya Kilombero Plantation Ltd (KPL) katika kata ya Mngeta Wilaya ya
Kilombero Mkoani Morogoro.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA), Bw. Aloyce Masanja
wawekezaji hao mbali na kutoa ajira, wanatoa ruzuku ya Tshs milioni 50 kwa
mwaka kwa vijiji vitatu vya wilaya hiyo.
“Kuna watu wanasema uwekezaji hauna
faida katika nchi hii, mimi nataka kuwaambia waache kupotosha…leo hii
tunazungumzia ajira elfu moja katika eneo la Mngeta ambapo kiwanda hiki kipo,
bila uwekezaji ajira zingetoka wapi,” alihoji Masanja.
Alisema kwa sasa RUBADA inafanya
mikakati ya kuhakikisha inatenga maeneo mengine kwa ajili ya uwekezaji mkubwa
ili vijana na watanzania wengine waweze kufaidika na uwekezaji huo.
“Kinachofanyika sasa ni kutenga
maeneo mengi iwezekanavyo, tayari kuna eneo la Lingamila katika wilaya ya
kilombero, ardhi ile inafaa kwa kilimo cha miwa hivyo ni jukumu la RUBADA kusimamia
zoezi hilo kwa ajili ya kuleta muwekezaji ili aanze kazi,” alisisitiza.
Akizungumzia uwekezaji mkubwa uliopo katika shamba la Mngeta
Wilayani Kilombero Bw. Masanja alisema mbali na ajira zilizopo pia wapo
wakulima wadogowadogo katika eneo hilo ambao wanashirikiana kwa karibu na muwekezaji
huyo kutoka nchini Uingereza.
“Kuna wakulima wadogo ambao
wanazalisha mpunga katika eneo la Mngeta na soko lao kubwa ni katika kiwanda
hicho kutokana na ukaribu na mahusiano mazuri yaliyopo kati ya wakulima hap na
muwekezaji huyo,” aliongeza Mkurugenzi huyo.
Bw. Masanja alielezea shughuli
nyingine za kijamii ambazo zinatekelezwa na muwekezaji kuwa pamoja na shule
moja pamoja na hospitali kwa ajili ya wananchi wa eneo la Mngeta na vijiji vya
jirani.
Alisema shamba hilo ambalo lina ukubwa
wa hekta 5800 ni mkombozi kwa wakazi wa eneo hilo ambao kwa muda mrefu wamekuwa
wakitegemea kilimo cha mkono kuzalisha mpunga lakini kwa sasa wamepata faida
kutokana na zana bora ambazo wanazipata kupitia muwekezaji huyo.
Alifafanua kwamba hivi sasa kuna
mashine za kisasa kwa ajili ya umwagiliaji, matreka pamoja na mbolea ya
kutosha, hivyo ni jukumu la wananchi kuwaunga mkono wawekezaji hao ili pia nao waendelee
kufaidika.
“Sioni sababu ya kuwachukia
wawekezaji, kama mtu anafanya kazi na inaonekana kwanini umchukie…wawekezaji
ambao ni wababaishaji, huwa tunawashughulikia na tunawapokonya na kuwapa watu
wanaoweza kufanya kazi,” alisema Masanja.
Aliwataka watendaji wa kata, vijiji
pamoja na vitongoji mbalimbali vilivyopo katika wilaya ya kilombero kutoa
ushirikiano kwa RUBADA pamoja na wawekezaji wanaokuja kuwekeza katika wilaya
hiyo ili uchumi wa eneo hilo uweze kukua na kuondoa umasikini uliopo.
“Viongozi waone kuwa hii ni fursa
muhimu kwao, hakuna sababu ya kulumbana,” alisisitiza Mkurugenzi huyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...