SHIRIKA la Ndege la Precision Air limejipanga kujiimarisha zaidi katika miaka michache ijayo baada ya utekelezaji wa mpango mkakati uliopitishwa na bodi ya shirika hilo wa miaka mitano, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Precision Air Michael Shirima amesema.

Akizungumza wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka jijini Dar es Salaam jana, Shirima alisema matokeo ya shirika ya nusu mwaka kwa kipindi cha Aprili mpaka Septemba kimeonyesha matarajio chanya ya kuwa na matokeo mazuri yatokanayo na mkakati huo.

“Kutokana na changamoto hizi, Precision Air ilipata hasara ya shilingi bilioni 30 kwa kipindi cha mwaka kinachoishia Machi 31, 2013. Kabla ya hasara hii, shiriki liliweza kupata kadirio la faida ya asilimia 4 katika kipindi cha miaka saba kuanzia mwaka 2006,” alisema Shirima. Alisema wakati wa kipindi hicho, mali za shirika ziliongezeka zaidi ya mara kumi kutoka shilingi bilioni 23 mwaka 2006 mpaka bilioni 276 ilipofika Machi 31, 2013.

“Ongezeko la mali za shirika lilienda pamoja na kukua kwa uwezo wa shirika kubeba abiria wengi zaidi. Kutoka kusafirisha abiria 340,000 kwa mwaka 2006 mpaka abiria 896,000 kwa mwaka 2013 siyo mafanikio madogo. Kufikia jumla ya abiria milioni 5 kwa kipindi hiki, wote wakifika katika maeneo yao “kwa amani” ni suala la kujivunia.

“Kwa bahati mbaya, kuongezeka kwa idadi ya abiria haukuliwezesha shirika kuongeza faida kwa sababu ambazo zimeelezwa hapa chini. Hasara iliyopatikana mwaka 2013 imesababisha kushuka kwa faida katika miaka nane iliyopita mpaka asilimia moja,” aliongeza. Shirima alisema kuwa biashara zinazokuwa na faida ndogo kiasi hicho utokana na sababu zitokazo nje zinazoathiri aidha mapato ya shirika au gharama za uendeshaji.

“Hali hii imekuwa mbaya zaidi kama kuna kutokuwiana kwa mapato na matumizi (currency mis-match). Kwa mfano sehemu kubwa ya mapato ya Precision Air ni katika shilingi wakati sehemu kubwa ya matumizi ni fedha za kigeni (ununuzi wa ndege, vipuri mafuta na mategengenezo makubwa), hivyo kuwa na uwezekano wa hasara inayotokana kupungua kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania ikilinganishwa na dola ya kimerikani,” alisema.

Alisema kuwa uongozi wa shirika ulitambua vikwazo na changamoto hizo mapema na kuchukua hatua za awali kukabiliana nazo ili kuinusuru kampuni na kuongeza kuwa njia mojawapo kubwa ya jitihada hizo ni kutafuta mtaji wa muda mrefu kupitia uuzaji wa Hisa kwa Umma kwa Mara ya Kwanza na hatimaye kuzioredhesha hisa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) mwaka 2011.

“Hatukuweza kufanikiwa katika kuongeza kiasi tulichokihitaji na upungufu huu ukaleta matatizo mengi. Kutopatikana kwa mtaji uliotarajiwa kuliliweka shirika mahali pabaya kwani ndege zilikwisha agizwa na kulipiwa fedha za awali na kiasi cha asilimia 15 cha bei za ndege hizo ililipwa”

“Haingekuwa busara kujitoa katika kununua ndege kwani fedha za amana zingepotea na uimarishaji wa shirika ungeadhiriaka kwa kukosa ukuaji. Na matokeo yake ni shirika lilipata shinikizo la mtiririko wa fedha (cash flow) na upatikanaji wa faida. Pamoja na hayo thamani ya hisa katika soko (DSE) haikuporomoka kwa kuwa zimesimamia kwenye Tshs 475 kwa kila hisa,” alisema Shirima.

Shirima alisema kuwa ni kweli sababu zilizo nje ya kampuni zimechangia kuwa na matokeo hafifu ya biashara. Ila ni hekima kukubali kuwa kulikuwa pia na sababu za ndani ya kampuni ambazo zimechangia kwa kiasi fulani kutufikisha hapa.

“Baada ya uchambuzi wa kina wa utendaji wa kampuni, Bodi imebaini maeneo yafuatayo kuwa inawezekana ndicho kiini cha kudorora kwa ufanisi. Maeneo hayo ni mtandao wa safari usio na ufanisi, ndege zenye gharama kubwa ya uendeshaji, tija hafifu, kukosekana udhibiti wa matumizi na udhaifu wa kufuatilia vyanzo mbadala vya mapato.

“Tumepata fundisho na hivyo Bodi imefanya mabadiliko makubwa ya kiuongozi ikizingatiwa kuwa haya matatizo yameonesha fursa ya kurudisha biashara katika mwelekeo wa faida siku zijazo,” aliongeza. Aidha, alisisitiza kuwa hivi sasa shirika hilo liko kwenye mazungumzo ya kupata mtaji wa muda mrefu ili kukidhi utekelezaji wa majukumu yaliyoahirishwa miaka miwili iliyopita.

Shirima alibainisha kuwa uwiano wa mitandao ya safari zilizopo utafanyika kwa kuangalia hali iliyopo sasa yakibiashara na utumiaji wa ‘sub-optimal capacity’ ambao ulipungua kwa asilimia 65 katika kipindi miaka nane iliyopita. “Hii itajumuisha uondoaji wa ndege zenye gharama kubwa na kuleta ndege kubwa aina ya Jet miaka mitatu kuanzia sasa. Ndege hizi zinauwezo mkubwa wa kubeba abiria na kuongeza mapato kutokana na mizigo,” alisema Shirima.

Alisema fursa za kuongeza mapato zitajikita kwenye vyanzo vikuu, ambavyo ni: nauli – kuboresha tija na tozo ya ziada kwa ongezeko la bei ya mafuta; mizigo ya ziada – udhibiti ili kuongeza makusanyo; mizigo ya jumla – kuongeza viwango vya tozo; na mapato mbadala – matengenezo ya ndege za kampuni nyingine na matangazo.

Njia nyingine zitakazotumika ni kupitia upya muundo wa biashara kwa ujumla na kufikiria upya utayari wake katika mazingira ambayo ushindani ni thabiti. Muhimu zaidi ni kwamba kuongeza thamani ya biashara kwa wamiliki wa kampuni kutahusisha matumizi mahususi ya rasilimali zilizopo katika kuongeza faida, kuongeza ufanisi wa kiutendaji, na kupunguza gharama ya mtaji. Hata hivyo, udhibiti wa gharama kamwe usifikie hatua ya kudhoofisha usalama wa vyombo vya usafiri.

Alisema mafanikio ya utekelezaji wa yaliyoainishwa hapo juu, pamoja na upatikanaji wa mtaji utaiwezesha kampuni kupata faida na hivyo kuwafaidisha wanahisa waliovumilia katika kipindi hiki cha dhoruba na mitetemo ya kibiashara.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Jitahidini Precision kibiashara msonge mbele ushindani upo boresheni huduma wasafiri mtawapata.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...