Washtakiwa wawili kati ya
wanne wa kesi ya mauaji dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Wilaya ya Rungwe, John Mwankenja, wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya
kupatikana na hatia katika Mahakama kuu kanda ya Mbeya.
Hukumu hiyo ilitolewa katika Mahakama kuu kanda ya Mbeya iliyokuwa
ikiendesha vikao vyake katika Mahakama ya Wilaya ya Rungwe chini ya Jaji
Samweli Karua, baada ya kuahirishwa kutolewa kwa hukumu hiyo kwa zaidi ya mara
tatu na kuzua hali ya sintofahamu kwa ndugu wa washtakiwa na wafuatiliaji wa
kesi hiyo.
Awali kabla ya kusoma kwa hukumu hiyo Mwendesha mashtaka wa Serikali.,
Archiles Mulisa, aliwataja watuhumiwa wote wanne kuwa ni Hakimu Mwakalinga,
Daudi Mwasipasa, Obote Mwanyingili na Kelvin Myovela wanaokabiliwa na tuhuma za
kumuua kwa maksudi aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe John
Mwankenja.
Alisema watuhumiwa hao wenye kesi namba 131/2012 walitenda kosa hilo Mei
19, 2011 katika kijiji cha Mpandapanda, Kata ya Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoani
Mbeya.
Mulisa aliyekuwa akisaidiwa na Wakili wa Serikali Lugano Mwakilasa kwa
upande wa mashtaka huku Watuhumiwa wakitetewa na Mawakili wawili ambao ni
Victor Mkumbe na Simon Mwakolo.
Mulisa alidai mahakamani hapo kuwa kesi inayowakabili watuhumiwa
hao walilitenda Mei 19,2011 kwa kumuua kwa maksudi John Mwankenja kinyume na
kifungu cha 196 sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Akisoma hukumu hiyo Jaji Karua ambaye alianza majira ya saa 14:37 mchana
na kukamilisha saa 15:37 alisema katika kesi hiyo upande wa mashtaka na utetezi
haubishaniwi kuhusu kifo cha marehemu.
Aliongeza kuwa pande hizo mbili pia hazibishaniwi kuhusu ripoti za
kitaalamu na dhamira za mauaji hayo bali kinachobishaniwa ni uhusika wa
watuhumiwa hao dhidi ya mauaji hayo.
Alisema katika kutetea hoja zao upande wa mashtaka ulileta mashahidi 11
ambao wote kwa pamoja wakiongozwa na shahidi namba moja waliwatuhumu
washtakiwa kuhusika na tukio hilo.
Shahidi huyo namba moja Weston Jacob(17) mkazi wa Kiwira Mwanafunzi
kidato cha Tatu katika shule ya Sekondari Kipoke ambaye pia ni Mjomba wa
marehemu ambaye aliiambia mahakama kuwa siku ya tukio akiwa nyumbani akijisomea
majira ya 2: 30 usiku ambapo marehemu alifika nyumbani na kupiga honi ya gari
akitaka afunguliwe mlango.
Mbali na ushahidi huo Jaji Karua alisema pamoja na ushauri wa wazee wa
baraza la mahakama ambao pia wanawatuhumu washtakiwa hao kuhusika na tukio hilo
nae anakubaliana nao lakini siyo kwa watuhumiwa wote.
Kutokana na ushahidi huo alisema Mshtakiwa namba moja na namba mbili
ambao ni Hakimu Mwakalinga na Daudi Mwasipasa wanatiwa hatiani kuhusika moja
kwa moja na mauaji kutokana na ukiri wao kwa mlinzi wa amani, Mchukua maelezo
na vipimo vya vinasaba.
Alisema Mshtakiwa namba tatu Obote Mwanyingili yeye anatiwa hatiani
kutokana na kosa la kumhifadhi mtuhumiwa namba moja baada ya kutoka kufanya
mauaji hivyo yeye hausiki moja kwa moja na kosa hilo.
Jaji karua alisema kwa upande wa mshtakiwa namba nne Kelvin Myovela
anatiwa hatiani kutokana na kuhifadhi silaha iliyotumika nkatika mauaji hayo
ingawa hakusika na kitendo hicho moja kwa moja.
Aliongeza kuwa kutokana na kifungu cha sheria cha mwenendo wa makosa ya
jinai kifungu namba 300 na 217 washtakiwa namba tatu na namba nne wanatiwa
hatiani na mahakama.
Mwendesha mashtaka wa Serikali Archiles Mulisa, aliiambia mahakama hiyo
kwamba itoe adhabu kali kutokana na kitendo alichofanyiwa marehemu na iwe
fundisho kwa watu wengine.
Kwa upande wa utetezi ambao siku ya hukumu uliwakilishwa na Wakili
Merick Luvinga alisema mahakama iwanee huruma washtakiwa kwa kuwa wote umri wao
ni mdogo wanaweza kujifunza na kurudi kuungana na jamii pia ni kosa lao la
kwanza hivyo wasipewe adhabu kali.
Kutokana na utetezi huo, Jaji Karua alisema kutokana na ushahidi
uliotolewa mahakamani hapo kuthibitisha kuhusika pasipo shaka kwa washtakiwa
namba moja na namba mbili hivyo adhabu yao ni kunyongwa hadi kufa.
Aliongeza kuwa Mshtakiwa namba tatu Obote Mwanyingili anayehusika
kumhifadhi mtuhumiwa wa kwanza ataenda jela miaka saba kwa kosa hilo sambamba
na mshtakiwa namba nne Kelvin Myovela aliyehifadhi silaha iliyotumika
kwenye mauaji.
Alisema kutokana kosa hilo mtuhumiwa huyo atatumikia kifungo jela miaka
saba ingawa pia tayari alikuwa amehukumiwa kifungo jela cha miaka 20 kwa kosa
la kukutwa na silaha kinyume cha sheria.
Wakati huohuo
MAHAKAMA kuu kanda ya Mbeya imemhukumu kwenda jela miaka 35 mtuhumiwa wa
mauaji dhidi ya watoto huku mwingine akiachiwa huru baada ya kukutwa bila
hatia.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Jaji wa Mahakama kuu kanda ya Mbeya Samweli
Karua mbele ya mwendesha mashtaka wa serikali Archiles Mulisa katika vikao
vilivyofanyika katika Mahakama ya wilaya ya Rungwe.
Awali mwendesha mashtaka wa serikali Archiles Mulisa aliiambia mahakama
kuwa washtakiwa Baraka Mwandibwa na Zuberi Lwila walifikishwa mahakamani hapo
wa kosa la kumlawiti na kumuua mtoto Esta James(5) Novemba 21, 2010.
Alisema kosa hilo ni kinyume cha sheria kifungu cha 196 (16)
kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2002, ambalo walilifanya katika kijiji cha
Bulyaga Wilayani Rungwe baada ya kumteka mtoto huyo.
Akisoma hukumu hiyo Jaji Karua alisema Mshtakiwa namba moja anatiwa
hatiani kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo ambao ulitoka kwa
shahidi namba moja ambaye ni mtoto aliyejulikana kwa jina la Marietha.
Alisema mtoto huyo ambaye alisema siku ya tukio alikuwa akicheza na
marehemu ambapo mtuhumiwa alifika na kumpa pipi aina ya Ivory marehemu kisha
kuondoka naye ambapo shahidi huyo aliwerza kumtambua mtuhumiwa katika gwaride
la utambuzi.
Mbali na hilo alisema ushahidi mwingine ni ushaidi wa Vinasaba ambao
unawahusisha moja kwa moja watuhumiwa wote wawili ikiwa ni pamoja na ushaidi wa
kimazingira unaomhusisha mtuhumiwa wa kwanza.
Alisema kutokana na ushahidi huo Mtuhumiwa wa kwanza anahusika moja kwa
moja na mahakama inamtia hatiani ingwa kwa mujibu wa ushahidi hakuua kwa
makusudi kutokana na kutokuwa na vifaa vya mauaji kama visu panga na silaha
zingine.
Alisema katika mwili wa marehemu ulikutwa ukiwa unadamu na mbegu za
kiume sehemu zake za siri na hakuwa amejeruhiwa nsehemu yoyote, hivyo mahakama
iliona mtuhumiwa hakuua kwa kukusudia bali ilikuwa ni bahati mbaya.
Hata hivyo upande wa Mshtaka uliomba mahakama itoe adhabu kubwa na kali
dhidi ya washtakiwa kutokana na mazingira aliyofanyiwa mtoto huyo ili iwe
fundisho kwa wanaume wengine wenye tabia za kuwalaghai watoto wadogo.
Akitoa hukumu hiyo Jaji karua alisema anakubaliana na ushauri wa upande
wa mashtaka kwamba tukio hilo ni kubwa na mstakiwa wa kwanza Baraka Mwandibwa
ataenda jela kwa miaka 35 huku mshtakiwa wa pili Zuberi Lwila akiachiwa huru
baada ya kutokuwa na ushahidi wa kuhusika katika tukio hilo.
|
Nilitaka kuona ajabu shitaka la kubaka mpaka kuua likawa na hukumu ya kifo. Wanaume wanajua siri ya utamu wa kubaka ndio maana hawawezi kutoa adhabu kali
ReplyDelete