JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI



       

     
MKUTANO KUHUSU ADHABU MBADALA YA KIFUNGO GEREZANI KUFUNGULIWA KESHO TAREHE 07 NOVEMBA, 2013

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman anatarajiwa kufungua mkutano kuhusu masuala ya adhabu mbadala wa kifungo gerezani, utakaoanza kesho (6 Novemba, 2013)  jijini Dar es Salaam.

Mkutano huo umeandaliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kupitia Idara ya Huduma kwa Jamii, kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa linalojishughulisha na Maboresho ya Sheria za Adhabu la Penal Reform International, na utafanyika katika Hoteli ya Holiday Inn, Dar es Salaam.

Lengo la Mkutano huo ni kujadili masuala mbalimbali kuhusu kuboresha adhabu mbadala wa kifungo gerezani na pia kupitia maazimio kuhusu  matumizi ya adhabu mbadala yaliyofikiwa katika Mkutano kama huu uliofanyika nchini Uganda na kuzindua Mtandao unaohusu Adhabu Mbadala wa Kifungo kwa nchi za Afrika, unaojulikana kama ‘African Alternative to Imprisonnment Network’.

Mkutano huu wa kesho utakaoendelea hadi keshokutwa, utawashirikisha Wakuu wa Vyombo vinavyosimamia adhabu mbadala wa kifungo kutoka nchi 10 za Afrika.  Nchi hizo ni  Ethiopia, Kenya, Malawi, Rwanda, Afrika Kusini, Sudani ya Kusini, Uganda, Zambia, Zimbabwe na wenyeji Tanzania.

Mkutano huu ambao unajulikana kama Mkutano wa Uzinduzi wa Mtandao unaohusu Adhabu Mbadala wa Kifungo kwa nchi za Afrika (Africa Alternatives to Imprisonment Network Inaugural Meeting) utafuatiwa na Mkutano mwingine wa Adhabu Mbadala kwa nchi za Afrika Mashariki (East Africa Alternantives to Imprisonment Conference) utaofanyika tarehe 7 hadi 8 Novemba, 2013.

Mkutano huo, mahsusi kwa nchi za Afrika Mashariki, utawashirikisha wawakilishi wa Idara zinazoshughulika na Adhabu Mbadala wa Kifungo (Probation and  Community Service) na Mashirika ya Kijamii kutoka nchi za Kenya, Uganda na wenyeji Tanzania. Wafadhili na Mashirika mbalimbali ya Kimataifa na washiriki wa Mkutano wa Afrika pia wamealikwa kuhudhuria mkutano huo.

Lengo la mkutano huo wa nchi za Afrika Mashariki ni kubadilishana uzoefu katika kusimamia utekelezaji wa Adhabu Mbadala wa Kifungo na kuweka mikakati ya kuboresha utekelezaji wake kwa nchi za Afrika Mashariki.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
05 NOVEMBA, 2013

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...