BENDI ya muziki wa dansi ya Mashujaa Musica 'Wazee wa Kibega'
inatarajia kupamba uzinduzi wa albamu ya 'Chuki ya Nini' ya bendi ya
FM Academia utakaofanyika Desemba 21 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Hayo yalisemwa jana Rais wa bendi hiyo, Nyoshi El-Saadat alipokuwa
akizungumza na waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari kuhusu
maandalizi ya uzinduzi huo aliodai kuwa utakuwa wa kishindo.
"Hii ni albamu yetu ya kumi ambayo imeandaliwa kwa ubora wa kimataifa
na sasa iko tayari kuzinduliwa Desemba 21 tukisindikizwa na bendi ya
Mashujaa Musica," alisema Nyoshi.
Nyoshi alitaja nyimbo za albamu hiyo kuwa ni 'Fataki', 'Otilia', 'Ndoa
ya Kisasa', 'Neema', 'Dai Chako Ulaumiwe', 'Maisha', 'Madudu',
'Miraessa' na 'Intro' ambazo zote zimeshaingizwa kwenye video.
Aliongeza kusema kuwa katika uzinduzi huo watawakumbuka pia kwa
kuwaombea watu wawili maarufu waliofariki dunia ambao ni Rais wa
zamani wa Afrika Kusini mzee Nelson Mandela na mwanamuziki mkongwe wa
Kongo, Tabu Ley.
Bendi ya FM Academia ilizindua albamu ya kwanza ya 'Hadija' mwaka 1998
kisha ikafuatia ya pili iitwayo 'Atomic' iliyozinduliwa mwaka 1999 na
baadaye mwaka uliofuata wa 2000 bendi hiyo ilizindua albamu ya tatu
iliyopewa jina la 'Prison'.
'Wazee wa Ngwasuma' hawakuishia hapo, mwaka 2001 walizindua albamu ya
nne iitwayo Freedom na kufuatiwa na ya tano ya 'Mpambe Nuksi'
iliyozinduliwa mwaka 2001 na kisha ikafuata ya sita iitwayo 'Dotnata'
mwaka 2003 kabla ya 'Dunia Kigeugeu' iliyozinduliwa mwaka 2006.
Baada ya hapo bendi hiyo ilikaa kidogo hadi mwaka 2010 ilipozindua
albamu mbili kwa mpigo ambazo ni 'Vuta Nikuvute' na 'Heshima kwa
Wanawake' na sasa mwaka huu wa 2013 unaumalizia kwa kuzindua albamu
ya 'Chuki ya Nini'.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...