Na Inspekta Lucas Mboje, Arusha
Kikao cha 24 cha Bodi ya Taifa ya Parole kimeanza leo Desemba 19, 2013 chini ya Uenyekiti wa Mhe. Jaji Mstaafu Eusebia Munuo katika Ukumbi wa Hoteli ya Charity iliyopo Jijini Arusha.
Kikao hiki cha siku mbili kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Sekretarieti ya Bodi ya Taifa ya Parole kitajadili Wafungwa waliopendekezwa kuachiliwa kwa Parole.
Aidha, Wajumbe watapitia mapendekezo ya Maboresho ya Sheria ya Bodi za Parole(Cape 400 RE 2002) pamoja na kuchambua maoni yanayohusu taarifa ya Mhe. Jaji Kiongozi ya kusamehe theluthi moja (1/3 ) ya Kifungo kwa washitakiwa watakaokiri Mahakamani.
Utaratibu huu wa Parole hapa nchini ni moja wapo ya adhabu mbadala wa kifungo ambao ni matokeo ya mfumo uliobuniwa na jamii katika nchi nyingi kwa miaka ya hivi karibuni ikiwa ni njia moja wapo ya kupunguza ongezeko la wafungwa ndani ya Magereza hivyo kuipunguzia Serikali na Wananchi ambao ndio walipa Kodi, Mzigo mkubwa wa kuwahudumia Wafungwa wawapo ndani ya Magereza.
Lengo Kuu la Sheria ya Bodi ya Parole ya Mwaka 1994 ambayo ilifanyiwa marekebisho Mwaka 2002 ni kuweka masharti Maalum kuhusu utaratibu wa Urekebishaji wa Wahalifu nje ya Magereza baada ya Mfungwa kutumikia sehemu ya kifungo chake na kuonesha mwelekeo wa kurekebika unaokubalika kwa mujibu wa Sheria hii na Kanuni zake.
Kumekuwepo changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa Sheria hii ikiwa ni pamoja na ufinyu
au wigo mdogo wa Kisheria uliowekwa na Sheria yenyewe. Kutokana na wigo mdogo uliopo wa Kisheria takwimu zilizopo zinaonesha kuwa wafungwa wengi hawawezi kujadiliwa kwa kuwa hawana sifa zinazotakiwa kwa mujibu wa Sheria iliyopo.
Kwa mujibu wa Sheria hiyo Mfungwa anayestahili Parole ni yule anayetumikia kifungo cha miaka minne(4) na kuendelea na awe ametumikia theluthi moja (1/3) ya kifungo chake na kuonesha mwelekeo wa kurekebika unaokubalika kwa mujibu wa Sheria hii na Kanuni zake.
Hiki ni Kikao cha Tatu kufanyika chini ya Uenyekiti wa Mhe. Jaji Mstaafu Eusebia Munuo tangu ateuliwe na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole Aprili, 2013.
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Mhe. Jaji Mstaafu Eusebia Munuo(kushoto) akiongoza Kikao cha kujadili wafungwa waliopendekezwa kuachiliwa kwa Parole(kulia) ni Katibu wa Bodi ya Taifa ya Parole ambaye pia ni Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja. Kikao hiki kimeanza leo Disembark 19 katika Ukumbi wa Hoteli ya Charity, Jijini Arusha.
Baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Taifa ya Parole wakipitia makabrasha yenye mapendekezo ya Wafungwa waliopendekezwa kuachiliwa kwa msamaha wa Parole(wa kwanza kulia) ni Mjumbe wa Bodi ya Taifa ya Parole, Bw. Francis Stolla akipitia makabrasha hayo kama anavyoonekana katika picha.
Katibu wa Bodi ya Taifa ya Parole ambaye pia ni Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja(suti nyeusi) akiteta jambo na Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Mhe. Jaji Mstaafu Eusebia Munuo mara baada ya kuahirisha Kikao hicho ambacho kitaendelea kesho Desemba 20, 2013 (kushoto) ni Mjumbe wa Bodi hiyo Dkt. Joseph Chuwa
Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Mhe. Jaji Mstaafu Eusebia Munuo(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Taifa ya Parole(walioketi) na Sekretarieti ya Bodi ya Taifa ya Parole(waliosimama). Wa tatu kutoka kulia ni Katibu wa Bodi ya Taifa ya Parole ambaye pia ni Kamishna Jenerali wa Magereza Nchini, John Casmir Minja.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...