Mhe. Kairuki
Naibu Waziri wa Sheria na Katiba Mhe. Angela Jasmine Kairuki (37) ametajwa katika  jarida la kimataifa la Forbes kuwa ni mmoja wanawake vijana 20 wenye nguvu barani Afrika mwaka huu. 

 Katika toleo lake la hivi karibuni chini ya kichwa cha habari ‘The 20 Young Power Women in Africa 2013’, jarida la Forbes linamuorodhesha Mhe Kairuki sambamba na wanawake wengine 19 kama vijana wa kike wenye nguvu kwa nafasi zao kikazi na kibiashara. 

Kutajwa kwa Mhe Kairuki katika orodha hiyo kumezua msisimko katika mawasiliano ya mtandao wa 'twitter' ambapo Watanzania wengi wamekuwa wakielezea furaha na fahari zao kwa kuona Mtanzania mwenzao, tena mwanamke kijana, anatambulika kimataifa kwa utendaji wake.

Mhe. Angela Kairuki akitembelea Jeshi la Magereza
 katika mojawapo ya shughuli zake za kikazi
 Wanawake wengine waliotajwa na jarida hilo ni Mimi Alemayehou (Ethiopia) Makamu wa RAis Mtendaji wa Overseas Private Investment Corporation (OPIC),   Vera Songwe(Cameroon) Mkurugenzi Mkazi World Bank Senegal, na Tara Fela-Durotoye (Nigeria) Mwanzilishi wa House Of Tara.
Wengine ni  Rapelang Rabana (Afrika Kusini) Mjasiriamali,   Claire Akamanzi (Rwanda) Afisa Mtendaji Mkuu wa Rwanda Development Board,   Valentina da Luz Guebuza (Msumbiji) Mwekezaji,  Hadeel Ibrahim (Sudan) wa Mo Ibrahim Foundation,  Alengot Oromait (Uganda) Mbunge, na   Monica Musonda, (Zambia) Afisa Mtendaji Mkuu na MWanzilishi wa kampuni ya Java Foods.
Wengine ni NoViolet Bulawayo (Zimbabwe) Mtunzi wa vitabu, Minoush Abdel-Meguid (Misri) Mwekezaji, mjasiriamali na mwendesha benki,  Ola Orekunrin (Nigeria) Daktari na Mwanzilishi wa The Flying Doctors,  Sibongile Sambo (Afrika Kusini) Afisa Mtendaji Mkuu na Mwanzilishi wa SRS Aviation,  Lupita Nyong’o (Kenya) Mwigizaji na mtengeneza filamu,    Amini Kajunju (Congo DRC) Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Africa-America Institute na  Folake Folarin-Coker (Nigeria) Mbunifu wa mitindo.

Wengine katika orodha hiyoni  Lindiwe Mazibuko (Afrika Kusini) Mwanasia na Kiongozi wa chama cha Democratic Alliance (DA) bungeni,   Minoush Abdel-Meguid (Misri) Mwekezaji, Mjasiriamali na mwendesha benki,  Sibongile Sambo (Afrika Kusini),  Wangechi Mutu, (Kenya) Msanii na mchongaji.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 12 mpaka sasa

  1. Hongera mama Angela Kairuki kwa kutambuliwa chapa kazi uwe role model wa vijana kutafuta nafasi za uongozi.

    ReplyDelete
  2. Mimi nitarudi kutoa hongera baada ya kupata katiba mpya tunayoitaka

    ReplyDelete
  3. Wadau, mimi sina nongwa na pongezi alizopewa dada yangu Dr. Kariuki hapo juu .... ila ukiangalia kwa jicho la "English Grammer" maneno ambayo yametafsiriwa na kuleta hicho kichwa hapo juu ni haya hapa: "The 20 Young Power Women In Africa 2013" ukipiga jicho hapo utaona kuwa maneno hayo ya "ki-ingereza" hayanatafsiri kama kichwa kinavyosomeka hapo juu (kwa-kiswahili)....inaonekana mwandishi ameweka mkazo kwenye neno "power" kama nguvu wakati hapo "kwa tafsiri ya chini ya mwembe" inapotosha maana halisi iliyokusudiwa ... kwahiyo utaona hayo maneno "young power women" yangepaswa yatafsiriwe kama "viongozi vijana wanawake" na siyo "wanawake vijana wenye nguvu" .... so mimi naona kuna lugha gongana hapo.....

    ReplyDelete
  4. Tehe tehe tehe...mdau wa lugha gongana hujatatua tatizo sababu wewe pia ni sehemu ya tatizo, hasa kujifanya kujua wakati jibu huna. Si afazali Ankoli kajaribu tofauti ya wewe ambaye unaleta bla bla tu hapa. Hebu tuondokee kule...Wivu tu umekujaa. Hapo ulikuwa unatafuta cha kumchokonyoa Mhe Angela umenoa, unageukia vichwa vya habari. Hilooooo....!

    MDAU DAR

    ReplyDelete
  5. Lanini si nime-declare kuwa Dr. Kariuki ni dadangu sasa wivu utoke wapi, Mdau Dar?

    Hoja binafsi: Nadhani mimi na "Mdau Dar" itabidi turudi shule/darasani....na sinauhakika kama mdau dar kabla hajapinga hoja yangu alichukua muda kufuatilia chanzo cha habari hiyo iliyotolewa kwa lugha ya "ki-nyamwezi" ukisoma huko Mdau Dar utaelewa nini hoja yangu....

    Ila Mdau Dar....ukizidi kukomaa sana, basi ntaacha mambo yaende "ki-bongobongo" ntaondoa hoja na pia ntafanya hivyo kwa heshima ya dadangu Dr. Kariuki....nisije nikamwekea kiwingu....(Peace & Love)

    ReplyDelete

  6. Unajidai kujua Kiingereza!!!!!!!!!!!!!!!!!!

    "...ila ukiangalia kwa jicho la 'English Grammer'" ...

    "Grammer" ndio mdudu gaani?


    Katika uandishi wa leo hii, inafaa sana kuangalia kitu kiitwacho, "verification" na mwandishi ametuonyesha wapi pa kubofya!

    ReplyDelete
  7. Hapa nakubali umenishinda, Mdau Dar....wewe leo bingwa....Hongera sana! "English Grammer"...hakuna kitu kama hicho kabisaaaa ni "English Grammar" ... ila umepata ushindi mwembamba na kwa mechi ya leo "e" imenigharimu badala ya "a" - Ahsante!

    Lakini kwenye hoja ya msingi nimekupiga bao....inaonekana ulipongeza bila kwenda kwenye "content" ya hicho kichwa cha somo hapo juu; pongezi siyo mbaya ila tuelewage kiini cha hizo habari zenyewe kabla ya kupongeza;

    Hao jamaa walifanya survey na kubaini kulingana na age profile (yaani 45 & below) kuwa Dr. Kariuki ni miongoni mwa wanasiasa 20 wakike walio vijana zaidi katika Afrika....hapa hakuna hoja kuwa yeye ni miongoni mwa wanasiasa vijana 20 wakike wenye nguvu katika Afrika - Hatahivyo nimependa umakini wako uliponishinda kwa goli "a"

    ReplyDelete
  8. MDAU DAR tena hapa.
    Ama hakika watu wangekuwa na kubishana bila kugombana kama wewe hapo juu, hali ya hewa isingekuwa inachafuliwa mara kwa mara. Na katika kuendeleza hilo bado hoja yako ya Mhe Kairuki kuwa ama kutokuwa mwanamke kijana mwenye nguvu hujaipiku. Na neno wanasiasa umeweka wewe, halikuwepo na halipo. LAbda kukusaidia tukubaliani kuwa katika kiswahili hakuna tafsiri ya 'power' (ila kama utamaanisha zao la nishati, yaani umeme), kwani nguvu imetafsiriwa VERBATIM, na imetumika kama verb na sio noun. Tukubaliane tu kuwa Kiswahili chetu bado ni 'maskini' na hakina utajiri wa maneno.


    ReplyDelete
  9. Ahsante kwakuwa umeliona hilo, kimsingi watu wanaweza kutofautiana kwa hoja na bado wakaelewana kwamaana ikiwa ni lazima sana basi wanaweza kufika mahali na "kukubali kutokukubaliana" - ila napata kigugumizi kusema kuwa wewe na mimi hapo ndipo tulipofika!

    Kwa upande mwingine ni kweli kuwa lugha yetu ya kiswahili inamapungufu katika matumizi fulani ya maneno, kama ulivyofafanua...ingawa hivyo, hii haiifanyi lugha hii isiwe adhimu...ni lugha iliyotukuka inayobeba sehemu kubwa ya utamaduni wetu waki-TZ na hivyo ni lazima tuienzi kwa gharama zozote zile.

    Kwa mara nyingine nakushukuru sana kwa muda na uvumilivu wako, niseme tu kuwa mimi nimenufaika sana na mjadala huu, na pia nimshukuru sana "Ankoli" kutuvumulia na kurusha hewani mawazo yetu hasa kwenye hizo "lugha gongana" napenda pia mawazo ya wadau wengine mbalimbali na pia nazidi kujifunza kuzivumilia hoja zilizo kinyume na mtazamo wangu - ni utamaduni mgumu, maana wakati mwingine unapokubali ni kama unakuwa umeshindwa hivi....lakini hizo ndizo gharama za hekima ambazo wachache wanaweza kuzilipa (mimi najitahidi kuwa mmoja wao)_Tutawasiliana zaidi katika "Blogi hii ya Jamii"

    ReplyDelete
  10. Yaani umenigusa hadi nalengwa na machozi. nilitaka kulala lakini nilingoja nione utajibu nini. Kumbe si kweli kwamba Watanzania wote wameoza, bado wapo wenye utu kama wewe. Na katika kusubiri huko nimekuwa nikiperuzi na kufanya research kupata neno muafaka la mada yetu, NIMEKOSA. Hivyo nakubali kutokubaliana nawe, na kuomba Ankoli arejeshe ukurasa wa kwanza post hii ili mjadala uendelee na tuweze kupata ukweli. Nisamehe kwa lugha kali niliyotumia awali, haikuwa nia yangu ila nilidhani wewe ni mmoja wao wa wale wanaopinga kila kitu mbele yao - kumbe sivyo.
    MDAU DAR

    ReplyDelete
  11. Nyie wadau wawili mnaorumbana mmenifurahisha kweli. Hivi ndivyo inavyotakiwa. sio kukosoa na kukashifu bila ustaalabu. Natumai admin atapandisha tena makala hii ili mjadala uendelee. hadi hapo naona ngoma droo. Ankal fanya mambo lete posti hii juu watu tujadili!!!!

    ReplyDelete
  12. Tunapojaribu kuhitimisha mjadala huu ambao kimsingi hatujahitimisha....hasa kwavile tunazidi "kukubaliana kutokukubaliana" inaonyesha wazi kuwa hata lugha ambayo Mdau Dar aliyoitumia mwanzo haikuwa mbaya, kwavile nia ilikuwa njema kama alivyosema yeye mwenyewe - mimi nampongeza sana kwa ukomavu huo!

    Aidha, nataka nikutie moyo Mdau Dar, kuwa mchango wako wa kwanza ndiyo uliofanya mjadala wetu huu uwe "live" zaidi....pamoja na hayo mie sina neno, na pia sijaona hasa neno linalohitaji "mtu asamehewe" ....Mdau...uwe na amani tu!

    MWISHO (angalau kwa sasa)-ikiwa wadau wengine watakuwa na jipya basi watuelimishe zaidi maana ya mada hii. Nami ntajaribu kuzidi "kudadavua" ikiwa kutakuwa na lolote jipya basi tutazidi kushirikishana ndani ya "Blogi hii ya Jamii"

    Ankal - napenda nikupongeze kwa dhati sana jinsi ulivyoonyesha unyenyekevu na kukubali kurudisha mada hii...moyo kama huu unadhihirisha kuwa wewe unazo sifa za "kiongozi mzuri"....unajua kiongozi mzuri anaweza akawa na sifa nyingi lakini mojawapo ni kuwa awe "mtumishi wa watu" na hapo kwenye utumishi kuna vitabia vingivingi utaviona vinajitokeza kama vile-unyenyekevu, uvumilivu, usikivu....n.k. naona niishie hapa nisije nikasababisha mada mpyaaa...Mdau Dar akapata mpenyo wa kupachika "bao" lingine!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...