Na Freddy Macha
Nimesalimiana na kusogoa kifupi na Mwalimu Nyerere, Rais Robert Mugabe (Dar es Salaam, 1978) na Rais Jakaya Kikwete. Vile vile nimekutana na kuwahoji washairi maarufu wa Kijamaika, Mutabaruka na Linton Kwesi Johnson; pia Ngugi wa Thiong’o wa Kenya, mtengenezaji sinema wa maisha ya Wamarekani weusi , Spike Lee, mwanariwaya wa Kizanzibari Adam Shafi na sasa Abdilatif Abdalla. Wote wana sifa moja. 

Mwandishi nikiwa na gwiji Abdilatif Abdalla, London 2013. Sifa gani? Muda wote nliokuwa naye Abdilatif hakuacha kufanya masihara,utani, kutafuta maana katika jambo hata liwe dogo kiasi gani. Tulipoingia mkahawani kupata chai, aliwasikiliza hata watu asiowajua wanasema nini, huku akijumuika kucheka au kutojitenga.
Hiyo tabia ya kuchanganyikana kila nukta na wanadamu wenzake na jamii, nimeiona katika kila mtu mashuhuri niliyempa mkono wa salamu. Mathalan, nlipokuwa na Mwalimu Nyerere mjini Rio De Janeiro mwaka 1991, tuliongea utadhani rafiki wa karibu sana.
Kawaida unapogongana na watu wa aina hii hukujia hisia kwamba wao ni wadudu wa sayari nyingine; lakini Mwalimu alikufanya ujisikie mtulivu kabisa kwa utani na matani. Hali kadhalika mwimbaji maarufu, marehemu Miriam Makeba (aliyefariki 2008).
Nilikutana naye London, mwaka 1987, akiwa na mjukuu wake. Nilivyomsalimia wala hakushtuka. Aliongea kwa upole na tabasamu. Tabia yake ilijaa upole, unyenyekevu na ucheshi wa mwanamke wa kitongoji chochote cha Afrika. Kubali au usipokubali mtazamo wao, watu maarufu- (waliofanya ya maana) huwa na hilo.
Hivi huyu mjamaika ilo jina la Mutabaruka alilipata wapi?je,ulimwuliza kama ana asili na watu wa Kanyigo au mitaa hiyo?
ReplyDeleteYaani Freddy Macha nakuonea wivu sana. Umekutana na mmoja wa washairi ninaowapenda sana Afrika ya Mashariki. Oh shairi lake la usiniue, kuhusu utoaji wa mimba lilivuma sana nilipokuwa kidato cha nne. (mama waniuliani?) inasikitisha sana siku hizi vijana wa kawaida hawatilii sana mkazo mashairi ( labda katika staili ya muziki wa rap tu) wanafunzi wa kawaida hawajui utamu wa mashairi. Oh nabwabwaja sasa maana umenifikisha mbali sana. Umenikumbusha Fumo Liyongo, Shaaban Robert na Kezilehabi( mwandishi wa Rosa Mistika na vitabu vingine vilivyotupa raha miaka ile, lakini nakipenda sana kitabu chake cha mashairi KICHOMI) Sikuonei wivu kwa kukutana na maraisi na hata spike Lee lakini Abdilatif Abdalla na Ngugi? Unatisha.
ReplyDeleteMdau uliyetaka kujua kuhusu Mutabaruka. Ukweli nilimuuliza kapataje jina hilo? Akasema ni la Kinyarwanda. Lina maana "mtu anayeshinda kila mara..." Jina lake la kubatizwa lilikuwa Alan Hope. Alilikataa zamani. Amekataa mambo mengi. Kwa mfano moja ya sifa zake ni kutovaa viatu kabisa. Nimewahi kukutana naye katika barafu za Ulaya, matope na mvua za Marekani ya Kusini. Havai viatu kamwe. Peku peku daima! Pia hanyoi nywele, hali nyama, havuti sigara wala bangi. Wala hali chakula mahotelini. Anapika mwenyewe au akisafiri ana mpishi wake maalum, kama alivyokuwa marehem Bob Marley. Mutabaruka hana unafiki, si mwoga; mkweli kwa vitendo na maneno.
ReplyDelete