Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe.
Bernard K. Membe (Mb.) atamwakilisha Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete kwenye
sherehe za kumwapisha Rais Mteule wa Madagascar, Mhe.
Henry Rajaonarimampianina zitakazofanyika nchini humo
tarehe 25 Januari, 2014.
Mhe. Membe ataondoka kwenda Madagascar tarehe 24
Januari, 2014. Mahakama Maalum ya Uchaguzi nchini
Madagascar ilimtangaza Mhe. Rajaonarimampianina kuwa
mshindi wa uchaguzi wa Urais tarehe 17 Januari, 2014.
Duru ya kwanza ya uchaguzi huo ilifanyika tarehe 31 Julai,
2013, ambapo hakupatikana mshindi. Katika duru ya pili
iliyofanyika tarehe 20 Desemba, 2013, Mahakama Maalum ya
Uchaguzi ilitangaza kuwa Mhe. Rajaonarimampianina alipata
asilimia 53.49 ya kura zote zilizopigwa huku mpinzani wake
Bw. Jean Louis Robinson akipata asilimia 46.51.
Kwa kushirikiana na wanachama wengine wa Jumuiya ya
Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) Tanzania,
ambayo ilikuwa mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na
Usalama ya SADC kwa mwaka mmoja ulioishia Agosti, 2013,
ilitoa mchango mkubwa kuhakikisha Madagascar inaendesha
uchaguzi wake katika hali ya amani na utulivu na kwa
kuzingatia misingi ya demokrasia, ili kumaliza mgogoro wa
kisiasa ulioibuka mwaka 2008 baada ya Bw. Andry Rajoelina
kuingia madarakani kwa kusaidiwa na Jeshi.
IMETOLEWA NA:
WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO
WA KIMATAIFA,
DAR ES SALAAM
23 JANUARI, 2014
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...