Na Mwandishi Wetu

Viongozi wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) wanachama wa Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) wanakutana mjini Addis Ababa, Ethiopia kujadili masuala mbalimbali juu ya utekelezaji wa utawala bora Barani Afrika.

Mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali ambao hufanyika kila mwaka mara mbili ikiwa ni kabla ya vikao vya AU, unalenga katika kujadili utekelezaji wa ripoti za utawala bora za nchi kadhaa zilizofanyiwa utafiti huko nyuma.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano katika Sekretarieti ya APRM Tanzania, Bw. Hassan Abbas, alisema mkutano wa safari hii wa viongozi hao ambao ni wa 20 utafanyika Januari 29 kwenye ukumbi wa mikutano wa AU mjini Addis Ababa, Ethiopia.

“Mkutano huu ni muhimu kwa sababu msingi mkuu wa APRM ni kuhamasisha na kuchagiza uboreshaji wa utawala bora katika nchi mbalimbali. Katika mkutano huu viongozi wa nchi za APRM watajadili namna baadhi ya nchi zilivyotekeleza changamoto zilizobainishwa huko nyuma,” alisema.

Alizitaja nchi za Afrika Kusini, Benin, Sierra Leone, Msumbiji na Burkina Faso kuwa zimepangiwa kuwasilisha ripoti zao za utekelezaji ili kuwaeleza viongozi wenza juu ya hatua walizochukua kutokana na mapendekezo waliyopewa awali na changamoto walizokumbana nazo.

“Mikutano hii huhusisha wakuu wenyewe wa nchi zote 34 za APRM ambapo hushiriki katika kubaini changamoto zinazozikabili nchi wenza na hivyo kushauriana juu ya namna ya kuzikabili lakini pia kubaini mambo ya kuigwa kutoka nchi wenza ili kujifunza na kuyachukua kuboresha utawala bora katika nchi zao,” alisema Bw. Abbas.

Akifafanua zaidi kuhusu Mkutano huo wa 20, Bw. Abbas alisema kuwa kwa mujibu wa ajenda za kikao zilizotolewa na APRM makao makuu yaliyoko Midrand, Afrika Kusini, nchi zaidi za Afrika zimeomba kujiunga na APRM na zitasaini mikataba.

“Kutokana na kuongezeka umuhimu wa APRM katika nchi mbalimbali za Afrika, tunayofuraha pia kuwajulisha wadau wetu kwamba idadi ya nchi wanachama wa APRM sasa itaongezeka kutokana na nchi zaidi kuomba kujiunga na zitasaini mikataba wakati wa mkutano huo,” alisema.

Tanzania ni miongoni mwa nchi 34 za Umoja wa Afrika zinazoshiriki katika Mpango wa APRM na tayari ilikwishakamilisha ripoti yake ya kwanza ambayo imeanza kufanyiwakazi kwa Serikali kutekeleza Mpango wa kuondoa mapungufu ya kiutawala bora yaliyobainishwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...