Baada ya Watanzania wa Ughaibuni na Watanzania wengine walioko Tanzania kuwakilisha maombi yao ya uraia wa nchi zaidi ya moja Serikalini na kwenye Bunge Maalumu la Katiba kumekuwa na Watanzania wengine waliodiriki kusema kuwa Watanzania wa ughaibuni ni wasaliti na hawahitaji kuwa Watanzania kwa sababu wameondoka nchini.
Sisi Watanzania tunaoishi ughaibuni tunatofautiana na kauli hii na hapa tutaonyesha kwa nini kila Mtanzania huku Ughaibuni anasema “Mimi ni Mtanzania.” 
 Watanzania wengi bado wanaamini Tanzania ni nyumbani kwao. Bado wana mapenzi na Tanzania. Bado wana ndugu Tanzania na bado wanamiliki mali Tanzania. Baadhi yao bado wanalipa kodi zinazotakiwa kwa mujibu wa sheria za nchi kutokana na umilikaji wao wa mali, ardhi na nyumba. Watanzania wa Ughaibuni bado wanafanya kazi kwa nguvu zote na sehemu ya mapato yao inaishia Tanzania. 
Watanzania hawa wanaamini kuwa wako ughaibuni kuboresha maisha yao kama ilivyo kwa raia wa nchi nyingine ambao uhama nchi zao na kwenda kuishi kwenye nchi nyingine. 
Kwa kifupi Watanzania wa ughaibuni sio tu waliohama nchi yao peke yao na hata huko waliko hukutana na raia wa mataifa mengine waliohama nchi zao. Sababu kubwa ya Watanzania wa Ughaibuni kuomba haki ya kubakia raia wa Tanzania ni kutokupoteza haki yao ya kuzaliwa Tanzania na kuwa karibu na ndugu zao pamoja na kuchangia maendeleo ya taifa lao. Pia bado wana uzalendo na mapenzi na Tanzania. 
 Kwa nini Watanzania wa Ughaibuni wanaliomba Bunge Maalumu la Katiba liingize haki ya uraia wa nchi mbili kwenye katiba mpya? 
 Sehemu ya 59 ya rasimu ya pili ya Katiba ukurasa wa 23 inasema “… mtu yeyote mwenye asili au nasaba ya Tanzania na ambaye ameacha kuwa raia wa Jamhuri ya Muungano kwa kupata uraia wa nchi nyingine, atakapokuwa katika Jamhuri ya Muungano, atakuwa na hadhi kama itakavyoainishwa katika sheria za nchi.” 
Watanzania tunaoishi ughaibuni ambao bado tuna mapenzi na Tanzania tunapochukua uraia wa pili tunapoteza uraia wa Tanzania ingawa sisi hatupendi kuupoteza. Hivyo, kwa mapenzi tuliyonayo kwa Tanzania, sisi Watanzania tunaoishi ughaibuni tunaliomba Bunge Maalumu la Katiba kurekebisha kipengele hiki ili kiweke wazi kuwa Mtanzania hapotezi Utanzania wake kwa kupewa uraia wa nchi nyingine. 
Wengi wetu bado tuna mila, desturi na utamaduni wa Kitanzania. Na bado tunajisikia Watanzania na tuna ndugu Tanzania, ndugu ambao bado tunawapenda kwa moyo wote na ambao hatutaki kutenganishwa nao. 
 Kwa mfano, Waafrika wa Kusini kutoka Afrika ya Kusini kwa mujibu wa Katiba yao ya mwaka 1996 hawapotezi uraia wao. Katiba ya Afrika Kusini imeweka wazi katika sura ya pili inayohusu haki za binadamu kuwa hakuna raia atakayenyang’anywa uraia wake. 
 Mfano mwingine mzuri ni kutoka Kenya. Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, sura ya tatu sehemu ya 16 inasema raia wa Kenya wa kuzaliwa hapotezi uraia wake kwa sababu ya kupatiwa uraia wa nchi nyingine. Katiba hizi mbili za Afrika ya Kusini na Kenya zinatosha kabisa kutoa mwanga wa ni jinsi gani baadhi ya nchi za Kiafrika zinavyothamini raia

wake. 
Nchi hizi hazikubali kupoteza raia wake, kwa nini Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakubali kupoteza raia wake? Kumekuwepo na malalamiko ya kwa nini nyie mliojiripua mnataka kuwa Watanzania tena? Ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya Watanzania wanaoishi nchi za nje hawakujiripua bali walikwenda mashule na vyuo mbalimbali Ughaibuni na wakati wengine walikwenda kwa shughuli za kikazi na kifamilia. 
Hivyo madai ya kuwa wote wamejiripua sio ya ukweli na hayana msingi wowote. Na tunaiomba Serikali, Bunge Maalumu la Katiba na Vyama Vyote vya Kisiasa kuyapuuza madai haya yasiyo na msingi wowote kwani hayahusiani na Watanzania wote waishio Ughaibuni. 
Sisi Watanzania wa Marekani, tunaiomba Serikali, Bunge Maalumu la Katiba na Vyama vya Siasa kulipigia kura suala la uraia wa nchi mbili ili kuhakikisha linapitishwa na Bunge Maalumu la Katiba na linawekwa kwenye Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
Sisi Watanzania wa Ughaibuni tunapenda kuwahakikishia Watanzania wote tuko tayari kushirikiana na Watanzania wote kulijenga taifa letu na kuleta maendeleo endelevu ambayo yanafaida kubwa kwa kila Mtanzania. 
 Imeandaliwa na Deogratius Mhella, 
Katibu wa Vikao vya Jumuiya za Watanzania Marekani na DICOTA katika jitihada za Watanzania waishio ughaibuni kuelimisha umma kuhusu Watanzania wa ughaibuni na kuhusiana na suala zima la uraia pacha.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. The mdudu,anasema makundi yalio nje ya Tanzania yako matatu 1 kuna mabeach boyz na Mabaharia kitambo hawa nawaweka kundi moja tena naiomba serikali iwasaidie hawa watu coz wako katika wakati mgumu sn ukweli usiopingika wengi wao hawana Elimu coz walijisahau mmno na KURUKA MAJOKA ila mm the mdudu nimejalibu kuwafuatilia nikagundua bado wana UZALENDO MKUBWA na TANZANIA YAO ijapokua walijilipua nakuombeni watanzania msiwatenge hawa watu mkifanya hivyo mtakua mmewaokoa sn tena sn,,kundi la pili ni la WATT wa Vigogo na ndugu zao kusema na ukweli hawa wameukataa utanzania wao kwa makusudi coz hawana matatizo ya kiuchumi na bado hao hao leo hii wanautamani utanzania wao coz ugaibuni kwa sasa hakukaliki njaa mtu so hawa kwa mtazamo wangu sina cha kuwatetea ila niwakumbushe tu na ule msemo mkataa pema pabaya panamuita,,kundi la tatu ni lile la watu walioigeuka SERIKALI ambayo imetumia MAPESA ya walipa kodi wa kitanzania nakuwaleta huku ili iwaendeleze na MASOMO ya UTAKITARI na Mengineyo pasipo na aibu wala woga kwa makusudi wameigeuka serikali yao na nchi yao kiujumla na kuitukana nchi yao na serikali ili wapate URAIA wa ile nchi wanayosoma sasa hapa tujiulize wenyewe je WATU KAMA HAWA uzalendo kwa nchi yao uko wapi? Mpaka leo hii walilie huo UPACHA?,,kundi la mwisho kabisa hili lina wahusu WADOSI ukipenda ita WAHINDI hawa ndio walioinyea PASIPOTI yetu huku UGAIBUNI mfano hapa Uingereza watanzania miaka ile tulikua tunaingia bila ya VIZA cha ajabu hawa watu walikua wanaingia hapa uingereza kama siafu uwanja wa ndege waingereza wakiwauliza kwa nini umekimbia tanzania? Majibu yao ni hivi Tanzadia hapana nzuri ile mtu nyeusi taka uwa mimi,,umekaa kwa muda gani pale tz jibu ni hivi mm kaa pale maka moja tu,sasa waingereza walikua wajiuliza haya maswali yaani mtu amekaa MWAKA MMOJA TU na anapata PASIPOTI ndio sababu kubwa ya wao KUIWEKEA Tanzania VIZA na hao hao huku ndio wanaopigia debe la huo UPACHA ndugu zangu watanzania tuwe makini sn na watu kama hao,asanteni sn ni hayo tu kwa leo,the mdudu nimeamua kujibu mapigo ya hizo COMMENT ambazo hazina mashiko toka mwanzo wa HII KASHESHE,mungu ibariki TZ yetu.

    ReplyDelete
  2. Acha kelele...mimi niko hapa Djibouti...nataka uraia!!!!!!!!

    ReplyDelete
  3. Uraia pacha oyeeee! Tanzania oyeeee! Bunge la Katiba oyeeee! Watanzania wote Oyeee!

    ReplyDelete
  4. Tunawataka ndugu zetu wasipoteze Uraia wao. Mimi kaka yangu Yuko ughaibuni na Sitaki apoteze Uraia wake hivyo naunga mkono Uraia pacha.

    ReplyDelete
  5. Article hii nzuri sana. Ni kweli Sio wote wamejiripua. This makes sense na Mimi nadhani Watanzania wote tuna haki ya kuwa raia popote tulipo.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...