
Watanzania tuliopo Ughaibuni tunaendelea kuelimisha umma juu ya changamoto zetu na maombi yetu ya uraia pacha tunayowakilisha kwenye Bunge Maalumu la Katiba ili yafanyiwe kazi na ili yaingizwe kwenye katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Tunapenda kuelimisha umma kuwa sisi ni Watanzania licha ya kuishi ughaibuni na tunapenda ieleweke hatuna tofauti yeyote na Watanzania wengine. Bado tunaipenda nchi yetu na bado tuna uzalendo na tuna mapenzi na Tanzania.
Lakini vile vile kama Watanzania tuishio ughaibuni tuna changamoto zetu ambazo tungependa zifahamike na jinsi gani uraia pacha utakavyorahisisha maisha yetu na yale ya ndugu zetu na hata familia zetu zinanzoishi Tanzania. Hapa chini tutajadili changamoto zetu.
Watanzania wengi wanaoishi nje bado ni Watanzania na wengi wao wamejenga Tanzania licha ya kuwa na nyumba au makazi huku ughaibuni. Hivyo wengi hulipa kodi mara mbili yaani kodi za ughaibuni na kodi za Tanzania.

Ulipaji wao wa kodi unawafanya wapate mafao ambayo serikali za kigeni zimewatengea lakini bado hawapati mafao mengine mengi kutokana na sababu kwamba sio raia wa nchi hizo. Kwa mfano, huduma za jamii kama huduma za matibabu zinaweza kuwa za gharama kubwa kwa watu ambao sio raia wa nchi ya ughaibuni.
Na kama mnavyojua, ukiumwa ughaibuni sio rahisi ukachukua ndege na kukimbilia Muhimbili au Agakhan. Unahitaji matibabu pale pale ulipo na kwa haraka. Hivyo uraia pacha utawapunguzia Watanzania wa ughaibuni karaha kama hizi kwa wao kupata matibabu na huduma nyingine za jamii kama raia wa nchi ile wanayoishi na kupata huduma za jamii ughaibuni.
Watanzania wengine wamezaliwa kwenye diaspora na wana haki za kuwa raia wa nchi wanazozaliwa. Lakini bado raia hawa wana haki za kuwa Watanzania vile vile kutokana na wao kuwa na wazazi wa kuwazaa wa Kitanzania. Raia hawa tunawapoteza pale wanapochukuliwa na nchi za kigeni na kupewa uraia. Je sio jambo la busara kwa watoto wetu hawa au ndugu zetu hawa kuwa Watanzania?
Tutaendelea kuwapoteza kama raia mpaka lini?
Kinachoshangaza ni kwamba kuna utafiti ulifanyika Tanzania na Tume ya Katiba ya Mheshimiwa Jaji Warioba.

Utafiti uliridhia kwamba kuna mambo ya kuwekwa kwenye katiba na kuna mambo yakutokuwekwa kwenye katiba. Utafiti huo ambao baadhi ya wajumbe wa Tume ya Katiba ya Mheshimiwa Jaji Warioba waliridhia kuwa suala la uraia pacha lisiingizwe kwenye katiba mpya ila lipelekwe kwenye vyombo vya sheria likatungiwe sheria kwa maana ya kwamba suala hili ni suala ambalo hubadirika badirika.
Hivyo si rahisi kulibadirisha kama litawekwa kwenye katiba kwa sababu kubadirisha katiba ni kazi ngumu sana. Sisi Watanzania tunaoishi kwenye Diaspora tunapishana kauli na kauli hii kwa kusema kwamba sisi tunachoomba ni suala la uraia pacha liingizwe kwanza kwenye katiba halafu lipelekwe kwenye vyombo vya sheria ili likatungiwe sheria. Hii itampa kila Mtanzania na sio Watanzania wa ughaibuni kuwa na haki ya kimsingi ya kutoweza kuupoteza Utanzania wao katika mazingira yeyote.
Kuna baadhi ya watu waliodiriki kusema kuwa basi hawa Watanzania wa Diaspora basi wapewe “special privileges” tunawashukuru kwa kufikiria hivyo lakini wakumbuke kama tatizo la special privileges ni kwamba special privileges zinaweza kuondolewa saa yeyote au hata siku yeyote na hivyo bado Watanzania wa Ughaibuni watakuwa na wasiwasi kuhusu hatima yao ya maisha ya baadae.
Lakini kama katiba ikisema Mtanzania hapotezi uraia wake kwa namna yeyote ile au kwa kupewa uraia mwingine kwa mujibu wa sheria za nchi basi Watanzania wa ughaibuni hawatakuwa na malalamiko wala wasiwasi wowote kwa sababu hawawezi kupoteza uraia wao na mapenzi na nchi yao yatendelea kudumu bila kikomo.

Tatizo jingine ni kwamba Tanzania inapoteza wataalamu pale ambapo Wataalamu hao wanapochagua kufanya kazi katika nchi nyingine. Kwa mfano Tanzania imeshapoteza Madaktari Mabingwa, Mainjinia na Wasomi wengi tu. Kama wataalamu hao wangekuwa na uraia pacha bado wangetambulika kuwa Watanzania na wangeweza kabisa kushirikiana na nchi zao katika kusaidia kuleta maendeleo ya nchi yao Tanzania;
Wataalamu wa kitanzania na wanasiasa wamekuwa kwa muda mrefu sasa wakishindwa kutekeleza sera za kuimarisha diaspora ya kitanzania katika maeneo ya kijamii na ya kimaendeleo ya nchi ya Tanzania kutokana na kutokutambulika kwa Watanzania walio na uraia wa nchi nyingine.
Je huu sio wakati wa kubadilika na pande zote mbili kuanza kufanya kazi kwa pamoja?
Tunachokiomba Watanzania wa ughaibuni ni kila Mtanzania popote alipo asikilize kilio chetu na amwombe mbunge wake, mwakilishi wake na Watanzania wote waliingize suala la uraia pacha kwenye katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hilo ndilo ombi letu na sisi tupo tayari kuwa mabalozi wazuri wa kujenga Tanzania imara yenye amani na utulivu na yenye maendeleo kwa kushirikiana na Watanzania wote bila ya kujali tofauti zao za kiitikadi, kidini na kikabila. Tunawaomba wabunge wote wa Bunge Maalumu la Katibu kumpa kila ushirikiano mwakilishi wetu kwenye Bunge hilo Mheshimiwa Kadari Singo. Mungu ibariki Tanzania.
Mungu ibariki Afrika.
Imeandaliwa na Deogratius Mhella,
Katibu wa Vikao vya Jumuiya za Watanzania Marekani na DICOTA katika jitihada za Watanzania waishio ughaibuni kuelimisha umma kuhusu Watanzania wa ughaibuni na kuhusiana na suala zima la uraia pacha.
labda mfike mbinguni,ila kwa hapa ardhini mtamaliza dunia,mtafanya makongamano,warsha,semina,midahalo mpaka mtaandamana kama chadema hakuna kitu itachange.mkiwa na nia ya kusaidia mtasaidia , vinginevyo mtakuja tu kama watalii,shida iko wapi kwani?
ReplyDeleteWatanzania tuungane Wakati huu kupitisha Uraia pacha na kuuweka kwenye katiba.
ReplyDeleteUraia Pacha hatuwezi kufuata kwa kila ambacho nchi zingine duniani zinafanya!
ReplyDeleteTunaweza kuwapa nafasi mshiriki mambo hapa nchini Tanzania kama Siasa na Kupiga Kura, Uchumi na Uwekezaji.
Lakini SUALA LA UONGOZI MTATUACHIA SISI WENYEWE WATANZANIA WENYE NCHI WENYE PASIPOTI MOJA!
Hatuwezi kuishi maisha ya nchi zingine kama Uganda, Rwanda na Kenya ambazo zime weka utaratibu wa Uraia Pacha kwa sababu wanazojua wao na kwa shida zao lakini sio Tanzania.
ReplyDeleteTunaweza kuweka mazingira ya kushirikiana nanyi mkiwa na status na Uraia mlio nao kwa sasa, lakini suluhisho sio kupewa Uraia Pacha ili iwe kigezo cha kushiriki kwa kuwa imeonekana pana wanaopigia chapuo Uraia pacha kwa kufikia malengo yao binafsi kama Uongozi hapa Tanzania.
Watanzania hatuwezi kukubali kuongozwa na mtu ama watu waliokuwa na rekodi chafu ya Kuasi nchi kwa kuomba Ukimbizi nje na Kukana Uraia wa Tanzania.
Tanzania itabakia kuwa nchi ya Pasipoti moja tu.
Mlisha inyea sana Tanzania huko nje mkiomba Makaratasi ya sheria na Ukimbizi.
ReplyDeleteNa sasa ndio ninyi tena mnamgeukia Raisi Kikwete awape Pasipoti ya Pili?