MIMI NI MTANZANIA...

Mnhomo Gwa Nzunzu ni Mtanzania aliyezaliwa Sengerema, Mwanza. Baada ya kuzaliwa wazazi wake walifariki wakati yeye akiwa na miaka mitatu tu kutokana na ajali ya gari. Baada ya kufariki wazazi wake Nhomo Gwa Nzuzu alilelewa na bibi yake ambaye alimsisitizia sana apate elimu ili ajikombowe kimaisha. Kwa vile Nhomo Gwa Nzuzu hakutaka kumsikitisha bibiye aliamua maisha yake ni kitabu na kitabu na yeye.

Kutokana na juhudi zake za kujisomea Nhomo Gwa Nzuzu alifaulu darasa la saba na akachaguliwa kwenda Old Moshi kuanza kidato cha kwanza. Nhomo Gwa Nzunzu ni msukuma na kwa mara ya kwanza alikutana na utamaduni tofauti kabisa na ule aliouzoea.

Wakati yuko Old Moshi alijifunza mila za kichaga na hapo alikutana na kipenzi chake aitwaye Aika. Baada ya kumaliza kidato cha nne, Nhomo Gwa Nzuzu alchaguliwa kwenda Tambaza kuendelea na masomo ya kidato cha tano na cha sita. Dar es Salaama kwake ilikuwa kama New York maana hakuwahi kuishi katika mji mkubwa kama ule. Lakini aliendeleza usongo na akafaulu vizuri kidato cha sita na kupata “scholarship” ya kusoma Chuo Kikuu cha Bologna huko Italia.

Baada ya Miaka Mitano alipata shahada yake ya kwanza kwenye masuala ya uchumi na kupata tena bahati ya kuendelea na shahada ya pili huko London Uingereza pale London School of Economics. Baada ya kufuzu shahada yake ya pili, Nhomo Gwa Nzunzu alipata nafasi ya kazi Geneva na Umoja wa Mataifa kwa miaka mitatu.

Baada ya kukaa Geneva kwa miaka mitatu, Nhomo Gwa Nzunzu aliamua kurudi tena shuleni kuchukua shahada ya Udaktari wa Uchumi. Na alipata nafasi ya kwenda Johns Hopkins University huko Maryland, Marekani. Baada ya miaka mitano ya masomo Nhomo Gwa Nzunzu alihitimu vizuri masomo yake na sasa kwa kipindi cha miaka mitano anafanya kazi New York.

Ili aweze kuendana na kazi yake aliamua kuchukua uraia wa Marekani. Kwa sasa Nhomo Gwa Nzunzu ni Mmarekani kwa sababu Tanzania haimkubali tena kuwa yeye ni raia wa Tanzania kwa sababu alibadilisha uraia wake. Pamoja na kubadilisha uraia wake Nhomo Gwa Nzunzu bado anamtunza bibi yake aishiye Tanzania. Kisha mjengea nyumba na kila mwezi humpelekea hela za matumizi.

Swali la kujiuliza Je Nhomo Gwa Nzunzu ni Mtanzania au sio Mtanzania? Na kama sio Mtanzania ni kwa nini sio Mtanzania? Amefanya kosa gani la kunyang’anywa Utanzania wake? Kama yeye sio Mtanzania mbona ana upendo kwa bibi yake aliyemlea na bibi yake anampenda sana Nhomo Gwa Nzunzu. Mbona anasomesha zidi ya ndugu zake watatu wa Kitanzania? Mbona serikali inasema Nhomo Gwa Nzunzu si Mtanzania lakini bibi yake ansema Nhomo Gwa Nzunzu ni Msukuma? Je inawezekana Nhomo Gwa Nzunzu akawa msukuma na asiwe Mtanzania?

Watanzania wengi wanaoishi Marekani wana hadithi inayofanana sana na Nhomo Gwa Nzunzu. Wanaambiwa kuwa wao ni wasaliti na sio Watanzania. Ukweli ni kwamba Watanzania hawa wanajisikia kuwa Watanzania kwa asilimia mia moja licha ya wao kuishi majuu kwa miaka mingi. Je tunapowakataa Watanzania hawa mbona hatuikatai misaada ya kifamilia wanayoituma Tanzania. Kumbukeni Watanzania wa Ughaibuni hutuma dolla milioni 250 kila mwaka Tanzania kusaidia ndugu zao. Je kuna sababu ya kimsingi ya kuwakataa Watanzania hawa na kusema sio Watanzania?

Tunaliomba Bunge Maalumu la Katiba liliangalie suala hili na kulipa kipaumbele ili Watanzania waishio nje wasionekane wasaliti na waruhusiwe kuwa na uraia wa nchi waishizo ili waweze kuendelea na maisha yao kama kawaida na ili waweze kuitumikia Tanzania na nchi waishizo kama kawaida. Kumbukeni maisha ni pale ulipo Wachaga au Wahaya uhamia Dar ili wapate maisha bora. Kwa nini leo Mtanzania anayehamia Marekani au Msumbiji aonekane ni wa ajabu na msaliti? Tunaliomba Bunge Maalumu la Katiba likomeshe kasumba hii kwa kuruhusu uraia wa nchi mbili.

Imeandaliwa na Deogratius Mhella, Katibu wa Vikao vya Muungano wa Jumuiya za Watanzania Waishio Marekani na DICOTA.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 19 mpaka sasa

  1. Historia ya taifa letu ingekuwaje iwapo Mwalimu Nyerere angeamua kuchukua uraia wa Uingereza wakati alipokuwa masomoni, tulijadili suala hili kwa umakini Watanzania.


    Ukweli ni kwamba, Mtanzania anaweza kuishi, kufanya kazi, kumiliki mali, kufungua biashara, na kuwekeza kihalali ughaibuni bila kubadilisha uraia. Kwa yule aliyebadilisha uraia, pale atakapoamua kurudi anaweza kuomba tena uraia wa Tanzania.


    Kupata uraia wa nchi ya kigeni kuna faida zake nyingi sana, wingi wa faida hizo usitufanye tufumbie macho changamoto zake. Wakati sisi tunamezea mate uraia wa nchi za wenzetu, kuna wale ambao wangeupenda uraia wa nchi yetu.


    Kwa njia ya mfano mdogo, kuna raia wengi sana sana wa kigeni walioajiriwa, wanaofanya biashara, na waliowekeza Tanzania ambao kinachowazuia kuchukua uraia wa Tanzania ni kutotaka kupoteza uraia wa nchi walizotoka. Iwapo uraia wa nchi mbili utaruhusiwa, kutakuwa na miminiko mkubwa wa raia wa nje ambao watachukua fursa zaidi za kazi, biashara, na uwekezaki zilizopo Tanzania. Fursa zilizopo Tanzania kwa Mtanzania aliye nyumbani na yule aliye ughaibuni zitapungua kwa kasi.


    Kwa heshima kubwa, naomba tulijadili swala hili kitaifa na kwa kina.

    ReplyDelete
  2. Sasa kipi cha kushangaza hapo? Si mshaambiwa mchague utanzania ama umarekani? Bila shaka huyo bwana hakulazimishwa kuchagua umarekani. Kwani ukisalia kuwa mtanzania utaongezewa dhambi?
    Kama utaratibu ndio huo, hakuna haja ya kupindisha sheria kwa sababu ya maslahi ya wanaoutaka umarekani ama ujerumani.
    Vinginevyo hakuna haja ya kuwa na sheria ikiwa watu wataamka kesho na kugundua wana maslahi fulani, basi tubadili.

    ReplyDelete
  3. tumewaelewa wamekuelewa

    ReplyDelete
  4. Jamani rasimu ya katiba haijasema kwamba mtu huyo akija Tanzania anapaswa kuomba uraia. Akiwa Tanzania anakuwa mtanzania kwa asili. Tusomeni kwa makini ibara ya 59.
    Kwa uchache ni hivi "Bila ya kuathiri yaliyomo kwenye sura hii,mtu yeyote mwenye asili au nasaba ya Tanzania na ambaye ameacha kuwa raia wa jamhuri ya Tz kwa kupata uraia wa nchi nyingine,atakapokuwa katika jamhuri ya tanzania atakuwa na hadhi kama itakavyoanishwa katika sheria za nchi"
    Kwa maana hiyo hawa watakuwa watanzania kwa mujibu wa ibara ya 58 ya rasimu ya katiba.
    Hii ndio hatua na sera muafaka kwa sababu mtu ambaye ameukana utanzania kwa hiari yao hawawezi kulazimishwa kuwa watz bali kama wameukosa uraia kwa kuchukua uraia wa nchi nyingine bado watakuwa watz wakiwa ndani ya jamhuri ya tz kwa ibara ya 58.
    Mimi naona hapa rasimu imekaa vizuri bali changamoto ni pale mtu ambaye ameukana utanzania kwa ibara ya 58 atakuwa sio raia wa tz bali pale tu atakapokuwa ndani ya TZ.Swali ni JE KAMA MTU ATAFARIKI NJE NA AKAWA AMEUKANA UTANZANIA MAITI ITAKUWA YA RAIA WA TZ? Mtu kama atakuwa amefanya uharifu na akauliwa hali itakayoathiri ushirikiano na nchi nyingine tutaikubali maiti kuwa ni ya raia wa tz kwa mujibu wa ibara ya 59?
    Konta,
    +255657447858
    Dar es salaam,Tanzania.

    ReplyDelete
  5. Wadau naomba kuuliza jee huyo jamaa kamjengea Nyanya yake huko Sengerema ni halali kwa mgeni kumjengea nyumba mwanae au nduguye? kama ni halali au sio halali sheria inasemaje na nini kifanyike au tuwafungie kuleta misaada yao ili kuepuka madhara yanayo kisiwa na watanzania waishio TZ? Mimi nijuwavyo ni kwamba sheria za uraia katika nchi zinazo jiamini kiusalama ziko kwa aina tofauti. Kuishi nchini kusio punguwa miaka 5 na kuendelea inategemea na nchi, kuowa au kuolewa na raia halali wa nchi husika na kuishi nae bila kutoka kwa kipindi inchi husika itajiwekea (kwa mfano Denmark miaka 7 kupata kibali cha kuishi tena kwa kufanya mtihani wa lugha) kuomba uraia unatakiwa kufanya mtihani wa uelewa wa nchi kama vile history ya utawala ulivyokuwa huko nyuma ukipasi ndio uombe uraia. Sasa TZ wajiwekee sheria zao na wao ili waepuke mivutano, kwani itafika sehemu haki za binaadamu kuingilia kati na kushinikiza serikali zisizo wakubali raia wao zitengwe kimataifa na sisi tulivyo kuwa wadhaifu wa kujituma kwani tunaishi kwa kutegemea misaada itabidi tukubali sharti na hao tunao waita wasaliti wataingia kwa roho mbaya kuliko ambapo wangeruhusiwa kukubalika bila sharti lolote. Mie sio mtabiri naomba radhi. Mr Babu Misemo

    ReplyDelete
  6. Huyo aendelee kutuma hiyo hela Mwanza kwa bibi yake ahakikishe bibi ana nyumba nzuri kabisa yenye vifaa vyote halafu hela ya kila mwezi nayo atume. Hii tupende tusipende inachangia uchumi Mwanza. Kwa hali ya kwaida Bibi asingekuwa na income ya kuconsume vitu vyote anavyoweza sasa. Hii nawasaidia wenye maduka, na kuchangia kodi za bidhaa, na maendeleo ya Tanzania. Kutuma pesa ni wajibu wake awe mtanzania au asiwe tena, la sivyo atakuwa hana shukrani.Hakuna fahari kukaa pazuri wakati ndugu zako wanalala hoi.

    ReplyDelete
  7. huo mfano wa mawlimu uliotolowa hapo juu ni mzuri sana, Gwa nzuzu kapotoka , huwezi changanyanya utamaduni wa kisukuma na kimarekani , chagua moja ama umarekani ama utanzania utaeleweka vizuri.
    siku hizi tunalalamika sana mambo hayendi sawa ni kwa sababu hatuna uwezo wa kuona mamabo vizuri halafu tunajifanya wasomi na hivyo tunajua mamabo kumbe ukweli ni kwamamba hatujui lotote tunaendaenda tu na mambo yanavyotokea

    ReplyDelete
  8. Sheria ni Msumeno Wa_Swahili walisema.

    Kupanga ni Kuchagua wa-Swahili walisema.

    Kwa kuwa Mnhomo Gwa Nzunzu moyoni mwake ni Mtanzania lakini kwa nje muonekano wake ni Mmarekani kwa 'karatasi' hilo si jambo jepesi kukana uraia wako na kuuitia katika karatasi kuwa wewe ni Mmarekani lazima kuna jambo unapenda juu ya utaifa wako mpya.

    Wazee walisema 'Ukionacho nje ndiyo kipo Ndani' mfano umevaa mavazi ya namna Fulani basi tabia/moyo wako unafanana na mavazi yako yanavyoonekana.

    Yaani wewe kwa muonekano wako ni Mmarekani pasi bila shaka wewe siyo Mtanzania.

    Mdau
    Mzalendo Ughaibunu
    Visiwani Hawaii bahari ya Pasifiki

    ReplyDelete
  9. Hapo huyo jamaa aliamua kuchagua kuwa mmarekani na kuukana utanzania. Kwani angeendelea kuwa mtanzania kazi angefukuzwa? Au angekosa mambo flani ambayo sasa inaonekana ni bora hawe mtanzania?

    Huyu jamaa ataendelea kiwa mtanzania hila sio kwenye makaratasi kwani ameshaukana. Jamani tuangalie swala hili kwa upana wake. Kuhusu mambo ya usalama tu, je mtu kama huyu kama Tanzania inapangwa kuvamiwa na USA yupo teyari kutoa siri hizo?

    Hakuna mambo ya uraia wa nchi mbili, wazazi wetu wengi wamesoma na kufanya kazi huko mliko hila wakawa wazalendo kurudi na kuiendeleza Tanzania. Je mwalimu Nyerere angeukana utanzania ingekuwaje? Je Hayati Sokoine angeukana utanzania ingekuwaje?

    Hapa kunamaslai ya watu ndiyo maana hili swala linakomaliwa kweli kweli.

    ReplyDelete
  10. Naona majadiliano yanajaa jazba na hamasa. Wakati ni ukweli usioyakinika kwamba inabidi tuwe makini katika hili la uraia pacha.

    Mimi naliona kwa mapana kwamba si swala la uraia wa nchi mbili bali la kuweka sawa hitilafu za kihistoria haki za uzawa za raia wastahiki wa Tanzania.

    Hakuna mtu wala chombo chochote kitachoweza kunyang'anya haki ya uzawa. Hiyo ni ya milele. Lililopo ni lile la kutambuliwa kwa haki hiyo. Faida yake yaenda pande zote na iwapo litafanyiwa kazi, mapungufu yanayodhaniwa kuwepo yatatatuliwa.

    Haki yaendana na wajibu na hilo ndo la msingi. Nahisi tume ya Warioba ililiona hilo na ndo maana ikaacha wazi ili lifanyiwe kazi. Wajibu gani wapaswa kwenda na haki hii ya uzawa?

    ReplyDelete
  11. Wenzetu Wamarekani wanaangalia je mtu(au taifa) fulani ana faida kwao?(wanaita interest). Wantanzania inabidi waangalie je Watanzania waliopo Ughaibuni wanafaida kwa TZ?! Na nadhani wamefanya utafiti nakuona kweli wana faida. Jamaa wengi wanaongea na kutoa mifano ya ajabu ajabu na si ywa kweli. Mfano, Marekani hawakulazimishi ukane uraia wako ili uwe na wa kwao, bali ukiwa na uraia wao kuna faida nyingi, kama mikopo ya shule, kuingia nchi nyingi bila visa n.k Jamaa wengine hapa wanaingiza jina la Nyerere, kwamba kwa vile alisoma UK angechagua kuwa raia huko.PUMBA! Nakumbuka wakati Nyerere anasema kuwe na vyama vingi watu walipinga sana, kama hivi wanavyopinga huu uraia pacha. baadaye ilibidi tukubali kwani mabadiliko yalikuwa ni lazima(mataifa ya wakubwa yakisema yamesema).Halafu we jamaa uliyesema ilo Unajua kwamba wajukuu wa Kambarage wanasoma na kukaa Marekani?! Halafu sio kila MTZ amekana uraia wake kwa kuchukua uraia mwingine. Mfano mie, wazazi wangu walikuwa tayari wa taifa lingine,lakini nilizariwa TZ. lakini nilipofika miaka 16 nikapewa pass ya nchi nyingine. Miaka karibu 20, kila mwaka nakuja Bongo kumwoona bibi yangu, ndugu, jamaa na marafiki. Nimepeleka umeme na maji kwa bibi yangu kwa hela zangu, nasaidia kufundish shule, kuwaletea vifaa kama computers n.k Naleta wageni, tena kundi kama 20-50 wanakuja kutalii na kusaidia shule. Vile vile nina timu(mimi si Kajumulo)kwa hiyo inabidi nitume pesa kila mala. Je watu kama mimi tuna faida TZ? Mie uraia pacha upite usipite ni sawa tu, lakini nasapoti, naomba wengine waache kuongea madudu, fanya utafiti kabla ujaropoka. Ndiyo maana ya shule. Serikali, imefanya utafiti wa kufafanisha mataifa yaliyo masikini kama, Kenya, Nigeria, nakuona faida wanayopata toka kwa jamaa zao Ughaibuni. Na kweli Ughaibuni siyo Marekani na Ulaya pekee. TZ inabidi tuwe mstali wa mbele siyo nyuma kila siku.

    ReplyDelete
  12. Nadhani hapa watanzania tunachanganya mambo mawili tofauti. Kwanza ni kumuangalia mtanzania mwenzako aliyechukua uraia wa nje kuwa anajidai tu na hakuna sababu za msingi zilizosabasha yeye kuchukua uraia wa nchi hiyo. Sasa tunakomoana tu. Fikiria iwapo wewe una watoto unaishi Ulaya wanasoma utabidi kuwatafutia pasi za nchi ile mnayoishi. Kwa sababu hapa kuna utaratibu wa wanafunzi kusafiri na darasa kwenda katika nchi nyingine. Kuna kuwa na adha ya kutafuta visa. Isitoshe atatengana na wanafunzi wenzake kwa kuwa si raia wa eu kwa mfano.
    Pili kama unasafiri nao kuja tz kwa mfano itabidi pia mtengane uwanja wa ndege, na kama watoto ni wadogo sijui utafanyaje. Kwa hiyo kuna sababu nyingi zinazosababisha mtu kuchukua uraia wa nje. Tusikomoane kwa kudhani mtu anajidai tu.

    ReplyDelete
  13. Watanzania tuna haki ya kupewa uraia wa pili. CCM na Serikali walisharidhia. Sasa kilichobakia ni kumpitishwa tu na bunge maalumu la katiba. Tanzania oyee! Uraia pacha oyee!

    ReplyDelete
  14. Nadhani uraia wa nchi nyingine sio dhambi na sio kosa la jinai. Mi naunga mkono kwa yeyote atakayekubali kuwa raia wa nchi nyingine na bado akaendelea kuwa Mtanzania. Watanzania wengine wana mawazo ya kukomoana na wanataka tu kuwakomoa Watanzania wenzao wanaoishi ughaibuni bila ya kuwa na sababu muhimu za kimsingi. Sababu muhimu za kimsingi za kukataza uraia pacha ni nini?

    Nawasilisha. Na mimi binafsi naunga mkono suala hili.

    ReplyDelete
  15. Nadhani uraia wa nchi nyingine sio dhambi na sio kosa la jinai. Mi naunga mkono kwa yeyote atakayekubali kuwa raia wa nchi nyingine na bado akaendelea kuwa Mtanzania. Watanzania wengine wana mawazo ya kukomoana na wanataka tu kuwakomoa Watanzania wenzao wanaoishi ughaibuni bila ya kuwa na sababu muhimu za kimsingi. Sababu muhimu za kimsingi za kukataza uraia pacha ni nini?

    Nawasilisha. Na mimi binafsi naunga mkono suala hili la uraia pacha.

    ReplyDelete
  16. Uraia wa nchi mbili utaongeza opportunities za kazi na maslahi ya Watanzania. Hii itapunguza wauza unga na wawindaji meno ya tembo na vifaru maana hawa wote maisha yamekuwa magumu kwao hapa Bongo. Labda wakienda kwingine watafanikiwa kihalali halafu watawekeza Bongo!

    ReplyDelete
  17. Mimi ni mdau wa tosamaganga. Siioni shida iko wapi. Wapeni Uraia wa nchi mbili maana wakiwekeza na sisi tunapatamo!

    ReplyDelete
  18. Suala la uraia wa nchi mbili lifikiriwe kwani ndio mda wake. Wa-Tanzania tumepitia mapitio mengi, embu angalia suala la vyama vingi lilivyoanza, na jinsi tulivyokuwa waoga na wenye wasiwasi lakini hatimaye kumekwenda mbele. Embu kumbuka kung'atuka kwa Baba wa Taifa kulivyoleta hofu na mashaka kuhusu hatima ya Tanzania bila Mwalimu, lakini tuliyazingatia mafundisho ya mwalimu na tukakubaliana na hali hiyo na tukasonga mbele, na tena kujipatia sifa kem kem ndani na nje ya Tanzania na ulimwengu mzima. Embu ona pia suala la katiba mpya ya Tanzania lilivyopigiwa kelele kwa takribani miaka 20 na sasa wakati umekuja tunapambana. Hapa ndipo hoja yangu ilipo yaani ndaniya hilo la uraia wa nchi mbili kwa Wa-Tz, basi embu tulione suala la uraia wa nchi mbili ni la msingi na tuliweke kwenye katiba tusonge mbele maana sidhani kama kuna ambaye mpaka sasa hafahamu ni faida gani za kuwatumia wa-Tanzania walioko nje kujenga nchi yao na pia kudhamini U-Tanzania wao kwani hawana makosa waliyofanya kuwanyang'anya haki hiyo ya msingi. Nchi nyingi ziko mbele ni sisi tuu tunasua sua kuleta mabadiliko yanayotakiwa- tuache woga tuache kusita sita, tufikiri na kutekeleza mara moja kilio cha Wa-Tz hawa. BINAFSI NITASIKITIKA SANA KAMA HILI JAMBO LITAPUUZWA NA SERIKALI YETU kwa kutowekwa kwenye katiba yetu tukufu!

    Deogratius Mshanga

    ReplyDelete
  19. Jamani kwanza tunapotumia neno kukana kwa maana kwamba mtu amechukua uraia wa nchi nyingine tutakuwatunakosea. Huu unaitwa uraia pacha yaani badala ya mtoto mmoja unazaa mapacha... hii ni baraka au hasara? Naomba nitoe mfano wa nchi jirani ya Kenya, wenzetu wameukaribisha vizuri uraia pacha. Sasa Mkenya mwenye raia pacha akija Tanzania baada ya mambo ya Afrika Mashariki kukamilika, yeye atakubalika zaidi Tanzania kuliko raia wa Tanzania aliyechukua uraia wa ughaibui. Mtoto wa Mtanzania mwenye uraia wa ughaibuni aliyezaliwa mfano Marekani hakubaliki kabisa Tanzania kwa sababu mzazi wake alichukua uraia wa Marekani, badala yake mtoto wa Mkenya atakubalika zaidi Tanzania (baada ya Afrika Mashariki kuungana) kuliko mtoto wa kitanzania aliye na mzazi mwenye uraia wa marekani. Mimi nadhani ni uoga wa walioko nyumbani wanadhani watu walioko nje watakuja kuchukua kazi huko. Tazameni mifano ya wageni wengi walioko marekani ambao wamechukua uraia wa marekani, wao ndio wanaleta kazi nyingi nchini kwao pamoja na uwekezaji wa hali ya juu. Nchi zao zinanufaika kwa kodi, ajira, kusomeshwa pamoja na kupelekwa nje ili waje wachukue nafasi katika vilivyo wekezwa. Nchi kama Marekani inanunua vitu vingi nje, hii itafunfua milango mipya ya export toka nchini kwetu. Nadhani tuangalie sana, tutaona faida ni nyingi kuliko uoga unaosababishwa na upeo mfupi.Tuangalie pia nchi wenzetu waliokwisha lifikiria hili watafaidika wao kuliko sisi.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...