Nimetumia muda mwingi kusoma vipeperushi vya kitaalamu kuhusiana na suala linalojadiliwa sasa la uraia pacha katika Tanzania na Afrika kwa ujumla. Wakati nchi nyingi za Kiafrka zikionekana kuelekea katika mfumo wa uraia pacha Tanzania bado tuna kazi kubwa ya kuelimisha jamii kuhusiana na umuhimu wa sulala hili. Inawezekana kabisa suala hili linaweza lisipewe kipaumbele katika Bunge Maaumu la Katiba. Maombi yetu ni kuliomba Bunge hilo lijadili mada hii kwa undani na kwa mapana yake. Watanzania wengi wanaoishi kwenye diasopora husema “Mimi ni Mtanzania” kila mara wakiulizwa wao ni nani.
Rasimu ya pili ya katiba inazungumzia kuhusu masuala ya uraia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na rasimu hiyo inaelezea uraia wa Tanzania unapatikanaje. Lakini rasimu hiyo haizungumzii uraia wa Watanzania wanaoishi kwenye Diaspora. Suala ambalo Watanzania wa ughaibuni tunalipendekeza ni suala lifuatalo, kuwepo na muda kwenye Bunge Maalumu la Katiba ambao utatumika kujadili uraia wa Watanzania wanaoishi kwenye Diaspora. Hii ni katika kuhakikisha kuwa haki ya uraia wa Watanzania waishio kwenye Diaspora inatambulika na Watanzania wote.
Wote tunafahamu manufaa ya kiuchumi na kijamii yatakayoletwa na uwepo wa uraia pacha kwa taifa la Tanzania. Kama suala la uraia pacha halitaingizwa kwenye katiba hii mpya itachukua miaka mingi sana kwa katiba hii mpya kubadirishwa. Hivyo wakati ni huu wa kulijadili na kuhakikisha Wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba wanaliingiza suala la uraia pacha kwenye katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bado hatujachelewa na ndio tunaweza (“Yes we can”).
Kwa kumaliza nakuomba usome sehemu hii rasimu ya katiba  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2013 sehemu ya 38 inayosema:
“Kila raia ana haki ya kutambuliwa uraia wake na kwa mathumuni haya, mamlaka ya nchi itaweka utaratibu wa sheria utakawezesha wananchi kupata hati ya kuzaliwa, kitambulisho cha uraia wake bila upendeleo na ubaguzi wa aina yeyote, na pale panapohitajika, nyaraka za kumwezesha kusafiri.”
 Sehemu hii inaposema “kitambulisho cha uraia wake”- kitambulisho hicho hakijasemwa kama kitawahusisha vile vile Watanzania tunaoishi ughaibuni. Tunaomba sehemu iweke bayana kuwa ruksa kwa Watanzania wa ughaibuni kupewa kitambulisho hiko kwa maana na wao ni Watanzania. Kwa maana nyingine tunaomba kutokupoteza haki ya kuzaliwa Tanzania ambayo inatupa uraia wa Tanzania moja kwa moja. Angalia: http://www.katiba.go.tz/attachments/article/185/RASIMU%20(Final).pdf
Wakati huo huo, sheria ya uraia ya Tanzania ya mwaka 1995 kwenye sehemu ya 14 inasema:
“The Minister may by order deprive any person, other than a person who is a citizen by birth, of his citizenship of the United Republic if the Minister is satisfied that person has at any time while a citizen of the United Republic and of full age and capacity voluntarily claimed and exercised, in a foreign country, any right available to him under the law of that country, being a right accorded exclusively to its own citizens, and that it is not conducive to the public good that he should continue to be a citizen of the United Republic.” Angalia: http://www.refworld.org/docid/3ae6b5734.html
Katika katiba mpya suala hili litarekebishwa vipi?
Imeandaliwa na Dakta Anicetus Temba katika jitihada za Watanzania wanaoishi kwenye Diaspora kuelimisha umma wa Watanzania wenzao kuhusu suala la uraia pacha. Na imetafsiriwa na Deogratius Mhella, Katibu wa Vikao vya Jumuiya za Watanzania na DICOTA.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 15 mpaka sasa

  1. Kwa wana diaspora wote. Niseme nimefurahishwa sana na jinsi mnavyoweza kunukuu vifungu mbali mbali vya rasimu na katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
    Swali langu kuu ni hili.
    Mlipokuwa mnaukana utanzania na kuchukua Uraia wa sehemu mliopokuwa ni matuamini yangu kuwa vipengele vyote vya katiba ya Tanzania kuhusu uraia mlikuwa mnavitambua na kuvielewa kama mnavyoelewa sasa au zaidi ya sasa, lakini kwa nia binafsi na maamuzi yenu binafsi bila kushurutishwa mliamua kuacha Utanzania na kuchukua uraia mwingine mkifahamu fika faida mnazopata na hasara mtakazo pata.
    Kuchagua ni uwamuzi sahihi kabisa na hakuna anaewalaumu lakini vile vile baada ya kuona makosa yenu basi msitake kulazimisha umma wa Tanzania kufata mnayotaka nyinyi kwa wakati huu wa mabadiliko.
    Ukweli ni kuwa maisha na faida mlizositaka na matarajio yenu ya utaifa mpya haujatimia ama imekuwa sivyo kama matarajio yenu sasa mnataka yafuatayo.
    Uraia pacha-ili huku hampo na huko mlipo pia hampo (individual indecisiveness). Mtu wa aina hii ni hatari kuliko hata terrorist. Maana yake kubwa hana uzalendo wowote zaidi ya maslahi yake binafsi.
    Mtu wa aina hii sio mkweli daima na sio muadilifu daima. .
    Tanzania kama ilivyo ujerumani na matiafa mengine yenye tija suala la utaifa ni suala la uzalendo na uasili na sio matamanio na matarajio binafsi (opportunity & opportunistic tendencies) hivyo basi kuondoa watu wa aina hiyo wisio wazalendo na wasio waadilifu na mapenzi ya dhati kwa Tanzania uraia pacha hapa. Uraia pacha ni sawa na kuweka Taifa la kitanzania kwenye kapu la rehani na kuwanadi taifa na watu wake wote kwa speculators na opportunistic individual. HAITAKUBALIKA.
    SIWEZI KUSEMA KAMWE LAKINI SIO KWA SASA.

    ReplyDelete
  2. hao diaspora wanaojibu kuwa wao ni watanzania wanakosea.wanapaswa kujibu kuwa wao ni raia wa nchi fulani(kwa mujibu wa passport walizonazo) wenye asili ya tanzania.
    wao si watanzania kwa sasa kwa sababu hawana uraia wa tanzania, si waliukataa?wachague tu kumoja,tanzania au huko walipo.mambo yapo kweupeni kabisa.si lazima kuiga kila kinachofanywa na wengine.

    ReplyDelete
  3. Hili swala la uraia pacha limewasilishwa likifuata utaratibu uliopo wa kujadili rasimu ya Katiba Nikuomba Bunge la Katiba lisilitupe nje ya Katiba.

    ReplyDelete
  4. Nyie mnataka kula huku na huku hahah hilo ndio jibu la mheshimiwa rais wako. Wahindi ruksa wale huku na huku!! poleni

    Mdau

    ReplyDelete
  5. Yote tisa, kumi tutabanana humo humo ndani ya TZ,iwe na urai pacha au bila urai pacha.

    ReplyDelete
  6. East African,
    tafadhali usitumie maneno makali kama madai yako kwamba eti aliyechukua uraia wa nchi nyingine ni mtu hatari kuliko terrosist au gaidi. sidhani kama unamfahamu Mtanzania yeyote yule wa aina hiyo.

    mimi nimechukua uraia wa nchi nyingine, lakini napenda kukuhakikishia kwamba uamuzi huo haukuwa mrahisi kiasi hicho. nilikuwa na uwezo wa kuchukua uraia huo tangu mwaka 2009, lakini nilisubiri mpaka mwaka jana 2013.

    pia nilipochukua uamuzi huo siyo kwamba siipendi nchi yangu niliyozaliwa TANZANIA. nimezaliwa, kukua, na kusoma Tanzania. hakuna hata siku moja niliyowahi kujihisi siyo Mtanzania.

    nimeachana na uraia wa Tanzania ili niweze kusonga mbele kikazi, kielimu, na kitaalamu, huku ninakoishi. kutokuwa raia wa nchi hii kuna vikwazo fulani fulani katika masuala hayo niliyoyataja.

    binafsi sidhani kama uamuzi huo ni kukosa uzalendo au kutukuipenda Tanzania na watu wake.


    Binafsi ningependa unieleze ni katika mazingira gani unafikiri naweza kuidhuru nchi yangu Tanzania, ambapo baba,mama,dada,kaka,shangazi, na ndugu zangu wengine wanaishi.

    Mwisho, ningependa utufafanulie kwa mtizamo wako uzalendo ni nini, na unapimwa namna gani. Je, mafisadi wanaohujumu nchi yetu kila kukicha ni wazalendo kuliko mimi ambayo sijavunja sheria yoyote ile ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania?

    ReplyDelete
  7. Hata kama Urai Pacha unafadia za Kiuchumi lakini upande wa pili wa sarafu mtu wa kuwa na Uraia wa namna hiyo anakuwa ni kinyonga na hachelewei kubadilika anaangalia maslahi yake tu.

    Wasiwasi wetu kama Mdau anavyosema kiwango cha Uzalendo wenu kimeingia dosari kwa kuukataa Utanzani, mfano wewe Diaspora ukubaliwe Pasipoti 2 halafu uje Tanzania tukupe madaraka utakapo hamisha Fedha kwenda kwenye Pasipoti yako ya pili tutakupata vipi?, wakati ninyi mmesha onyesha mpo kimaslahi zaidi?

    Inaeleweka baadhi ya Mataifa huwakingia kifua watu wao wenye Uraia wao tunaogopa mtatuhujumu!

    Mfano ktk zoezi hilo la kuupoteza Utanzania kirahisi rahisi hivyo hamkuona kwamba siku moja Utanzania utakuwa na thamani tena?

    ReplyDelete
  8. Je mkitaka Uraia wa pili wa Tanzania tena mpo tayari kwenda Mfunzo ya JKT au Mgambo kwa miezi 6?

    ReplyDelete
  9. Dr. Temba na Ndg.Mhela,

    Kutokana na ninyi kuwa hamuaminiki na kuwa kiashiria cha Hatari mpo kama 'TIME BOMB' au 'TICKING BOMB' ni kuwa mtagesha mnapoona maslahi mbele basi mnaweza kufanya lolote lile kama jinsi mlivyo weza kuupoteza Utanzania kirahisi rahisi.

    Pana jamii zingine duniani mtu anapoondoka kwao akakaa nje tena bila sababu za kueleweka akitia mguu kwao anafikia Gerezani ama atashikiliwa na vyombo vya Usalama kwa muda na kuhojiwa kabla hajaachiwa.

    Inafahamika wapo waliokuwa na ukazi wa nje kwa sababu za kueleweka lakini wengi ukiwauliza watakupa sababu za Kiuchumi na hali ya shida iliyokuwepo Tanzania, hivyo sababu za namna hiyo ni za mtu dhaifu na wa kuogopa kwa sababu kujenga nchi kunataka watu wenye moyo na uzalendo.

    Makundi ya Diaspora:
    1.Wapo wanaokaa nje kwa Vibali vya Kudumu huko wakiwa bado ni Watanzania (HAWA NI WENZETU HATA MIMI NAPENDEKEZA WAFIKIRIWE URAIA PACHA)

    2.Wapo walioomba Uraia mwingine nje, ama wameachia hadi wameupoteza Utanzania (HAWA NI WA KUOGOPA KAMA UKOMA, NA SIO WENZETU)

    3.Wapo walioomba Ukimbizi kwa kudanganya wametokea nchi zingine (HAWA NI MATUTUSA ZAIDI SIO WENZETU KABISAAA)

    Tunaweza kuwafikiria watu wa Kundi la No.1 (WAKAZI WA KUDUMU WALIOPO KIHALALI NJE) kuhusu kuchangia ama kushirikiana nao KWA KUBADILI SERA 'POLICIES' NA KUWAPA MAZINGIRA RAFIKI KWAO KWA KUWA BADO NI WATANZANIA KUWAWEZESHA LAKINI SIO KUWAPA KUNDI No.2 na No.3 PASIPOTI YA PILI!.

    ReplyDelete
  10. Uraia wa Tanzania mliukana kwa tama ya maisha ya Majuu leo vipi tena?

    ReplyDelete
  11. wote mnaotoa maoni yenu hapa inaonekana kama mnauchungu sana na Watanzania wanaoishi nje ya nchi bila sababu za kimsingi. unadiriki hata kusema watanzania walio nje ya nchi watawahujumu, ha ha ha, wewe nani kuwaambia wenzako sio watanzania. Tatizo naloliona hapa ni 1. wivu wa kipuuzi, 2. kutokuelewa unachoongea 3. uoga wa wachache wanaoogopa competition (hasa viongozi)

    kwa kuongezea na kuwajulisha ndugu zetu watanzania wote, hakuna watanzania wenye uchungu na nchi ya Tanzania kama wanaoishi nje ya nchi, amini usiamin. wala rushwa na wahujumu wa mali za umma ni hao wanaishi hapo nchini na ndio wanao sambaza propaganda za kipuuzi.

    Hakuna mtu ana haki ya kumwambia mzawa yeyote eti sio mtanzania.

    Mzawa ni mtanzania mpaka atakapoamua mwenyewe hataki kuwa mtanzania tena. na asie taka kuwa mtanzania hawezi kupoteza muda wake kuongelea au kudai haki ya kuwa mtanzania tena.

    Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Africa!!!

    ReplyDelete
  12. Uraia pacha (Tanzania/Djibouti) ni rahisi kuupata!

    ReplyDelete
  13. Rafiki, hiyo ya 1995 inasema wale wasio wazawa (wahindi, warabu, wakongo, n.k.). We kama ulizaliwa TZ hamna mtu ana mamlaka ya kuchukua uraia wako.

    ReplyDelete
  14. Hii kesi ina tatizo liitwalo "conflict of interest." Kuna uwezekano wabunge kwa husuda zao wakatupilia mbali kwani wao binafsi hawafaidiki na uraia huo. Bongo afisa hufanya jambo limfaidishaye yeye binafsi, si taifa.

    ReplyDelete
  15. Kwa mimi ntaukana uraia wa tanzania panapo majaaliwa na sitarajii kuuomba tena au kurejea tz hata kwa matembezi.majambazi wengi wakisikia jamaa kaja toka ulaya hamna kulala.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...