Yamekuwepo malumbano na mada nyingi kuhusu uraia pacha na jinsi ilivyo muhimu kuwa na uraia pacha kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi, na hapa namaanisha siyo ughaibuni tu hata wale waishio nchi jirani zinazotuzunguka.
Pamoja na mada zote nzuri naomba kwa ruksa yenu turudi kwenye sheria yenyewe ya uraia Tanzania kama inavyojulikana kama (Tanzania citizenship Act no 6 1995). 
Katika mada yangu hii naomba tujikite hasa kwenye aina ya uraia unaotambuliwa na sheria hii pamoja na lengo la kutunga sheria hii iliyofanyiwa marekebisho mara kwa mara kulingana na mahitaji ya muda huo na mwanzo baada ya uhuru iliitwa Tanganyika Citizenship Ordinance 1961 na Zanzibar Citizen Decree. Mwaka 1964 ndipo Tanzania Citizenship Act ilipotungwa na kupewa no. 6. Mabadiriko haya yalikuwa yanafanyika kwa nia ya kuwabana walowezi, wahaini. pamoja na kuhakikisha usalama wa taifa changa la Tanzania kwa kipindi kile.
 Ndani ya sheria hii inatamka kuwa Tanzania itakuwa na uraia wa aina nne kama ifuatavyo: uraia wa kuzaliwa; uraia wa kuandikishwa; uraia tajinisi nauraia wa kurithi. Kwa muda huu naomba tujikite kwenye uraia wa kuzaliwa na maana halisi ya uraia huu. 
Hii ni haki ya kwanza ya msingi ya kila binadamu aipatayo mara tu anapozaliwa na hii haki inaambana na ulinzi na ustawi wa huyu binadamu .
 Haki hii unaipata hajali wazazi wako ni kabila gani, rangi gani au dini gani. Tunaposema huyu ni mtanzania tuna maana gani? Ni mtu yeyote mwenye sifa moja wapo hapo juu aidha kazaliwa, kaandikishwa, karithi au katajinisiwa. Sasa turudi kwenye kiini. Uraia pacha hapa ndipo mkanganyiko unapoanzIa, nini maana yake? 
Huyu ni mtu mwenye uraia wake wa asili na amepewa au anatarajia kupata uraia wa nchi nyingine kwa kujiandikisha Kwenye nchi anayoishi. Siku zote bila kuelewa historia ya wapi ulikotoka, uliko na unapotarajia kuelekea ni vigumu kutambua nia na madhumuni ya kila jambo . Kuhahama kwa binadamu kulikuwepo tangu enzi za Adam na Hawa. Kuhama huku ilikuwa ni kujitafutia riziki pamoja na maisha bora kwa binadamu wenyewe wanyama, ndege na hata wadudu hufanya tendo hili ila kuhama hama huku hakumfanyi mtu aache asili yake. 
Mifano ya wazi kabisa ndani ya nchi yetu tunaona wachaga, wahaya wanyakyusa, wamakonde na makabila mengine mengi yalivyohamia Dar es salaam lakini hatujasikia mchaga aliyehamia Dar ameacha kuwa mchaga anaendelea na asili yake. 
Siyo rahisi kumnyanganya asili yake eti kwa sababu tu anakaa kwa wazalamo na wadengereko . Vivo hivyo . Mkude akiwa mmarikani hataacha kuwa mlugulu hata muta akiitwa smith hataacha kuwa mhaya. 
 Katika sheria ya uraia iliyotajwa hapo juu imekuwa ikiwanyima haki hii ya msingi kabisa Watanzania waliokwenda nchi za inje kuchuma na kutafuta marisho mabichi ili kuwasaidia ndugu zao na Taifa kwa ujumla. Ieleweke wazi kuwa kondoo kuzaliwa zizi moja na mbuzi habadiriki kuwa mbuzi anabaki kuwa kondoo. 
Watanzania tunaoishi nje tunataka hii haki yetu ya msingi iwekwe kwenye sheria mama ya Katiba na itamke wazi kabisa kuwa mtanzania wa kuzaliwa yeyote na kizazi chake hawapotezi uraia wa Tanzania. Kwamba, hakutakuwa na mamlaka yeyote ndani na nje ya mipaka ya Tanzania ya kumvua uraia na haki zote. 
Manufaa ya kuwa na uraia pacha yamegawanyika katika nyanja zote za maisha kama mada zilizotangulia zinavoelezea.
 Imeandaliwa na Emil Muta, 
Mwenyekiti wa Watanzania wa Washington-Seattle 
katika jitihada za Jumuiya za Watanzania za Marekani na DICOTA katika kuelimisha umma kuhusu suala la uraia pacha.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Kondoo kuzaliwa kwenye zizi la mbuzi hawi mbuzi atabaki kuwa kondooo. Inamaana mnyarwanda akizaliwa Tanzania atabaki kuwa Mnyarwanda si ndio maana yako, au nimekuelewa vibaya??? Wadu naomba msaada wenu. Mhindi akizaliwa Tanzania atabaki kuwa Mhindi!!! Ninavyojuwa mie ni kwamba Mwaarabu akizaliwa na wazazi waliohamia Tanzania hawi Mwaarabu bali anakuwa MTZ UKIFUATA SHERIA MAMA YA MWAKA 1964, Mwalim Nyerere alileta hoja hiii ya uhaini na kuwavua uraia wabaya wake na ubinafsi wake wa roho ya uchoyo ndio umeleteleza yote haya, tunamlaumu hadi sasa kuwa alipokubali wahaini warudi inchini angetenguwa kauli ya kuukana uraia sidhani kama yupo mtu anaeweza kuukana uraia wake ikawa kweli umefutika haipo hiyo. Wewe hata ukijiita Mcanada utabaki kuwa mcanada kwenye karatasi tuuu na sijuwi kama hata ukimwambia mtu asiejuwa ucanada ni nini kama ataelewa kuwa wewe sio mwenzetu. Namaanisha kuwa hakuna atakaejuwa kama mimi nimebadili uraia bila ya mimi mweneyewe kukwambia. THAT'S MY POINT

    ReplyDelete
  2. Hili la uraia pacha linakubalika na wengi,watanzania lzima tukubali kubadilika ,tuangalie mabadiliko ya dunia leo hii wachina wanauza mitumba kariakoo baada ya miaka 10
    watapewa jina la watanzania wenye asili ya kichina,na watahakikisha kuwa kizazi cha RACE ya kichina bado kinazaliwa yaani awatakubali kabisa kuoana na wamatumbi

    ReplyDelete
  3. Kila muwamba ngoma huvutia upande wake.Mtoa hoja wavutia kwako,walio wengi ndani ya Tanzania wanavutia kwao na huyo Julius Nyerere alivutia kwake pia. Muono wa Jaji Warioba suala la Uraia si la kikatiba isipokuwa kwa mtizamo wake ni la kisheria.Lakini mdau ujuwe,hakuna sheria isiyotoa mwanya yaani loop hole.Kama na wewe ukiwa bingwa na wengine pia waweza kuutumia huo mwanya katika kupata unachokitaka ndani ya sheria. Kazi kwako au kwenu.Katiba haihitaji utata.

    ReplyDelete
  4. Emil watanzania wengi wanaelewa vyema kabisa kwamba watanzania wa kuzaliwa hawawezi kuhatarisha usalama wa Tanzania kama inavyoelezwa na wanasiasa wengi ambao wameamua kulifanya hili swala la uraia kuwa la kisiasa zaidi. Wengine hoja zao zimejaa chuki na wivu. Nimeshangazwa hata muheshimiwa rais pamoja na kusema kwamba uongozi wake umeanzisha na kusimamia mambo ya Diaspora, mara kwa mara akiulizwa hili swala amekuwa akisema nyie mnataka kula huku na huku. Nimekuwa nikijiuliza hawa wahindi wanaopewa uraia wa Tanzania kila kukicha ila hali wao ni raia wa India, UK, Canada na USA mbona hawaulizwi hili swala la kula huku na huku? Pinafsi naona ni chuki tu inatusumbua, dola tunazotuma nyumbani wazipenda na mheshiwa rais alipokuja Canada alituuliza kwanini hatutumi hela nyingi kama Kenya na Uganda? wenzetu wanajua wao bado ni raia wa nchi zao, sisi tunaitwa wakimbizi lakini hela zetu zinapendwa. Hi ni nini kama sio wivu?

    Mdau Canada

    ReplyDelete
  5. Kama wewe kweli ni Mtanzania ambaye kweli huna wivu wala kinyongo kwa Mtanzania mwenzako kuwa na uraia wa nchi mbili hata kumi akipenda basi mpe Ruhusa hiyo,tutaona nchi yetu na watanzania wakicheka na kujivunia matunda na maendeleo ya kweli.Tutakuwa mfano wa kuigwa Afrika mashariki na dunia yote. MTANZANIA WA KWELI UGHAIBUNI UOTA NDOTO ZA NYUMBANI TZ.Kumnyima haki yake si kumtendea haki.UWEZO NA NIA TUNAYO ILA NI WEWE TU.
    EEh MOLA WAFUMBUE MACHO WATANZANIA WALIOKO NYUMBANI. AMEN

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...