IDARA ya Uhamiaji Mkoa wa Mbeya inawashikilia wahamiaji Haramu 62 ambao
ni Wahabeshi raia wa Ehtiopia pamoja na Watanzania wawili wakituhumiwa kuingia
nchini kinyume na utaratibu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisinin kwake Afisa Uhamiaji
Mkoa wa Mbeya, William Bambanganya alisema watuhumiwa hao wote wameshafunguliwa
mashtaka ya kuingia nchini bila kufuata sheria huku Watanzania wawili
wakishtakiwa kwa kuhusika kuwasafirisha Wahamiaji haramu.
Alisema wahamiaji hao walikamatwa katika matukio mawili kutokana na
kupata taarifa kutoka kwa Watanzania ambao hawapendi vitendo vya kujihusisha na
usafirishaji wa Wahamiaji haramu kinyume na taratibu hivyo kukiwezesha kikosi
cha Uhamiaji kuwatia mbaroni kirahisi.
Alisema katika tukio la kwanza lililotokea Februari 8, mwaka huu ambapo
Jeshi hilo lilipokea taarifa kutoka kwa raia wema zikisema kuna wahamiaji
haramu katika moja ya Nyumba za wakazi wa kitongoji cha Mwaka katika Mji mdogo
wa Tunduma Wilaya ya Momba mkoani Mbeya.
Alisema baada ya kufika eneo la tukio walifanikiwa kuwakamata Wahabeshi
45 raia wa Ethiopia pamoja na Mtanzania mmoja aliyefahamika kwa jina la
Shukrani Sastoni wakiwa katika nyumba ya Elisha Mwazembe usiku majira ya
saa sita.
Aliongeza kuwa Mwenye nyumba hawakufanikiwa kumkamata ingawa Washtakiwa
wote walifikishwa Mahakamani na utaratibu wa kumtafuta mwenye nyumba bado
unaendelea huku hatua za kisheria za kutaifisha nyumba hiyo kuwa mali ya
Serikali zikiwa zinafanyika.
Alisema tukio la pili lilitokea Februari 11, Mwaka huu majira ya saa 11
asubuhi katika eneo la Mbozi ambapo Wahamiaji 17 raia wa nchini Ethiopia
walikamatwa wakiwa kwenye gari aina ya Noah lenye namba za usajili T 340 BUP
likiendeshwa na Lugano Albert.
Alisema mbinu iliyotumika ni Dereva wa gari hilo kutaka kusimama kwa
kificho katika moja ya nyumba iliyojitenga peke yake akidhani pana usalama bila
kujua nyumba hiyo inakaliwa na watu na kujikuta wakiwekwa chini ya ulinzi na
maafisa Usalama wa Taifa ambao ndiyo waliokuwemo kwenye hiyo nyumba.
Aliongeza kuwa tayari watuhumiwa hao wamefikishwa katika vyombo vya
sheria wakisomewa mashtaka ya kuingia nchini bila kibali huku Mtanzania ambaye
alikuwa ni dereva akisomewa mashtaka ya kuwasafirisha wahamiaji haramu kinyume
cha Sheria huku taratibu za kulitaifisha gari hilo kuwa mali ya Serikali
zikiendelea.
Afisa huyo aliongeza kuwa utaratibu wa kutaifisha mali au kitu
kinachohusika na Wahamiaji haramu utasaidia kupunguza wimbi la uhamiaji haramu
hapa nchini ingawa alikiri kuwepo kwa ongezeko la wahamiaji kwa kipindi cha
Mwezi huu ukilinganisha na Mwaka jana.
Alisema Februari 2, Mwaka huu walikamatwa wahamiaji 15 raia wa Burundi
ambao walifanikiwa kuwarudisha nchini kwao, na kuongeza kuwa Ofisi ya Uhamiaji
Mkoa wa Mbeya iko katika Mazungumzo na Uhamiaji Mikoa mingine ili kuangalia
mianya wanayopitia kabla ya kufika Mkoa wa Mbeya ambapo wanavuka mikoa mingi
kabla ya kufika.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...