Na Dixon Busagaga
wa Globu ya Jamii, Moshi.
Waandaaji wa mbio za Kilimanjaro Marathon wametangaza njia mpya
zitakazotumika kwa mbio za mwaka huu ikiwa ni hatua nyingine muhimu
katika mafanikio ya mbio hizo ambazo sasa zinaingia mwaka wa 12 tangu
kuanzishwa.
Njia mpya zimelenga kuboresha mwendo wa washiriki
barabarani na kuwafanya wafurahie zaidi mbio hizo zilizopangwa
kufanyika tarehe 2 Machi, 2014 mjini Moshi.
Akitangaza njia hizo mpya jana, John Addison, Mkurugenzi wa Wild
Frontiers, waandaaji wa mbio hizo alisema alisema:
"Tumeanzisha njia
mpya ili kuzuia msongamano wa watu wakati wa mbio kutokana na
kuongezeka idadi ya washiriki kila mwaka. Washiriki wa mbio ndefu za
marathon ya km 42, nusu marathon km 21, mbio ya walemavu na mbio ya
kujifurahisha ya Vodacom 5km Fun Run sasa hawatapishana tena
barabarani bali kila njia itatiririka katika muelekeo mmoja.
"Pia kutokana na mabadiliko haya washiriki watakuwa wameepuka kilomita
3 za mwinuko mkali kuelekea Chuo cha Mweka ambapo awali ndio palikuwa
mahali pa kugeuzia washiriki wa mbio za full marathon na nusu
marathon".
Mbio ya walemavu za Gapco ambazo zitakuwa na makundi mawili
tu mwaka huu ya kiti cha magurudumu (wheelchair) na baisikeli ya
mikono (handcycle) imefupishwa kutoka nusu marathon na kuwa kilomita
10 ili kutoa fursa kwa watu wengi zaidi kushiriki na njia sasa itapita
eneo tambarare na lenye kivuli.
Mbio ndefu za Kilimanjaro Premium Lager 42km Marathon zitaanza saa
12.30 asubuhi kutokea uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika na Biashara
(MUCCoBS) na kuelekea barabara iendayo Dar es salaam kwa kilomita kumi
na kurudia geti la ushirika halafu zitaenda kilomita 8 kuelekea
hospitali ya KCMC na kukata kushoto hadi Barabara ya Lema (Lema Road).
Wanariadha watatelemka na Lema Road wakitelemka kupitia shule ya ISM
halafu watamalizia na kipande tambarare cha Barabara ya Kilimanjaro na
kipande cha mita chache za barabara ya Sokoine kuelekea uwanjani.
Mbio za Nusu Marathon zitaanza saa moja kamili asubuhi kutokea MUCCoBS
na kupandisha kaskazini kuelekea hospitali ya KCMC kwa kilomita 8
ambazo ni sawa na ongezeko la mwinuko wa futi 250 kutoka usawa wa
bahari.
Halafu mbio hizo pia zitapita njia ya Lema Road na kurudi
uwanjani.
Addison alisema kuwa mbio za full marathon na nusu marathon zinapita
kwenye maeneo mbalimbali yenye vivutio na mandhari nzuri ya mji wa
Moshi na sehemu zenye mandhari ya mashamba ya kahawa na migomba jambo
ambalo pia litawavutia wananchi wengi kujitokeza kuwashangilia
wanariadha.
"Njia zote zitakuwa na vituo vya maji vya kutosha ili kuwafanya
wanariadha wafurahie mbio bila kushikwa na kiu muda wote wa mbio.
Vilevile, njia nzima itakuwa na madaktari na wauguzi wa kutoa huduma
ya kwanza pamoja na magari ya kutosha ya wagonjwa huku mamlaka husika
zikidhibiti usalama wa wanariadha barabarani. Madaktari wengine na
wauguzi wataukuwa uwanjani ambapo kutakuwa na zahanati ya dharula kwa
ajili ya huduma ya kwanza na kuchua misuli", alisema.
Mbio ya walemavu ya Gapco Disabled 10km Marathon itaanzia uwanja wa
MUCCoBS na kufata barabara ya Kilimanjaro halafu mpaka Lema Road na
kugeuza.
Addison alisema mbio za kujifurahisha za Vodacom 5km Fun Run zitaanzia
kwenye mzunguko wa YMCA upande wa barabara ya Arusha na zitaenda hadi
kwenye mnara wa saa halafu kupita Boma Road kuelekea mzunguko
(roundabout) wa barabara ya Arusha na mzunguko wa YMCA tena na
watapita Uru Road na kuingia uwanjani kupitia geti la mashariki.
Executive Solutions ni waratibu wa mbio za Kilimanjaro Marathon 2014
wakishirikiana na Riadha Tanzania, Chama cha Riadha Kilimanjaro na
Kilimanjaro Marathon Club huku zikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium
Lager (wadhamini wakuu), Vodacom Tanzania, GAPCO, Simba Cement, and KK
Security among others, Keys Hotel, TPC Sugar, TanzaniteOne, CMC
Automobiles Ltd, RwandAir, FNB Tanzania, UNFPA na Kilimanjaro Water.
Ramani ya njia itakayotumika kwa wakimbiaji wa mbio za kujifurahisha za Vodacom fun run.
Mkurugenzi wa mbio za Kilimanjaro marathoni 2014, John Bayo akizungumzia njia mpya ambazo wakimbiaji watazitumia mwaka huu.
Mabango mbalimbali ya wadhamini wa mbio za Kimatafa za Kilimanjaro marathoni tayari yameanza kuupamba mji wa Moshi.
Ramani ya njia itakayotumika kwa wakimbiaji wa mbio za Full marathon,half marathoni pamoja na mbio za walemavu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...