Na Asteria Muhozya, Dar es Salaam
Tanzania inatarajiwa kuwa, miongoni mwa nchi 150 zitakazoshiriki maonesho ya 53 ya Kimataifa ya madini ya vito na usonara yatakayofanyika Bangkok Thailand, kuanzia tarehe 25 februari hadi tarehe 1 Machi, 2014.
Kutokana na kuwa na hazina kubwa ya madini ya aina mbalimbali, Tanzania imealikwa kuwa miongoni mwa nchi zitakazo shiriki maonesho hayo yanayojulikana kama ‘Bangkok Gems and Jewelry  Fair’.
Akizungumzia ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo jana,   Kamishna wa Madini, Mhandisi Paul Masanja alieleza  kuwa, Tanzania inatarajia kuyatumia maonesho hayo kukuza ushirikiano kati ya Tanzania na Thailand katika biashara ya vito na usonara, kutangaza madini ya vito yanayopatikana hapa nchini, kutafuta masoko mapya ya biashara na bei za uhakika katika tasnia ya madini ya vito, kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna ya kusimamia na kukabiliana na changamoto zilizopo katika tasnia ya madini ya vito na usonara hapa nchini ikiwemo pia kukubaliana maeneo ya kushirikiana.

Aidha, aliongeza kwamba, maonesho hayo yatasaidia Tanzania kujifunza uzoefu wa kuandaa maonesho ya Kimataifa ya vito na usonara ili kuboresha maonesho ya ‘Arusha Internal Gem, Jewelry and Minerals Fair’ (AIGJMF) yanayofanyika nchini kila mwaka.
Mkurugenzi wa idara inayoshughulikia kuthamini Almas na madini mengine ya Vito, ‘Tanzania Diamonds and Gemstones Valuation Unit’, (TANSORT) Bw. Archard Kalugendo, ameongeza kuwa, ushiriki wa Tanzania vilevile unalenga kuwavutia wanunuzi na wauzaji kununua bidhaa hizo moja kwa moja nchini badala ya manunuzi kufanyika katika nchi na miji mengine mathalan Tanzanite ambayo kwa sasa inanunuliwa kutoka Hongkong, Mumbai na Afrika Kusini, na madini ya Almas  kutoka India, Dubai na Antwerp.

Aliongeza kuwa, ushiriki huo, utaiwezesha Tanzania kupata nafasi ya kutangaza fursa mbalimbali za uwekezaji hususan katika madini ya vito yanayopatikana hapa nchini, kutoa taarifa za tafiti mbalimbali, ugunduzi mpya na kuelezea mipango endelevu iliyopo katika sekta hiyo.

Aidha, mbali na ushiriki wa Wizara, Tanzania itawakilishwa na  Shirika la Madini Tanzania (STAMICO), Kampuni sita za wafanyabiashara wa madini za Isle of Gems, Suju Gem Ltd, Tom Gems, H.B Mining Ltd, Swala Gems Traders, Gems and Rock Ventures. Aidha, kutakuwa na uwakilishi wa shirikisho la wachimbaji Tanzania (FEMATA), (TAMIDA) na kampuni nyingine za madini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...